ANGALIA LIVE NEWS

Monday, June 27, 2011

Wakulima Bunda wagoma kuuza pamba waliyovuna

Wakati msimu wa zao la pamba ukitangazwa kuanza, mamia ya tani za zao hilo ambayo tayari yamevunwa katika vijiji zaidi ya sita wilayani Bunda haijaanza kuuzwa na wakulima, kwa madai ya kupinga ukiritimba uliofanywa na Bodi ya Pamba nchini.

Maelfu hayo ya tani ya zao la pamba hivi sasa yamehifadhiwa katika nyumba za wakulima kama njia moja wapo ya kushinikiza bodi hiyo kuruhusu kampuni nyingi zaidi kuingia katika soko, badala ya kampuni tatu tu zilizoruhusiwa, jambo ambalo limedaiwa kuwanyima wakulima fursa ya kupata bei nzuri.
Baadhi ya wakulima waliliambia NIPASHE mjini hapa juzi kuwa, kampuni hizo zilizoteuliwa na Bodi ya Pamba licha ya kutoa bei ndogo na kwamba zimeanza kuwakopa wakulima, jambo ambalo linawakatisha tamaa.
Mwandishi wa gazeti hili ambaye ilitembelea vijiji vya Mariwanda, Hunyari, Sarawe, Mgeta, Kihumbu na Kyandege, ilishuhudia mamia ya tani za zao lapamba yakiwa yamevunwa na kuhifadhiwa ndani ya nyumba za wakulima.
Wakizungumzia hali hiyo, baadhi ya wakulima walisema wameshangazwa na hatua ya serikali wilayani Bunda kushirikiana na Bodi ya Pamba kuteua kampuni tatu tu kununua zao hilo kwa maelezo kuwa zilingia mkataba na wakulima, wakati wakitambua wazi idadi kubwa ya wakulima wanaendesha kilimo hicho pasipo mkataba wowote.
Walisema kuzuia kampuni nyingine kununua pamba katika maeneo hayo kunaweza kusababisha wakulima kuchukia kilimo hicho kwa vile wengi wao walilima zao hilo kwa kutumia fedha zao.
Mwenyekiti wa serikali ya kijiji cha Mariwanda, Samson Kisung’uda, alisema robo tatu ya wakulima katika kijiji chake hawakuingia mikataba hiyo, lakini anashangazwa kuona wanazuiwa kuuza pamba yao kwa kampuni nyingine.
Hata hivyo, Mkuu wa Wilaya ya Bunda, Francis Issac, amekiri kupata taarifa hizo lakini alisema kampuni zitakazoruhusiwa kununua pamba msimu huu ni zile ziliteuliwa na Bodi ya Pamba kwa vile ziliingia mkataba wa kutoa pembejeo kwa wakulima na si vinginevyo.
CHANZO: NIPASHE


No comments: