ANGALIA LIVE NEWS

Wednesday, March 2, 2011

KABICHI:Kinga kubwa dhidi ya saratani-GPL

Ugonjwa wa saratani (cancer) ni miongoni mwa magonjwa hatari yanayosumbua watu duniani hivi sasa, Tanzania ikiwemo. 

Wagonjwa wanaongezeka kila kukicha katika Hospitali ya Ocean Road jijini Dar es Salaam, ambayo ni maalum kwa ugonjwa huu.

Katika makala ya leo, tutajifunza faida za kabichi katika mapambano dhidi ya ugonjwa huo, licha ya kuchukuliwa kama ni mboga ya kimaskini na ambayo huliwa kwa shida zaidi kuliko kimanufaa ya kiafya. 

Ingawa inaonekana kuwa kabichi ni miongoni mwa mboga za majani zinazolimwa kwa wingi na kusambazwa kwenye masoko mengi nchini, hasa katika miji mikubwa, lakini ni watu wachache sana wanaopenda kula mboga hii.

Katika miji mikubwa, kabichi inatumika zadi kwa walaji wa chips. Hata hivyo hawaitumia ipasavyo kwa sababu huwa inapikwa na kukaangwa kwa mafuta kwa muda mrefu na hivyo kupoteza baadhi ya virutubisho vyake muhimu.

 KINGA DHIDI YA SARATANI
Miongoni mwa faida nyingi zinazopatikana kwa kula kabichi (nyeupe na nyekundu), inayoongoza ni ile ya kutoa kinga dhidi ya ugonjwa hatari wa saratani. 

Inaelezwa kuwa zaidi ya tafiti 475 zimefanyika kuhusu virutubisho vinavyopatikana kwenye kabichi na kuthibitisha kuwa vina uwezo wa kuzuia ugonjwa wa saratani na wakati mwingine kutibu.

Kabichi imeonekana kuwa na uwezo wa kipekee katika kupambana na ugonjwa huu kutokana na kuwa na kiasi kikubwa cha aina tatu muhimu za virutubisho; 
‘Antioxidant’, ‘Anti-inflammatory’ na ‘Glucosinolates,’ ambazo zina uwezo wa kudhibiti magonjwa nyemelezi kadhaa ambayo husababisha saratani za aina mbalimbali mwilini.

Kwa kuzingatia madhara na mateso yatokanayo na ugonjwa wa saratani, na kwa kuzingatia upatikanaji wa kabichi usiokuwa na gharama, huna sababu ya kupuuzia ulaji wake. Laiti kama watu wote tungejua sawasawa faida za kabichi, bila shaka mboga hii ingekuwa ghali kuliko hata samaki.

AHUENI YA VIDONDA VYA TUMBO
Mbali ya kuwa na uwezo wa kutoa kinga dhidi ya ugonjwa wa saratani, juisi ya kabichi inaelezwa kuwa na faida nyingi tumboni, hasa kwa wale wenye matatizo ya vidonda vya tumbo (peptic ulcers). Ikitumika mara kwa mara huwa kama tiba kwao. Hali kadhalika mfumo wa usagaji chakula tumboni, huwa imara.

HUIMARISHA MFUMO WA MOYO
Utafiti mwingine uliofanyika kuhusu kabichi umeonesha kuwa mboga hii huimarisha mfumo mzima wa moyo kwa kudhibiti utengenezwaji wa lehemu (cholesterol) mbaya mwilini ambayo inapozidi mwilini, husababisha matatizo ya moyo.

VITAMINI ZINAZOPATIKANA KWENYE KABICHI
Ndani ya kabichi, kuna kiwango cha kutosha cha aina mbalimbali za vitamin, hususan Vitamin K, Vitamin B1, Vitamin B2, Vitamin A na Vitamin C. Aidha, kabichi ina kiasi kingi cha kambalishe (fiber) Manganizi (Manganese), Potashiamu (Potassium) na Fatty-3 acids. Vyote hivi ni kinga ya mwili dhidi ya magonjwa nyemelezi.

Ili kupata faida za kabichi na kujenga kinga imara dhidi ya magonjwa ya saratani, weka mazoea ya kula kabichi mara kwa mara, angalau mara tatu kwa wiki, kwa namna ambayo utaona mwenyewe inafaa, iwe kama mboga au kachumbari.

No comments: