ANGALIA LIVE NEWS

Thursday, February 3, 2011

CUF yalia na CHADEMA-Majira

[Civic United Front]
*Yashutumu kuwatenga katika Kambi Rasmi Bungeni
*Yadai CHADEMA na wabaya wao watakufa na kuiacha


Na Rabia Bakari

CHAMA cha Wananchi (CUF) kimedai kuhujumiwa na Chama cha
Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) kutokana 'kauli za kichochezi' zinazotolewa dhidi yake kuhusu sababu za kukataa kushirikiana nao bungeni.

Akizungumza na waandishi wa habari jijini jana, Naibu Katibu Mkuu wa CUF, Bw. Julius Mtatiro alisema kuwa licha ya kuhujumiwa na CHADEMA lakini pia wanasikitishwa na kauli zilizotolewa na Katibu Mkuu wa CHADEMA Dkt. Wilbroad Slaa kwa kudai kuwa CUF sio chama cha upinzani nchini.


"Tunasikitishwa na kauli hiyo ya Dkt. Slaa na nikimnukuu anasema kuwa 'CUF siyo chama cha upinzani Tanzania tena, eti kwa sababu kiko serikalini Zanzibar' na kwa hiyo CHADEMA hawawezi kushirikiana na CUF katika kuunda kambi ya pamoja bungeni.

"CHADEMA wanaishambulia sana CUF hivi sasa, wanataka kuwaaminisha Watanzania kuwa kitendo cha CUF kuwa katika Serikali ya Umoja wa Kitaifa Zanzibar ni dhambi kubwa mno na kuwa Watanzania wasiiunge mkono CUF Tanzania bara, jambo ambalo ni ndoto za alinacha na kamwe halitatokea kwani Watanzania wa sasa hawadanganywi kwa propaganda zisizo na maana,"aliongeza.

Kauli ya Bw. Mtatiro inatokana na Tamko la Kamati kuu ya CHADEMA lililotolewa na Dkt. Slaa, kuwa CC ya chama hicho imemuagiza Kiongozi wa Kambi ya Upinzani bungeni, kuunda baraza kivuli kwa kuhusisha wabunge wa CHADEMA pekee.

Akitoa tamko hilo, Dkt. Slaa alisema: "Kamati Kuu imeendelea kuzingatia umuhimu wa vyama vya siasa kushirikiana katika kuimarisha nguvu ya upinzani hapa nchini. Hata hivyo, kamati kuu imezingatia kuwa Chama cha Wananchi (CUF) wamejiunga na CCM kuunda Serikali ya Umoja wa Kitaifa Zanzibar.

"Na kwa kuwa sheria inayoruhusu uwepo wa vyama vya siasa inahusu pande zote za muungano na kwa kuwa vyama vingine vya upinzani vyenye wabunge vimo katika ushirikiano na CUF, Kamati Kuu imeona kuwa CHADEMA haiwezi kuwa na ushirikiano wenye tija na vyama hivyo.

"Sasa kwa mfano tukiazimia kitu kinachopingana na serikali, Katibu Mkuu wa CUF ambaye ndiye Makamu wa kwanza wa Rais huko Zanzibar unategemea atakubaliana nacho ili apingane na serikali, hivi vyama vingine navyo tayari vimeshakuwa sehemu ya watawala maana wameamua kushirikiana na CUF katika kamati yao," alisema Dkt. Slaa.

Akizungumzia maazimio hayo, Bw. Mtatiro alisema kuwa CUF haiwezi kuwalamba miguu viongozi wa CHADEMA kwani hakuna faida yoyote wala umuhimu ambao wao wameonesha tangu walipojaribu kila namna kuwafanya wafanye kazi kwa umoja na vyama vingine na kugonga ukuta.

"Mara zote CHADEMA wamekuwa na historia ya kuvisaliti vyama vingine vya upinzani huku wakikimbilia kwa umma kuomba waungwe mkono wao peke yao," alidai.

Aliongeza kuwa CHADEMA kina matatizo mengi sana tangu mwaka 2007, na waliwavumilia kwa kiasi kikubwa na hata baada ya uchaguzi mkuu kuisha mwaka jana, CUF iliiomba CHADEMA iweze kushirikiana na vyama vingine vya upinzani ili kuwa na kambi ya upinzani imara zaidi na yenye nguvu.

"CHADEMA walikataa kabisa suala hili kwa maelezo kuwa “wao wako tayari kuungana na CUF tu katika kambi ya upinzani na kuwa hawaviamini vyama vya NCCR, TLP na UDP, na tulijaribu kuwasihi lakini hawakutaka kubadili msimamo huo.

"Lakini baada ya yote hayo, jana (juzi) CHADEMA wametoa kauli ya kinafiki,  eti wao hawawezi kushirikiana na chama kinachoongoza dola, yaani CUF na kuwa wao CHADEMA wako tayari kushirikiana na NCCR-Mageuzi," aliongeza.

