ANGALIA LIVE NEWS

Wednesday, March 2, 2011

Mbowe amjibu Rais Kikwete

Mwenyekiti wa Chadema Freeman Mbowe
Waandishi Wetu
SIKU moja baada ya Rais Jakaya Kikwete kusema Chadema kinataka kuleta machafuko kwa kudai mambo yasiyoweza kutekelezeka, Mwenyekiti wa chama hicho, Freeman Mbowe amemtaka apishe Ikulu ili kitekeleze madai hayo.

Akilihutubia taifa juzi, pamoja na mambo mengine, Rais Kikwete alisema: "Ni kweli kuna hali ngumu ya maisha na kukabiliana nayo ndiyo kazi tunayoendelea kufanya kila siku. "Tumeelekeza nguvu zetu na rasilimali zetu huko na mafanikio yanaonekana katika nyanja mbalimbali na maeneo mbalimbali. Hayo si matatizo ya kumalizika ndani ya siku tisa."

Rais Kikwete alifafanua kuwa kikwazo siyo upungufu wa sera wala dhamira, bali ni kiwango cha maendeleo madogo ya uchumi wa nchi na hivyo uwezo siyo mkubwa wa kuyakabili na kuyamaliza matatizo yote haraka kama ambavyo ingepaswa iwe.


Kikwete akirejea zama mbali za viongozi mbalimbali tangu uhuru, alisema hata Baba wa Taifa Mwalimu Nyerere aliongoza kwa miaka 23 na hakuyamaliza matatizo ya maendeleo ya nchi hii.

"Wale wa umri wangu au kunizidi wanakumbuka hali ilivyokuwa wakati anang’atuka. Hakuacha nchi ikiwa tajiri. Mzee Mwinyi kakaa miaka 10 hakuyamaliza, Mzee Mkapa naye kakaa miaka 10 hakuyamaliza. Mie nimekaa miaka mitano hayakwisha na nitamaliza mitano hayataisha yote," alisema.

Hata hivyo, akiwahutubia wakazi wa Miji ya Isaka, Kahama na Bukombe jana, Mbowe alisema "Kama siku tisa hazimtoshi kutekeleza hayo, aipishe Chadema ifanye kwani inaamini inawezekana."

Akiwa wilayani Kahama, msafara wake ulikuwa ukisimamishwa mara kwa mara na umati wa watu waliokuwa wamejipanga kando ya barabara wakimshinikizwa azungumze nao. Katika Mji wa Isaka, alisimamishwa na wafuasi wa chama ambao walisukuma gari lake huku wakimtaka azungumze nao.

“Rais Kikwete anasema kuwa njia ya kubadilisha uongozi ni uchaguzi na kuwasilisha matatizo ni bungeni, hatuendi huko. Tukisema bungeni wanatuzomea kwa vile wao wako 300, tukifanya uchaguzi wanachakachua kura zetu sasa na sisi tukiwa nje tuko milioni, tumepita mikoa mitatu sasa analalamika,” alisema Mbowe.

Aliwataka wananchi kusimama na kudai haki kwa vile serikali ya CCM imezoea kutenda hivyo kutokana na wananchi kuwa wapole na kutoa mfano kuwa katika malalamiko yao ya siku tatu, tayari serikali imeanza kujadili namna ya kushusha bei ya sukari.

Naye mbunge wa Musoma Mjini (Chadema), Vincent Nyerere akizungumza mjini Kahama alisema kuwa wananchi wanapaswa kufikiria zaidi na kuunga mkono jitihada za chama chake kutokana na kuwa na sera za kuwasaidia.

Alisema ikiwa serikali ya sasa inashindwa kutumia rasilimali watu, chama chake kinampango wa kuangalia namna ambavyo kinaweza kuwatumia wafungwa wenye taaluma mbalimbali kusaidia matatizo mbalimbali kama nchi nyingine badala ya kuwafungia gerezani huku wakipasua kuni na mawe.

Katika hatua nyingine, wasomi na wanasiasa wameiponda hotuba ya Rais Kikwete wakisema haina jipya. Baadhi yao wamekitetea Chadema na kupinga kauli ya Rais kwamba chama hicho kina lengo la kuleta machafuko.

Wakizungumza kwa nyakati tofauti jana wasomi hao walisema pamoja na uzuri wa hotuba yake, Rais Kikwete amekosea kitu kimoja, kuishambulia Chadema.

Mwasisi wa Chadema Edwin Mtei alisema madai ya Rais Kikwete dhidi ya Chadema hayana ukweli kwani lengo la maandamano yake siyo kuiondoa serikali iliyopo madarakani, bali kufikisha ujumbe wa kudai haki.
 
“Ah! Nimemsikia jana anasema kuwa sisi tunataka kuleta machafuko. Hakuna, hawana jipya sisi lengo letu ni kuwaeleza wananchi kuhusu ufisadi uliopo ndani ya serikali ya CCM na tutaendelea kuandamana hadi kieleweke,” alisema Mtei

Alisema serikali ya CCM imeshindwa kuondoa hali ya umaskini kwa Watanzania, badala yake viongozi wa chama hicho wamekuwa wakijilimbikizia mali kwa ukwasi na alisisitiza kuwa Chadema kitaendelea kupigana kufa na kupona na kupaza sauti zao kwa kueleza shida za Watanzania.

Kwa upande wake, Shirikisho la Wenye Viwanda Tanzania (CTI), limepongeza mikakati ya serikali kukabiliana na ugumu wa maisha lakini likaonya kuwa kama gharama za uzalishaji hazitapungua, hali inaweza kuwa mbaya zaidi.

Mtendaji Mkuu wa CTI, Christina Kilindu akizungumza ofisini kwake Dar es Salaam jana alisema jambo la kwanza ni kukabiliana na tatizo la nishati ya umeme.

''Kwa kweli, mfumuko wa bei ni tatizo kubwa linaloumiza kichwa. Chanzo ni ongezeko la gharama za uzalishaji na gharama za uzalishaji hazitashuka kuondoa mfumuko wa bei itakuwa ngumu,'' alisisitiza Kilindu. 

Alifafanua kwamba gharama za kufanya biashara nchini zimekuwa zikipanda huku akitoa mfano wa mwajiri kupaswa kulipa asilimia sita tofauti na nchi kama Kenya na Uganda ambako ni kati ya asilimia moja hadi mbili.

"Asilimia sita ni nyingi, asilimia mbili kulipwa kwa ajili ya Elimu ya Ufundi kwa VETA sawa lakini hizi asilimia nne zinazoingia Hazina zingepaswa kuondolewa," aliaema na kuongeza:

"Zamani kiasi hicho cha asilimia nne kilikuwa kikiingia kama 'housing levy' lakini sasa hivi hakuna benki ya nyumba hizo asilimia nne zinakwenda wapi?"

Akizungumzia umeme, alisema kama mali zilizopo hazitatumika kwa sasa hali itakuwa mbaya zaidi kwani uzalishaji utakuwa mgumu kwa kutumia majenereta, ambayo hutumia mafuta.

''Sasa hivi pipa tunasikia limefikia dola 120 lakini kama ghasia katika nchi za Kiarabu zitaendelea, kuna hatari likafikia hatua ya juu kabisa ya dola 200. Libya sasa hivi mambo siyo mazuri."

Licha ya kuonyesha matumaini juu ta mipango ya Serikali, alisema kupanda kwa mafuta pia kutaongeza gharama za usafirishaji mazao kutoka mashambani na huduma za usafiri.

Alisema ni vyema serikali ikatumia rasilimali za ndani kumaliza tatizo la umeme nchini ikiwa ni pamoja na kufanya uamuzi mgumu wa kuzalisha umeme katika mradi mkubwa wa Stiglers, ambao utaifanya nchi kuuza ziada nje.

Akirejea ahadi ya Rais Kikwete alipohutubia Bunge na kuahidi kuendeleza mradi huo aliwapa matumaini wawekezaji wakiwemo wao wenye viwanda,
Kilindu alisema msimamo huo wa kutaka uzalishaji katika eneo hilo pia umewasilishwa na CTI mbele ya Kamati ya Bunge ya Nishati na Madini.

''Mgawo wa umeme tangu mwaka 1992 hauishi, huwezi kuzungumzia uchumi kama huzungumzii umeme. Sasa hivi tumesema kila kinachoweza kuzalisha umeme nchini kizalishe na tuweke kando siasa,'' alisema.

Chama cha APPT-Maendeleo kimeitetea Chadema kikieleza kuwa yote yanayozungumzwa na chama hicho ni mambo ambayo yapo na yanayomgusa Mtanzania.

Mwenyekiti wa chama hicho, Peter Mziray alisema jana kuwa anachotakiwa kufanya Rais Kikwete kwa sasa ni kutekeleza ahadi zake alizozitoa wakati wa kampeni na zile za kiporo kabla ya mwaka jana kwa kuwa wananchi wanataka kuona maendeleo.

Alisema licha ya mkuu huyo wa nchi kumaliza siku 100 katika ngwe yake ya pili, hakuna cha maana kinachoendelea bali kumekuwa na shida kila mahali.

“Mimi sioni kama Chadema wana kosa, mfano wamezungumzia suala la mgawo wa umeme ambao umedumu kwa zaidi ya miaka saba sasa hapa wana kosa gani wakati suala hili linamgusa kila Mtanzania? Sasa kama anawaambia watu wasikifuate Chadema wafuate nini, wafuate CCM ambayo inakufa? Alisema Mziray.

Mziray alimshauri Rais Kikwete kuwa makini na kwamba asiendelee kufanya kazi za kila siku pekee, bali aangalie jinsi gani watu wanaweza wakamsaidia kutatua matatizo mbalimbali yanayolikabili taifa.

Mbunge wa Kigoma Kusini (NCCR-Mageuzi), David Kafulila alisema hotuba ya Rais Kikwete imeshindwa kutoa majibu kwa maswali mengi ambayo wananchi wamekuwa wakijiuliza... “Cha kushangaza Rais Kikwete anazungumzia kutenga asilimia 10 ya bajeti ambayo ilizungumzwa miaka ya nyuma, tunakwenda wapi?”

Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Bashiru Ally aliipongeza hotoba ya Rais akisema imebashiri kuwa Tanzania ina tatizo la msingi lakini akaikosoa kuwa haikujielekeza kwenye tatizo la msingi ambalo ndiyo chanzo cha kutoweka kwa amani.

Alisema tatizo walilonalo Watanzania kwa sasa ambalo linafanya hali kuwa tete nchini ni mfumo mbovu wa uchumi na siasa.

“Maandamano ya Chadema hayawezi kuwa chanzo cha kutoweka kwa amani hapa nchini, nilitarajia Rais angezungumzia mfumo mzima wa uchumi na siasa ambayo ni mbovu na imeshindwa kuwasaidia wananchi wake,” alisema Bashiru.

Alisema mfumo wa uchumi na siasa ni mbovu na kwamba hali hiyo ndiyo inayoonyesha viashiria vya kutoweka kwa hali ya amani hapa nchini.

“Yapo matatizo mengi ambayo ni viasharia vya kutoweka kwa amani, kitendo cha polisi kupigana na wafanyabishara katika eneo la Darajani Visiwani Zanzibar, migogoro ya ardhi baina ya wanachi na wawekezaji, vijana kukosa ajira na wengine kukosa elimu, hivyo ndivyo viasharia vya kutoweka kwa amani,” alisema.

Bashiru alisema Rais Kikwete hakustahili kuzungumzia maandamano badala yake angejikita katika mambo ya msingi likiwamo suala la kuporomoka kwa elimu, ukosefu wa ajira na tatizo la ugumu wa maisha linalowakabili  wananchi kwa sasa.

“Kuna wananchi wengi wamekata tamaa, watu hawa hawana muda wa kusikiliza hutoba ya Rais wala kwenda kwenye maandamano ya Chadema wao wanazungumzia ugumu wa maisha, hali hii inatutaka kuchukua hatua ya kutafakari na kuufanyia kazi mfumo wetu wa uchumi,” alisema.

Alisema ili kutatua tatizo hilo, juhudi za makusudi zinafaa kuchukuliwa ikiwa ni pamoja na kutafakari kwa kina ili kuhakikisha mfumo wa uchumi na ule wa kisiasa unaboreshwa na kwenda sambamba na mahitaji ya wananchi.

Bashiru alisema huu si wakati wa malumbano ya kisiasa na baina ya vyama kwa kuwa hayatalisaidia taifa, bali kinachopaswa kufanywa ni kwa wadau kushughulikia tatizo la msingi ambalo ni mfumo uliopo sasa.

Mkazi wa Tabata, Mndame Mchande alisema anakubaliana na kinachofanywa na Chadema na kwamba hatua inayofanywa na chama hicho ndiyo inayotakiwa kwa kuwa hata wabunge wake wakipeleka hoja bungeni hupingwa.

“Wanachofanya ni sawa…. hao wanaolalamika juu ya Chadema hawawezi kufanya kitu kama hicho, wao wanachokijua ni kung’ang’ania madaraka tu,” alisema Mchande.

Alisema wanaopiga makelele dhidi ya Chadema ni kama wanataka kuidanganya jamii akisema chama hicho kinatekeleza yale kilichoahidi ikiwa ni pamoja na kuwatetea wananchi maskini.

Mfanyabiashara kutoka Mafinga, Victory Kipanguala alisema kwamba alitegemea Rais Kikwete angejadili tatizo la umeme na namna ya kumaliza mgawo na lakini akasema kitendo chake cha kusema kwamba bidhaa zitapungua bei wakati viwanda vinatumia umeme wa bei kubwa zaidi ni kuidanganya jamii.

Alisema kitendo cha kuijadili Chadema na kuacha mambo ya msingi ndiyo sababu ya yeye kuiona hotuba ya Rais haina lolote.

Mfanyabiashara mwingine kutoka Iringa, Godson Sanga alisema alitegemea Rais Kikwete angefafanua sakata la Kampuni ya kufua umeme ya Dowans.

“Kuna mchakato wa kuilipa kampuni hii ya Dowans, mimi nilifikiri Rais angezungumzia msimamo wa serikali kuhusu ulipaji wa kampuni hii, lakini amezungumzia mambo mengine kabisa ambayo hayana tija kwa Watanzania,” alisema Sanga.

Habari hii imeandaliwa na Moses Mashalla, Arusha; Frederick Katulanda, Mwanza; Ramadhan Semtawa, Nora Damian Fidelis Butahe, Geofrey Nyang’oro na Raymond Kaminyonge, Dar es Salaam.

CHANZO:MWANANCHI

No comments: