Maafisa polisi wanne wameshtakiwa kwa kosa la mauaji baada ya kudaiwa kusababisha vifo vya watu wawili waliokuwa wakitazama mechi ya mpira baina ya timu za Chelsea na Manchester kwenye baa.
Polisi walisema baa hiyo ilikuwa iko wazi kinyume na sheria ikionyesha mechi ya ligi kuu ya soka ya England.
Wateja walikataa kuondoka kwenye baa hiyo na polisi walirusha mabomu ya kutoa machozi katika mji wa Mazabuka kusini mwa nchi hiyo.
Polisi walisema, hali hiyo ilisababisha watu kukurupuka ambapo mwanammke mmoja mwenye umri wa miaka 21 na mwanamme wa miaka 23 walifariki dunia.
Mwandishi wa BBC Mutuna Chanda wa Zambia alisema baa zinaruhusiwa kuwa wazi mpaka saa nne unusu.
Ligi ya England ina ushabiki mkubwa sana Zambia, kama ilivyo kwa nchi nyingine barani Afrika.
Mwandishi wetu alisema kulikuwa na maandamano Mazabuka, kilomita 100 kusini mwa mji mkuu Lusaka, baada ya taarifa kutapakaa siku ya Jumatano juu ya vifo hivyo.
Waandamanaji hao waliziba barabara ya Great North inayounganisha mji ulio maarufu kwa utalii nchini Zambia Livingstone na Lusaka.
Maafisa wa ziada wa polisi walipelekwa mjini humo na hali kwa sasa ni shwari.
No comments:
Post a Comment