Bw. Mtatiro alisema kuwa hivi karibuni NCCR ndio walikuwa kikwazo kwa CHADEMA kushirikiana na vyama vingine, hata mwezi haujapita wamegeuka na kudai CUF ndiyo adui.

"CHADEMA ni chama popo sana, hawajui wanachofanya, wamelewa madaraka na kuchanganyikiwa vibaya baada ya kupata majimbo 20 Tanganyika, sasa hawana haja na CUF na vyama vingine, wanadhani majimbo 20 ndio Ukombozi wa Tanzania umemalizika.

“Ni sawasawa na maskini sana anayeamka ghafla anajikuta tajiri, hajui namna gani atatumia utajiri wake, anaanza kuwatukana majirani zake alioishi nao kwa shida na raha katika umaskini wao, anawatukana majirani huku anaendelea kuponda mali na wasichana warembo katika kijiji hichohicho, siku moja mali zinaisha……hadithi ya tajiri mjinga inaishia hapo," aliongeza Bw. Mtatiro kwa jazba.

Aliendelea kukishutumu chama hicho kuwa kinafanya kusudi kutoa kauli za kichochezi, wakiamini kuwa CUF ikifa bara wao watapumua mno.

Alisema ni wazi CHADEMA wanaiogopa CUF, huku wakifahamu fika kuwa chama hicho kina mtandao mkubwa na kina mbinu ya kujiimarisha bara na hatimaye kuongoza nchi.

Bw. Mtatiro alidai kuwa kitendo cha CHADEMA kuwadharau Wazanzibari, kudharau maamuzi ya wananchi wa Zanzibar katika nchi yao, kudharau katiba ya Zanzibar ni kitendo cha kijinga mno.

"Wazanzibar ndio walioamua kwa kupiga kura kuwa wanahitaji serikali yao, ya umoja wa kitaifa kwa maslahi ya nchi yao ya Zanzibar kwa kujali amani maendeleo na ustawi wa taifa lao.

"Wazanzibari ndio walioamua kuwa chama kitakachoongoza katika uchaguzi kitatoa rais na mawaziri na cha pili kitatoa pia makamu wa kwanza wa rais na mawaziri. Wakapiga kura, wakatoa maamuzi haya, wakayaingiza katika katiba yao ya Zanzibar katika mabadiliko ya 10 ya katiba," aliongeza.

Alisema ni ujinga kudai CUF kuwa katika mfumo wa serikali iliyoamuliwa na wananchi katika upande mmoja wa nchi ni dhambi.
  
Alihoji kuwa, CUF ilipopata nafasi ya pili Zanzibar CHADEMA walitaka ikiuke matakwa ya wananchi na kukataa kuingia serikalini ili iwafurahishe CHADEMA ambao Zanzibar hawana hata mjumbe wa mtaa wala tawi?

"Nani asiyejua kuwa CUF ni chama chenye nguvu na mtandao Zanzibar na Tanganyika na ni chama cha pekee cha upinzani chenye wabunge kutoka pande zote za muungano? Nani asiyejua kuwa CHADEMA ni chama kilichoko Tanganyika peke yake?

"Nani asiyejua kuwa CHADEMA kinaumizwa sana na mafanikio na utulivu wa kisiasa Zanzibar yaliyochangiwa kwa kiasi kikubwa na busara na viongozi wa CUF ambao hawakuweka maslahi ya chama mbele katika kulinda uhai na maisha ya Wazanzibar?" alihoji.

Bw. Mtatiro aliyewania ubunge katika Jimbo la Ubungo na kushindwa na Bw. John Mnyika wa CHADEMA, alidai kuwa CUF kama chama chenye nguvu kubwa Zanzibar watazidi kuheshimu maamuzi ya wananchi walio wengi kila mara bila kujali kama CHADEMA watakasirika au la.

Aliongeza kuwa chama kipi ili kuwatumikia Watanzania, kuwatetea katika madhila yote na manyanyaso wanayofanyiwa.

"Tutaendelea kuwa katika SUK na kulinda maamuzi na matakwa ya wananchi wa Zanzibar lakini kwa upande wa Tanzania bara ambako katiba iko wazi, kuna chama kimoja kinachoongoza dola na vingine vyote vikiwa vyama vya upinzani, tutaendelea kuheshimu matakwa ya kikatiba yaliyopo Tanzania bara," alisema.

Aliwataka CHADEMA wafahamu kuwa CUF kitazidi kuwa chama cha kitaifa kwa kuzidi kupata wabunge wengi kutoka Bara na Zanzibar, kujiimarisha pande zote za nchi hadi waione njema inayosubiriwa na Watanzania wote.

Bw. Mtatiro aliongeza: "CHADEMA na watu wote wanaoitakia mabaya CUF watakufa na kukiacha chama hiki kikishamiri kama tegemeo la pekee la Watanzania," alisema.

No comments: