ANGALIA LIVE NEWS

Tuesday, January 25, 2011

Marekani kuisaidia Tunisia kutanzua mzozo wa kisiasa-VOA

Waandamanaji Tunisia wamelala mbele ya jengo la waziri mkuu.
Utawala wa rais Obama umempeleka mjumbe maalum huko Tunisia, kusisistiza uungaji mkono wa Marekani katika juhudi za nchi hiyo kubadilisha mfumo wa serikali kutoka ule wa kimabavu na kuwa wa kidemokrasia.
Mjumbe huyo Jeffrey Feltman, ambaye ni naibu waziri wa mambo ya nchi za nje kwa ajili ya masuala ya Afrika Magharibi na Mashariki ya Kati, atasisitiza hamu ya Marekani katika kupatikana matokeo ya amani na ya kidemokrasi, baada ya mzozo wa kisiasa uliomng’owa madarakani rais Zine el-Abidine Ben Ali.

Majuma kadhaa ya maandamano na ghasia, zilimpelekea  Ben Ali kutoroka na kwenda uhamishoni hapo Januari 14, baada ya kutawala nchi hiyo kwa miaka 22.
Ghasia zimeendelea, na waandamanaji wakitaka viongozi wengine kutoka serikali hiyo ya zamani, kuondolewa kutoka serikali mpya ya mpito.

Akitangaza kazi za Bw. Feltman, masaa kadha kabla ya kuondoka kuelekea Tunis, msemaji wa wizara ya mambo ya nchi za nje, P.J Crowley alisema, waziri huyo mdogo atajaribu kutathmini binafsi hali ya mambo ilivyo, na kuieleza serikali mpya ya mpito juu ya jinsi Marekani inaweza kuwasaidia katika kujenga demokrasia iliyothabiti.
Amesema “tunaunga mkono serikali ya mpito inayopangwa, na tunatumaini kipindi cha mpito kitakua cha amani. Tunafahamu kuwa jamii ya kiraia imetoa hoja juu ya umbo la serikali. Ni wazi kuwa baada ya miongo ya kutokuaminiana, kuna maswali ambayo raia wanaendelea kuuliza. Serikali nayo inajaribu kuyajibu. Tunafahamu kuwa hili ni jambo gumu. Na tunajuwa kuwa serikali mara kadhaa itafanya makosa inapoendedlea mbele.”
Waziri wa mambo ya nchi za nje wa Marekani Hillary Clinton, katika mazungumzo kwa njia ya simu na waziri mkuu wa Tunisia Mohammed Ghannouchi siku ya Jumamosi, alisifu juhudi za serikali ya mpito kutaka kufanya uchaguzi katika muda wa miezi 6, na hatua za mwanzo za kutaka kuchunguza ulaji rushwa na ukiukaji wa haki zilizotendeka siku za nyuma.
AP
waandamanaji wakiwataka viongozi wa zamani kuondoka
Bw. Ghannouchi ameshikilia wadhifa hiyo tangu mwaka 1999 na yeye pia amelengwa na waandamanaji, kutoka vyama vya wafanyakazi na makundi mengine, yanayomtaka aondoke madarakani.
Bw. Crowley amesema maafisa wa Marekani wametiwa moyo na hatua zilochukuliwa na serikali ya mpito kuanza mazungumzo na makundi ya kiraia, kuwaachilia wafungwa, na kuondoa vikwazo dhidi ya vyombo vya habari. Hata hivyo anasema bado kuna kazi nyingi zinahitaji kufanywa.
Alisema sehemu ya ziara ya Bw. Feltman itakuwa ni kutathmini jinsi Marekani itakavyoweza kusaidia utaratibu wa uchaguzi huko Tunisia. Pengine kupitia msaada wa kiufundi kutoka makundi yasiyo ya kiserikali ya Marekani ambayo yamejihusisha sana katika juhudi za kuleta demokrasia katika sehemu nyingine za dunia.

No comments: