Pamela Chilongola na Ellen Manyangu
ONGEZEKO la dawa za kulevya nchini limesababishwa na mabadiliko ya kukua kwa uchumi na maendeleo ya sayansi na teknolijia duniani.
Akihutubia kwenye maadhimisho ya siku ya kupiga vita dawa za kulevya duniani, Makamu wa Rais, Dk Mohamed Gharib Bilal, alisema mabadiliko hayo yamesababisha pia dawa hizo kuingizwa kwa urahisi nchini.
Dk Bilal alisema awali tatizo la dawa za kulevya lilikuwa dogo kwani lilihusisha zaidi bangi na mirungi, aina nyingine ya dawa za kulevya zilikuwa zikipitishwa nchini kuelekea mataifa mengine.
“Hivi sasa hali imebadilika, kwani utumiaji dawa za kulevya za viwandani hasa heroin, cocaine na mandrax umeongezeka kwa kasi na nchi yetu iomegeuzwa soko la dawa hizi,” alisema Dk Bilal.
Aliongeza kuwa watanzania 211 walikamatwa nje ya nchi kwa kujihusisha na biashara ya dawa za kulevya ambao baadhi yao walihukumiwa kunyongwa na wengine kutumikia vifungo katika nchi mbalimbali.
“Kipindi cha kuanzia mwaka 2005 mpaka 2010, watuhumiwa 30,830 walikamatwa kwa makosa mbalimbali ya dawa za kulevya na kufikishwa kwenye vyombo vya sheria,” alisema Dk Bilal.
Alisema ongezeko la matumizi ya dawa za kulevya hivi sasa yako vijijini na mijini, suala ambalo ni hatari zaidi yameanza kuonekana kwa watoto wadogo shuleni na mitaani.
“Watoto wetu wako katika hatari kubwa ya kuangukia janga hili, hii inatokana na ukweli kwamba uwezo wao kujilinda ni mdogo, hivyo wanahitaji ulinzi kutoka kwa wazazi na walezi,” alisema Dk Bilal na kuongeza:
“Tusiwaache watoto walelewe na television na inteneti, kwani mitandao hii ina taaarifa nyingi ambazo hazifai kwa watoto wetu, hali hii inachangia matumizi ya dawa za kulevya.”
Naye Kamishna wa Tume ya Kuratibu Udhibiti wa Dawa za Kulevya, Christopher Shekiondo, alisema matokeo ya ushirikiano na vyombo vya udhibiti ni kukamatwa kwa viwango vikubwa vya dawa za kulevya, ambavyo havijawahi kukamatwa kwa miaka mingi iliyopita katika historia ya nchi.
“Julai 2010 hadi Juni 2011, kuna matukio makubwa ya ukamataji wa kilo 268 za heroin na kilo 86 za cocain, zilikamatwa jambo ambalo siyo la kawaida kwa dawa nyingi kiasi hiki kukamatwa,” alisema Shekiondo.
Alisema changamoto zinazokabili nchi, ni watu kushawishika kuingia kwenye biashara haramu ya dawa za kulevya na kuongezeka kwa watumiaji sugu wanaohitaji tiba.
Mwananchi
No comments:
Post a Comment