ANGALIA LIVE NEWS

Monday, June 20, 2011

Baba adaiwa kuua watoto wake kinyama

Mganga wa kienyeji maarufu kama sangoma, Modoka Kubekwa (34), mkazi wa kijiji cha Lung’eya Wilaya ya Sengerema Mkoa wa Mwanza anadaiwa kuwaua watoto wake wawili, akiwemo mwenye umri wa siku mbili kwa kuwachoma mkuki na kuwapiga kwa rungu kichwani baada ya kuzuka ugomvi kati yake na mkewe.
Kwa mujibu wa Ofisa Mtendaji wa Kata ya Nyakariro, Alfonsi Kube, tukio hilo lilitokea usiku wa kuamkia jana.

Kube alisema inadaiwa kuwa mtuhumiwa huyo alitenda kosa hilo baada ya kutoka kilabuni kunywa pombe.
Alisema baada ya baba huyo kufanya kitendo hicho, alianza kupiga ngoma za mashetani hadi asubuhi akidhani kwamba anaweza kuwazindua watoto hao.
Aliwataja watoto hao waliuawa kuwa ni Taabu Modoka (2) na Kwigema (siku mbili).
Kube alisema mtuhumiwa huyo alikamatwa jana asubuhi na wananchi na kwamba anashikiliwa katika Kituo cha Polisi Nyakariro.
MAMA AMNYOFOA MWANAWE NYETI

Naye mtoto mwenye umri wa miezi 11, Kasimu Mohamed, mkazi wa Kijiji cha Ufuruma kilichopo Wilaya ya Uyui amelazwa Hospitali ya Mkoa wa Tabora ya Kitete baada ya kunyofolewa sehemu za siri kwa kung’atwa kwa meno na mama yake mzazi.
Mganga Mfawidhi wa Hospitali hiyo, Dk. Paskali Nyango amethibitisha mtoto huyo huyo kulazwa katika wodi ya watoto namba 11 kwa ajili ya kupatiwa matibabu ya majeraha makubwa aliyopata baada ya kunyofolewa sehemu hizo.
Dk. Nyango alisema mtoto huyo alipelekwa hospitalini hapo na bibi yake mzaa mama yake huyo, Mariam Mohamed na kuanza kumpa matibabu, lakini hakuwa na viungo hivyo vilivyonyofolewa kwa kung'atwa na meno.
" Ukweli ni kwamba mtoto huyo aliletwa hospitalini hapa na bibi yake akiwa na kidonda kikubwa baada ya kung’atwa... sehemu zote za siri hazikuwepo," alisema Dk. Nyango.
Alisema bibi wa mtoto huyo alipoulizwa kuhusiana na chanzo cha tukio hilo, alisema mama wa mtoto huyo aliondoka naye siku moja kabla na aliporudi ndipo alipobainika kuwa hana sehemu zake za siri.
Hata hivyo, Dk. Nyango alisema mama wa mtoto huyo ambaye naye amelazwa hospitalini ana matatizo ya akili baada ya kubainika kuwa amechanganyikiwa.
Alisema kutokana na kutopatikana sehemu zilizonyofolewa ili kujaribu kuzirudishia, wameamua kumtibu mtoto huyo majeraha huku wakifanya utaratibu wa kumpeleka katika Hospitali ya Rufaa ya Bugando iliyopo jijini Mwanza.
Akizungumza kwa masikitiko, Bibi huyo, alidai mama wa mtoto huyo ambaye aliondoka Juni 16 na mtoto wake huyo na kurudi naye Juni 17 akiwa amemfanyia kitendo hicho, amechanganyikiwa.
Alisema mama huyo amezaa watoto sita kati yao, wawili walifariki.
Hata hivyo, alisema mama huyo ambaye ni mwanawe hajawahi kufanya kitendo kama hicho.
" Ukweli ni kwamba amerukwa na akili kwa siku nyingi na amejifungua watoto sita ila wawili walishafariki, lakini tunashangaa kutokea kitendo hicho," alisema Mariamu
Baadhi ya wananchi waliokuwa katika hospitali hiyo wamesikitishwa na tukio hilo.
Jeshi la Polisi Mkoa wa Tabora limethibitisha kutokea kwa tukio hilo na kusema mama huyo amelazwa hospitalini hapo chini ya uangalizi wa askari ili akipata nafuu limchukulie hatua.
CHANZO: NIPASHE

No comments: