Siku moja baada ya Waziri Mkuu, Mizengo Pinda, kusema uzinduzi wa Katiba mpya utafanyika Aprili 26 mwaka 2014, Mbunge wa Ubungo, (Chadema), John Mnyika, amemjia juu na na kuutahadharisha umma kuwa kauli yake hiyo ni dalili kuwa serikali inataka kuchakachua mchakato wa kupata Katiba mpya.
Amesema kama kauli ya Pinda ni ya dhati basi awasilishe rasmi bungeni kupitia kauli ya serikali au kupitia majumuisho ya hotuba yake kabla ya mjadala wa muswada wa sheria na uzingatiwe katika mipango, maazimio na sheria.
Mnyika ametahadharisha kuwa ukomo wa muda usipowekwa kwa mujibu wa sheria ama maazimio ya Bunge, serikali inaweza kuchelewesha mchakato mzima kwa kutoa visingizio mbalimbali ili usikamilike mapema kuwezesha maandalizi ya kisheria na kitaasisi kufanyika kabla ya Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2015 kwa kutumia Katiba mpya.
Mnyika katika taarifa yake ya jana alisema umma unapaswa kuipokea ahadi hiyo ya Pinda aliyoitoa kupitia Semina Elekezi kwa wakuu wa mikoa, wilaya na makatibu tawala wa mikoa kwa tahadhari kwa kuwa imeambatana na kauli tata kuhusu mchakato mathalani serikali kutokuwa na uhakika kuhusu wakati ambapo muswada wa sheria ya mapitio ya sheria ya marekebisho ya Katiba wa mwaka 2011 utawasilishwa bungeni.
Alisema alisema umma unapaswa kuipokea kwa tahadhari ahadi hiyo ya Pinda kwa kuwa imeambatana na kutolewa kwa maelekezo kwa wakuu wa mikoa, wilaya na makatibu tawala kuhusu maudhui ya mchakato wa Katiba na kipi kinakusudiwa kufanywa na serikali wakati ambapo bado Sheria haijapitishwa na Bunge.
Alisema maelekezo hayo ya Waziri Mkuu Pinda yanadhihirisha kwamba tayari serikali imeshachukua msimamo kuhusu mchakato utakaotumiwa kuandika Katiba mpya, hali inayoashiria kuwa serikali ina dhamira ya kulitumia Bunge kama muhuri (rubber stamp) ya kupitisha mchakato ambao tayari ulishapitishwa ndani ya serikali na maelekezo ya utekelezaji kuanza kutolewa kwa watendaji wa serikali ngazi ya chini kabla ya Sheria kupitishwa.
Mnyika aliendelea kusema kuwa umma unapaswa kuipokea ahadi hiyo ya Pinda kwa tahadhari kubwa kwa kuwa imeambatana na maelekezo ya kuwataka wakuu wa mikoa na wilaya wawe mstari wa mbele kuongoza mchakato huo wakati inaeleweka wazi kwamba wadau mbalimbali wamelalamikia mamlaka waliyopewa watendaji wa serikali katika mikutano ya kukusanya maoni kuhusu Katiba kwa mujibu wa muswada uliowasilishwa awali ambao wananchi walitaka vifungu husika vibadilishwe.
CHANZO: NIPASHE
No comments:
Post a Comment