ANGALIA LIVE NEWS

Monday, June 27, 2011

Muujiza waiokoa Yanga, APR yaua Moro

Winga mshambuliaji wa timu ya Yanga, Julius Mrope akijaribu kumtoka beki wa El-Mereikh, Wawa Pascal wakati wa mechi ya mashindano ya Kagame Castle Cup iliyofanyika jana kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam. Picha na Jackson Odoyo.
Sosthenes Nyoni, Doris Maliyaga, Morogoro
KLABU ya El Mereikh imetengeneza historia mpya kwenye michuano ya Kagame Castle Cup baada ya kufunga mabao yote manne wakati walipoilazimisha Yanga sare ya 2-2 , huku APR ikiichakaza Ports 4-0 mjini Morogoro.


Katika mchezo huo wa ufunguzi wa Kundi B, El Merreikh ilipata bao la kuongoza katika dakika ya kwanza lililofungwa kwa kichwa na Kelichi Osunwa aliyeunganisha vizuri krosi ya winga ya kushoto kutoka kwa Remi Adiko.

Uzembe wa kipa wa zamani wa kimataifa wa Misri, Elhadari Isam kushindwa kuzuia kwa makini mpira wa kurudishwa na beki wake uliwapa zawadi Yanga bao la kusawazisha dakika ya 6 ya mchezo, kabla ya beki Balla Gabir kujifunga bao jingine na kuifanya Yanga kuondoka mapumziko wakiwa mbele na mabao 2-1.

Mshambuliaji Jonas Sakumaha aliyeingia kutokea benchi dakika 63, aliisawazishia El Merreikh kwa shuti kali lililogonga mwamba na kudunda ndani ya goli kabla ya kurudi uwanjani na mwamuzi Denis Batte kukubali goli hilo.

Yanga na El Mereikh zimekutana mara sita katika mashindano tofauti ya kimataifa hadi jana ambapo El Mereikh iliweza kuifunga Yanga mara tatu na kutoka sare mara tatu.

Zilikutana katika fainali ya michuano kama hii ya Cecafa mwaka 1986  na El-Merreikh kuibuka na ushindi wa penati 4-2 dhidi ya Yanga na hii ni baada ya kufungana mabao 2-2 katika muda wa kawaida.

Mara ya mwisho ilikuwa mwaka 2007 katika michuano ya Kombe la Shirikisho Afrika ambapo katika mchezo wa kwanza uliofanyika jijini Dar es Salaam timu hizo zilishindwa kufungana wakati katika mchezo wa marudio uliofanyika nchini Sudan Al Mereikh iliichapa Yanga mabao 2-0.

Mashabiki hawakuwa na raha muda mwingi wa mchezo huo ambao wachezaji wa Yanga walionekana kufukuza vivuli vyao na kuwaacha El Mereikh kutawala sehemu kubwa ya mchezo kwa kupigana pasi watakavyo, lakini walikosa umakini kwenye umaliziaji.

Kiungo mpya wa Yanga, Julius Mrope alithibisha kweli anaweza kuziba pengo la Mrisho Ngassa kwa mabingwa hao kwani kila alipokuwa na mpira aliweza kuanzisha mashambulizi ya kushtukiza yaliyokuwa mwiba mkali kwa ngome ya El Mereikh.

Kocha wa Yanga, Sam Timbe dakika 19, alimtoa Jerryson Tegete aliyekuwa ameumia na kumuingiza Kenneth Asamoah.

Mrope alishindwa kuiandikia Yanga bao la pili dakika 28, baada ya kukosa umakini wa kumalizia krosi safi ya Davis Mwape, kabla Karim Edafi kuwalamba chenga mabeki wa Yanga na kupiga shuti hafifu lililodakwa na kipa Yaw Berko kwa ustadi mkubwa dakika 31.

Krosi ndefu ya Oscar Jushua ilitua kichwani mwa beki Balla Gabir wa El Merreikh aliyejifunga mwenyewe akiwa karibu na Asamoah aliyenyoosha mguu wake kutaka kupiga mpira huo na kuipa Yanga bao la pili.

Beki wa Yanga, Chacha Marwa nusura ajifunge mwenyewe  dakika 84, baada ya kurudisha mpira vibaya kwa kipa wake Berko ambaye alilazimika kufanya kazi ya ziada kuutoa kona mpira huo.

Mjini Morogoro; Mabingwa watetezi APR wameanza vema kampeni yao kwa kuichakaza Ports ya Djibouti kwa mabao 3-0 kwenye mchezo wa ufunguzi wa Kundi C uliofanyika kwenye uwanja wa Jamhuri.

Mabingwa hao walifungua karamu yao ya mabao dakika 44 kwa bao  lililofungwa na Nyirenda Victor akiunganisha kwa kichwa mpira wa kona uliopigwa na Haruna Niyonzima.

Mshambuliaji Nyirenda aliifungia APR bao la pili dakika 60 akiunganisha vizuri kwa kichwa mpira wa kurushwa na Iranzi Jean Claud, kabla ya Logbo Didier kufunga bao la tatu kwa mabingwa hao dakika 69 baada ya mabeki wa Ports kushindwa kuokoa mpira.

Wakicheza mbele ya mashabiki wachache na majukwaa matupu, APR  walihitimisha karamu yao kwa kufunga bao la nne dakika 87, lililofungwa na Kwizera Ernest aliyemaliza vizuri pasi ya Niyonzima.

Awali APR walikosa penalti dakika ya 9, iliyopigwa na Mugiraneza Jean Baptiste na kupanguliwa na kipa Khalid Ally wa Ports baada ya beki Abdourahman Ismail kumchezea vibaya Laybo Didier.

Porto watajilaumu wenyewe kwa kukosa nafasi nyingi za kufunga katika kipindi cha kwanza kupitia Warsama Moussa, Gasana Jean Bosco na Ramzi Galah kwa mashuti yao mengi kushindwa kulenga goli.

Mwananchi

No comments: