ANGALIA LIVE NEWS

Monday, June 27, 2011

Waathirika wa mabomu bado walala nje

Waathirika wa mabomu ya Gongo la Mboto wameitaka Serikali kuwapatia orodha ya majina ya watu watakaojengewa nyumba zao na lini ujenzi huo utaanza ili waondokane na adha wanazoendelea kuzipata.

Wakizungumza na NIPASHE mwishoni mwa wiki jijini Dar es Salaam, miongoni mwa waathirika hao walisema hawana taarifa yoyote licha ya serikali kusema watawajengea nyumba, jambo ambalo linawanyima matumaini ya kuishi katika nyumba.
“ Sisi hatuna taarifa yeyote inayohusiana na kujengewa nyumba kwani tangu tuorodheshe majina yetu kwa nia ya kujengewa nyumba ni miezi miwili sasa imepita na hakuna dalili yoyote, na kama ni taarifa ndo kwanza tunazisikia kwako,” alisema Veronika Manyema.
“Kama suala hili lipo hatulifahamu kwani hata kwenye vyombo vya habari hatujasikia taarifa yeyote, kama wametoa sisi hatujasikia wapo ambao wangesikia na kutupa taarifa kwani hata viongozi walioteuliwa kushughulikia suala ili hatujawahi kuwaona tangu zoezi la kuorodhesha majina liishe,” alisema Manyema.
Naye Fatuma Juma alisema katika mahema waliyojengewa wamekuwa wakipata shida jambo linalowalazimu kulala ndani ya nyumba zao zilizobomoka huku wakiishi kwa hofu ya kudondokewa na matofali kutokana na nyumba hizo kuwa na ufa.
“Hatuwezi kabisa kulala katika haya mahema kwani yana joto kali wakati wa mchana na wakati wa usiku, kutokana na mvua zinazonyesha kumekuwa na unyevu na hivyo kusababisha mazulia na magodoro kuloa,” alisema Juma.
Joseph Lustiki mmoja waathirika hao mkazi wa Pugu Bombani alisema kuwa wakati wa usiku kwa maeneo mengine vibaka wamekuwa wakichana mahema hayo na visu jambo linalowatishia amani na kushindwa kulala wakihofia kuchanwa na visu wakati wamelala ndani ya mahema.
“Tunashindwa kulala katika mahema kwani usiku vibaka wanachana na visu, na wakati mchana kuna kuwa na jua kali kiasi kwamba mtu huwezi kukaa ndani na hivyo inatubidi kukaa kwa jirani au kwenye nyumba zetu zilizobomoka,” alisema Rustiki.
Sambamba na hayo waadhirika hao wamewalalamikia wagawaji wa misaada katika makazi ya waathirika kutokana na kitendo chao cha kuwasainisha sahihi za uongo ambazo hazilingani na hali halisi ya vitu vinavyopokelewa na waathirika hao.
Josephina ambaye ni mmoja wa waadhirika ambao wamekuwa wakipewa misaada pungufu ukilinganisha na ilivyo orodheshwa katika vitabu ambavyo hupitishwa kwa kila familia kwa lengo la kusainisha mpokeaji wa misaada hiyo.
“Wanakujaga mara moja kwa mwezi hilo tunashukuru, ila sasa unapokabidhiwa misaada hiyo unatakiwa kusaini katika kitabu chao walichobeba lakini idadi ya vitu tunavyopatiwa na tunavyotakiwa kusaini ni tofauti, kwani wakati mwingine unakuta viroba hivyo vimefunguliwa na kufungwa na nyuzi za kufumia vitambaa,” alisema Josephina.
“Utakuta unakabidhiwa maharage au mchele kilo 30 lakini unaambiwa utie saini kilo 50 jambo ambalo si sahihi na wakati mwingine tukiuliza huwa tunajibiwa hii ni misaada kwa hiyo na wao wenyewe hawafahamu, alisema Ester Mahanga ambaye pia ni mwathirika.
CHANZO: NIPASHE

No comments: