ANGALIA LIVE NEWS

Wednesday, January 26, 2011

Bodi ya Mikopo ‘yapasua jipu’

Image
Mkurugenzi Mtendaji wa Bodi ya Mikopo ya Wanafunzi wa Elimu ya Juu, George Nyatega akizungumza na waandishi wa habari (hawapo pichani) Dar es Salaam. (Picha na Yusuf Badi).
BODI ya Mikopo ya Wanafunzi wa Elimu ya Juu (HESLB) imeshutumu kile ilichoeleza kuwa ni kugeuzwa jimbo la uchaguzi na baadhi ya watu, kwa kutumia mgongo wake kutoa shutuma bila kuzifanyika uchunguzi, ili wasikilizwe na wanafunzi wa elimu ya juu. 


Mkurugenzi Mtendaji wa Bodi hiyo, George Nyatega, jana aliwambia waandishi wa habari Dar es Salaam, kwamba Bodi yake imekuwa ikigeuzwa ajenda na watu hao huku ikihusishwa moja kwa moja na migomo ya wanafunzi wakati kasoro nyingi zinachangiwa na vyuo vyao na Tume ya Vyuo Vikuu (TCU).

Nyatega alisema lengo lake si kujibu tamko la Umoja wa Vijana wa Chama Cha Mapinduzi (UVCCM) ambao hivi karibuni ulitoa tamko kutaka Bodi ipanguliwe.

Lakini taarifa ya maandishi iliyogawiwa kwa waandishi na pia kuchapishwa katika baadhi ya magazeti jana, Mkurugenzi Mtendaji aliijibu UVCCM kwa kusema imekurupuka kwa kutoa shutuma ambazo hazijafanyiwa uchunguzi.

“Bodi inapenda kusisitiza, kwamba hata kama ikivunjwa, kama kiongozi mmoja wa UVCCM
walivyokurupuka kusema, hata chombo kitakachoundwa badala ya Bodi nacho itabidi kivunjwe baadaye endapo changamoto zinazosababishwa na wadau wengine na si Bodi ya Mikopo, hazijapatiwa ufumbuzi,” ilisema sehemu ya taarifa hiyo.

Alisema suala la Bodi kutumiwa kisiasa halikuanza leo wala jana, bali ni la muda mrefu kwani hata Serikali za Wanafunzi katika kujinadi ili zikubalike, zimekuwa zikitumia mgongo wa HESLB kushawishi wanafunzi wenzao .

Nyatega ambaye alikiri kukosekana ushirikiano mzuri kati ya Bodi, TCU na vyuo vya elimu ya juu ya utoaji mikopo kwa wanafunzi, alivitupia lawama zaidi vyuo vikuu vya umma, kuwa
vimekuwa vikiingiza Bodi yake kwenye lawama zisizo za msingi kutokana na kutofanya kazi yao ipasavyo.

Alisema, “taasisi nyingi za elimu ya juu ambazo wanafunzi wao wanakopeshwa na Bodi zimekuwa zikichelewa kuleta taarifa muhimu zikiwamo orodha za wanafunzi wa mwaka wa kwanza waliosajiliwa, matokeo ya mitihani na orodha ya majina ya wanafunzi wanaokwenda katika mafunzo kwa vitendo.

“Matokeo ya kucheleweshwa kwa taarifa hizo, yameibua malalamiko miongoni mwa wanafunzi na hivyo kuelekeza shutuma kwenye Bodi bila sababu za msingi,” alisisitiza.

Alisema licha ya Bodi kuwa na hati ya makubaliano na vyuo juu ya mambo kadhaa, lakini bado upo upungufu katika kutekeleza.

Alitoa mfano, kwamba katika makubaliano hayo, vyuo vinapaswa kuleta orodha ya wanafunzi wa mwaka wa kwanza waliosajiliwa ndani ya siku 30, lakini vyuo havizingatii hilo.

Kuhusu TCU, mtendaji huyo wa Bodi alisema pia imekuwa ikichelewesha taarifa za wanafunzi waliodahiliwa ili waandaliwe mkopo wao.

Alitoa mfano, kwamba zipo taarifa ambazo Bodi ilipaswa kuzipokea Novemba mwaka jana, lakini majina yaliletwa mwezi huu.

Alitoa mifano mingine ya vyuo ambavyo vilikumbwa na migomo na maandamano huku Bodi ikitajwa kuwa chanzo, kikiwemo Chuo Kikuu Kishiriki cha Elimu Mkwawa (MUCE) na kusema chuo hicho kilishindwa kuwasilisha namba za akaunti za wanafunzi kwa wakati na hivyo kusababisha ucheleweshaji kwa zaidi ya wiki tatu.

Kwa upande wa Chuo Kikuu Kishiriki cha Elimu Dar es Salaam (DUCE) ambacho wanafunzi waligoma hivi karibuni, chuo kiliwasilisha orodha ya majina kikiwa kimechelewa mwezi mzima. Wakati huo huo kiliwasilisha majina bila namba za akaunti.

Juhudi za kumpata msemaji wa TCU ili atoe maelezo juu ya shutuma hizo za Bodi hazikuweza kuzaa matunda kutokana na simu yake kutopatikana.

Katika hatua nyingine, Waziri Mkuu Mizengo Pinda, ameitaka Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi kuwa karibu na vyuo vya elimu ya juu, ili kutambua na kutatua migogoro inayozuka mara kwa mara.

Aidha ameitaka Kamati ya Wabunge iliyoundwa kwa ajili ya kuchunguza mgogoro uliozuka hivi karibuni katika Chuo Kikuu cha Dodoma (UDOM), kutoishia chuo hicho pekee bali itembelee na kuchunguza migogoro ya vyuo vyote vikuu nchini.

Akizungumza na waandishi wa habari mara baada ya kumaliza semina ya wabunge wa CCM Dar es Salaam juzi usiku, alikiri kuwapo kwa matatizo mengi katika vyuo hivyo, ambayo yamekuwa kero kwa wanafunzi na wahadhiri na hivyo kuzua migogoro ya mara kwa mara.

Alisema uongozi wa wizara hiyo, hauna budi kutembelea menejimenti na uongozi wa wanafunzi na kuwa nao karibu ili kuelewa matatizo yaliyopo badala kutokea tatizo, wizara iegemee taarifa ya kuambiwa na si kushuhudia.

Alisema kimsingi matatizo ya vyuo vikuu ni changamoto kubwa kwa Serikali na mengi yametokana na ongezeko kubwa la wanafunzi mwaka hadi mwaka, wakati bado miundombinu ya shule ikiwa haitoshelezi.

“Changamoto tuliyonayo ni kuendana na idadi ya ufaulu wa wanafunzi kwani ongezeko ni
kubwa na miundombinu ni ile ile na wakati mwingine inafikia chumba cha kulala wanafunzi wawili hulala sita, tatizo hili pia huwa ni kero na kuchangia migogoro vyuoni,” alisema.

Alisema pia tatizo lingine ni ufinyu wa bajeti ya mikopo kutokana na idadi kubwa ya wanafunzi ambapo pia mfumo wa utoaji mikopo nao umekuwa ukichangia kutokana na kulalamikiwa hali ambayo imeilazimu Serikali kuunda Tume kuchunguza mfumo huo na kuona namna ya kuuboresha.

Waziri Pinda alisema matatizo mengine yanahusu uongozi wa vyuo hivyo kwa upande wa wanafunzi lakini pia wahadhiri.

“Kwa hapa tutajipanga kuhakikisha tatizo linajulikana na kuwekwa wazi, ndiyo maana tunasisitiza Kamati ya Taaluma iliyoundwa ishughulikie pia masuala ya utawala katika vyuo hivi.
                                                                                                               Chanzo:HabariLeo

No comments: