ANGALIA LIVE NEWS

Thursday, February 3, 2011

Wabunge kujengewa nyumba kama mawaziri.


WABUNGE sasa watakuwa na makazi yao maalumu mjini Dodoma maarufu kama Bunge Estate, sawa na ilivyo kwa mawaziri jijini Dar es Salaam na Dodoma, baada ya Spika wa Bunge, Anne Makinda, kuweka bayana mpango huo kwa wawakilishi hao.


Mradi huo mkubwa na wa kisasa ambao umewakuna wabunge wanaohudhuria semina elekezi ya siku kumi, unatekelezwa kwa pamoja kati ya Ofisi ya Bunge na Shirika la Nyumba la Taifa (NHC), huku ukitarajiwa kuathiri biashara ya nyumba za kukodi na hoteli.

Kwa mujibu wa duru za habari za kuaminika kutoka katika semina hiyo kisha kuthibitishwa na Makinda, zilifafanua kwamba hatua iliyofikiwa hadi sasa ni mchoro wa ramani ya eneo la mradi, huku shabaha ikiwa hadi katikati mwakani kuwe na nyumba zilizojengwa.

"Ndiyo, huo mradi tulikuwa tukiujadili hapo ndani (ukumbi wa semina). Ni mradi ambao tutashirikiana na wenzetu wa NHC (Shirika la Nyumba)," alithibitisha Spika Makinda.





Kwa mujibu wa Makinda, kitu cha kwanza kilichokuwa kikifanyiwa kazi ni kupata eneo na sasa kinachofanyika ni michoro.

"Kuhusu gharama bado hatujapata kwa sababu ndio kwanza mradi uko hatua za awali," alisema.

Aliendelea kuwa, NCH kazi yao ni kujenga nyumba hizo huku Ofisi ya Bunge ikijipanga kurejesha fedha hatua kwa hatua kipindi cha miaka isiyopungua sita.

Spika Makinda alifafanua kwamba, wabunge watatozwa kiasi cha fedha kitakachoamuliwa kama sehemu ya kusaidia kurejesha deni hilo hapo baadaye.

Makinda akithibitisha hayo, duru za ndani ya semina zilizidi kuweka hadharani mpango huo kwamba, zitakuwa nyumba 350 ambazo kati ya hizo 200, zitakuwa kwenye muundo wa ghorofa na nyingine 150 za chini na hautakuwa mbali na Chuo Kikuu cha Dodoma (Udom).

Kwa mujibu wa chanzo hicho huru, ili kuhakikisha nyumba hizo zinabaki kuwa mali ya Bunge, kila mbunge atakaa kwa muda wa miaka mitano na kuongeza: "ikimalizika unaondoka na familia yako."

Chini ya mpango huo, Makinda na Naibu wake, Job Ndugai, waliufafanua vema kwa wabunge kuhusu usimamizi wa mradi huo kuhakikisha unanufaisha wabunge wapya watakaokuwa wakiingia bungeni.
 
Source: Mwananchi.

2 comments:

Anonymous said...

Pesa zitatoka wapi na kwa nini wajengewe nyumba, marekani na pesa zao wawakilishi, senators na representative" hawajengewi nyumba. hizo pesa zitumie kuwasomesha watanzania nchi za nje.

Anonymous said...

Marekani awapati per DIEM!!!!!!!!!!!OYEEEE TANZNANIA CHUKUA CHAKO MAPEMA.