MADEREVA wa daladala jijini Dar es Salaam wametangaza mgomo kuanzia leo, wakidai kuwa hawatendewi haki na askari wa usalama barabarani.Pia, wamedai wanapopandishwa kizimbani kwa makosa mbalimbali hunyimwa dhamana kwa sababu ya kukataa kutoa hongo kwa polisi wanayoitaka kwa maelezo ya kuwaepusha na faini ya Sh 300,000.
Wamesema kama kazi ya udereva wa daladala ni uhuni basi ifutwe na kama si uhuni watafanya mgomo wa siku mbili na kwamba abiria watasafirishwa na magari ya Serikali.Licha ya Mwenyekiti wa Chama cha Madereva nchini (TDA), Tawi la Dar es Salaam, Ahmed Ally jana kuwashawishi madereva hao kusitisha mgomo, walikataa huku wakisisitiza kuwa mgomo ndiyo njia sahihi ya wao kusikilizwa.
Madereva hao walifikia uamuzi huo baada ya kuona viongozi wa TDA, Umoja wa Madereva, makondakta na wasimamizi wa foleni za Daladala Dar es Salaam (UMMADADAR) pamoja Umoja wa Maendeleo ya Madereva na Makondakta Wilaya ya Ilala (Uwawawi), kuwakatisha tama kwa maelezo kwamba mgomo siyo suluhisho la kero hizo.
Wakizungumza katika mkutano uliofanyika jana katika Shule ya Msingi Buguruni, madereva zaidi ya 60 walilitupia lawama Jeshi la Polisi Kitengo cha Usalama Barabarani, huku wakiwataja kwa majina baadhi ya askari wake kuwa wanawakamata na kuwalazimisha watoe fedha.“Mimi nilikamatwa kwa kosa la kuacha mlango wa daladala wazi, nilipelekwa Kituo cha Polisi Buguruni na waliniambia nitoe Sh 300,000, na kwamba nisipotoa nitapelekwa mahakamani,” alisema Amani Abdallah.
Aliongeza, “Nilimwita mmiliki wa gari ili anidhamini, wale askari walikataa na kumwambia achukue gari lake na aondoke ila mimi nibaki kituoni,baadaye walikubali ila walisema tutoe Sh 60,000 lakini katika risiti walituandikia Sh 20,000, hii ni haki?Alihoji.Dereva mwingine, Alex Maduka alisema kuwa Askari wa Usalama barabarani wakilikamata daladala, kila kosa moja humtaka dereva kulipia Sh 20,000.“Wakikamata gari hulichunguza na kuorodhesha makosa zaidi ya 10 na kukutaka kulipia Sh 300,000, wanasema kosa hilo liko chini ya Sumatra (Mamlaka ya Usafiri wa Nchi kavu na Majini),wanatuambia ili tusilipe kiasi hicho cha fedha tuwape Sh 50,000,”alisema Maduka.
Mfaume Mbulu alidai wanaposhindwa kulipa faini wanazotozwa na askari hao hufikishwa mahakamani na kudai kuwa kesi hizo husimamiwa na Askari wa Usalama barabarani ambao wanahakikisha mtuhumiwa ananyimwa dhamana.“Ukishindwa kutoa dhamana maana yake ni kwamba unakwenda rumande wiki mbili, hii hali imetuchosha ni bora tugome tu, wanagoma wanafunzi vyuo vikuu itakuwa sisi madereva,”alihoji Mbulu.
Mara baada ya madereva zaidi ya 20 kuwasilisha kero zao huku wakisisitiza kuwa kuanzia leo wataanza mgomo wa siku mbili, Ally aliwataka kutofanya hivyo kwa kuwa lengo la mkutano huo ni kusikiliza kero zao na kuziwasilisha sehemu husika.
“Jamani kuweni wastaarabu, sisi ni viongozi na hapa tumekuja kwa ajili ya kusikiliza kero zenu na kuziwasilisha sehemu husika, sasa hata mkigoma ni kwa faida ya nani, mgomo ni hatua ya mwisho kabisa,” alisema Ally.Mwenyekiti huyo wa TDA, alisema malalamiko ya madereva hayo yatapelekwa rasmi kwa Jeshi la Polisi na Mahakamani, huku akisisitiza kuwa kama yasipopatiwa ufumbuzi, madereva hao wanaweza kuamua kugoma.Baada ya kauli hiyo kuliibuka mvutano mkubwa huku baadhi ya madereva wakinyanyuka na kuanza kuondoka eneo hilo na kusisitiza kuwa suluhisho ni mgomo na si vinginevyo.
Hadi gazeti hili linaondoka eneo hilo saa 11 jioni mkutano huo ulikuwa hauna mwelekeo kwani kila dereva aligeuka mzungumzaji huku viongozi wakiwataka watulie ili kutoa maamuzi ya pamoja.
Polisi wazungumza
Kamanda wa Kikosi cha Usalama Barabarani nchini, Mohamed Mpinga alialipoulizwa juu ya suala hilo alisema malalamiko hayo si ya kweli na ndio kwanza anayasikia na kufafanua kwamba utaratibu wa kuwapeleka madereva mahakamani umekuja baada ya kuona kuwa wanavunja sheria za barabarani kwa makusudi.
“Hawawezi kutupangia adhabu ya kuwapa,unajua baada ya kuanza kuwapeleka mahakamani wamepunguza kufanya baadhi ya makosa kwa kuwa wapo madereva waliofungwa,”alisema Mpinga.
Alisema Jeshi la Polisi, halitaacha kusimamia sheria na kwamba wanaoomba rushwa watoe taarifa sehemu husika.“Makao Mkuu wa Jeshi la Polisi kuna kitengo cha maadili wakatoe taarifa huko zitafanyiwa kazi, lakini pia kuna Taasisi ya Kupambana na Kuzuia Rushwa (Takukuru),” alisisitiza.
Aliongeza, “Wapo madereva wanaowasingizia askari kwa kuwa askari hao wanafanya kazi yao kwa kufuata maadili, hilo tunalijua,”
CHANZO:MWANANCHI
No comments:
Post a Comment