ANGALIA LIVE NEWS

Monday, June 27, 2011

Vita ya posho yahamia Baraza la Wawakilishi

Rais Ali Mohamed Shein
Wajumbe wa Baraza la Wawakilishi wameibana Serikali ya Umoja wa Kitaifa (GNU) kupunguza safari za nje za viongozi wake na kuacha kupoteza fedha za umma kwa kuwanunulia magari ya kifahari.

Tamko hilo limo katika msimamo wa wajumbe hao wakati wakijadili hotuba ya bajeti ya Serikali kwa mwaka wa fedha wa 2011/12 katika ukumbi wa Baraza la Wawakilishi mwishoni mwa wiki iliyopita katika kijiji cha Chukwani.
Mwakilishi wa Kiwami, Hija Hassan Hija, alisema viongozi katika Serikali hiyo kwa muda sasa wamekuwa wakitumia fedha nyingi kwa safari za nje.
Alisema kupunguzwa kwa safari hizo kutaimarisha udhibiti wa mapato ya serikali na kupata uwezo wa kuimarisha huduma za jamii.
Hija alisema cha kushangaza safari zinazofanywa na viongozi hao hazileti manufaa yoyote kwa taifa.
"Viongozi, hasa mawaziri, makatibu na wakurugenzi, wanakwenda safari wakirudi hawaelezi faida ya ziara zao kwa taifa," alisema Hija.
Hata hivyo, aliwapongeza viongozi wa kitaifa, akiwemo Rais Ali Mohamed Shein na makamu wake wawili, kwa kuwa na utaratibu wa kueleza mafanikio ya ziara zao kila wanaporejea Zanzibar.
"Serikali ipunguze safari za mawaziri, makatibu wakuu na wakurugenzi ili mapato ya serikali ya umike kwa shughuli za maendeleo ya jamii," alisema Mwakilishi huyo.
Kuhusu utawala bora, Hija alisema inashangaza ripoti za Mkaguzi Mkuu na Mdhibiti wa Hesabu za Serikali kwa Zanzibar inaonyesha ukubwa wa tatizo la matumizi mabaya ya fedha za umma, lakini mpaka sasa hajasikia wala kuona mtu akikamatwa na kufikishwa mahakamani.
"Mahakama zetu ni za kusikiliza kesi za watu wanaotuhumiwa kwa wizi wa nazi na ndizi, lakini hakuna hata kesi moja inayohusu ubadhirifu wa mali za umma iliyowahi kupelekwa na kusikilizwa na mahaka hizo,” alisema.
Mwakilishi wa Magomeni, Salmin Awadh Salmin alisema asilimia 50 ya mapato ya serikali yanapotea kutokana na ukwepaji kodi unaofanywa na wafanyabiashara visiwani Zanzibar.
Alisema wananchi wanauziwa bidhaa madukani bila kupewa stakabadhi za malipo na kwamba kitendo hicho kinafanywa makusudi kuinyima serikali mapato kwa sababu kinaficha kumbukumbu za mahesabu.
Naye Mwakilishi wa Viti Maalum, Panya Ali Abdallah alisema sekta ya utalii Zanzibar inahitaji kuangaliwa kwa umakini kutokana na vitendo vya unyanyasaji vinavyofanywa na wawekezaji dhidi ya wafanyakazi katika sekta hiyo.
Alisema wawekezaji katika sekta hiyo hawazingatii sheria za kazi , matokeo yake hivi sasa Zanzibar kuna vitendo vya kuwafukuza wafanyakazi bila kuzingatisha mikataba ya ajira zao. Mwakilishi huyo alisema serikali hiyo ya umoja wa kitaifa kama imedhamiria kuimarisha uchumi wa Zanzibar iweke kipaumbele kikubwa kufufua sekta ya Viwanda kwasababu itasaidia kuondoa tatizo la ajira na pato la taifa.
CHANZO: NIPASHE


No comments: