MAHAKAMA ya Hakimu Mkazi mkoani Arusha imekataa ombi la Wakili wa Serikali, Neema Ringo alilolitoa jana mbele ya Hakimu Hawa Mguruta la kutaka washtakiwa John Materu na Peter Marua kukamatwa baada ya kutohudhuria kesi inayowakabili wafuasi wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) inayowakabili washtakiwa 19 wakiwamo viongozi wa chama hicho.
Hakimu Mguruta alikataa ombi la Wakili Ringo la kutolewa hati ya kukamatwa kwa washtakiwa Marua na Materu kwasababu wanadharau Mahakama pia wadhamini wao hawakuwepo mahakamani hapo kutoa sababu ya washtakiwa hao kukamatwa.
Aidha Ringo pia alimtaka Hakimu Mguruta kutoa onyo kwa mshtakiwa Samson Mwigamba Mwenyekiti wa Chadema Mkoa ambaye hakuwepo mahakamani hapo wakati kesi ilipoanza saa 2:00 badala yake alifika saa 3:30 wakati kesi hiyo ilipokuwa ikiendelea hali iliyosababisha wakili upande wa utetezi, Method Kimomogoro kusimama mahakamani hapo na kumwomba Hakimu kutumia busara ili afanye mawasiliano na washtakiwa Murua na Materu ambao tangu kesi hiyo ilipoanza walikuwa wanahudhuria mahakamani bila kukosa.
Kimomogoro alimsihi Hakimu kutochukua uamuzi wa washtakiwa hao kukamatwa badala yake awasamehe leo na siku nyingine kesi hiyo itakapotajwa tena wasipofika mahakamani ndio Hakimu achukue uamuzi kwani washtakiwa hao hawana rekodi mbaya ya kutohudhuria mahakamani hapo.
Wakili huyo pia alidai mahakamani hapo kuwa mshtakiwa Josephine Slaa amepewa ruhusa na Daktari wake kuwa haruhusiwi kuhudhuria mahakamani hapo hadi atakapojifungua pia washtakiwa wengine ambao ni wabunge, Godbless Lema, Philemon Ndesamburo, Joseph Selasin na Freeman Mbowe Mahakama imewapa ruhusa kuhudhuria vikao vya Bunge na baada ya vikao hivyo kuisha watafika mahakamani hapo kusikiliza kesi inayowakabili.
Baada ya Hakimu Mguruta kusikiliza hoja za pande zote mbili aliamua kutoa maamuzi ya kutotoa hati ya kukamatwa kwa washtakiwa Marua na Materu kwa sababu hawana tabia ya kudharau Mahakama na kuongeza kuwa kesi hiyo itakaotajwa tena Julai 29 mwaka huu washtakiwa hao wawili wanatakiwa kuhudhuria mahakamani hapo bila kukosa pia hakutoa onyo kwa mshtakiwa Mwigamba ambaye alichelewa kufika mahakamani hapo.
Kesi hiyo inayowakabili washtakiwa 19 ilifika mahakamani hapo kwa ajili ya kuanza kusikilizwa lakini Mahakama ilishindwa kusikilizwa kutokana na baadhi ya washtakiwa kutokuwepo mahakamani kutokana na kuhudhuria vikao vya Bunge .
Habari Leo
No comments:
Post a Comment