Imeandikwa na Joseph Lugendo
Mama wa Taifa la Afrika Kusini, Albertina Sisulu.
MNAKUMBUKA ahadi ambazo naweza kuita amri kuu za mwana TANU za 'Binadamu wote ni ndugu zangu na Afrika ni moja...Nitajielimisha kwa kadiri ya uwezo wangu na kutumia elimu yangu kwa faida ya wote...Cheo ni dhamana sitatumia cheo changu wala cha mtu mwingine kwa faida yangu…”?
Sidhani kama leo hii kuna watu wengi wenye imani hiyo, imani ya utu iliyojaribu kuondoa matabaka katika jamii na kujenga heshima kwa kila mtu bila kujali cheo, tabaka, elimu au mali alizonazo. Si wote tunajua mwisho wa yote ni futi sita chini ya ardhi?
Sidhani kama leo hii kuna watu wengi wenye imani hiyo, imani ya utu iliyojaribu kuondoa matabaka katika jamii na kujenga heshima kwa kila mtu bila kujali cheo, tabaka, elimu au mali alizonazo. Si wote tunajua mwisho wa yote ni futi sita chini ya ardhi?
Hivi karibuni nilipata fursa ya kutembelea kwa Mzee Madiba, Afrika Kusini katika mkutano wa kuunganisha jumuiya tatu zinazoundwa na kanda za Afrika ambazo nadhani Tanzania, chini ya uongozi wa Rais Jakaya Kikwete, tulikuwa wajumbe maalumu.
Hizo ni Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC), ambayo sisi ni moja ya nchi wanachama, Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC) ambako pia sisi ni nchi wanachama na Soko la Pamoja la Nchi za Mashariki na Kusini mwa Afrika (Comesa), ambamo pia tuliwahi kuwa nchi wanachama.
Sina hakika ya nchi nyingine iliyowahi kuwa katika jumuiya zote isipokuwa Tanzania, ndiyo maana nasema ilikuwa mjumbe maalumu. Lakini, kabla ya mkutano huo, uliohudhuriwa na wakuu wa nchi hizo zipatazo 26 huku wakishuhudiwa na vigogo wa Umoja wa Afrika (AU), kulikuwa na maziko ya mwana mapinduzi, Mama wa Taifa la Afrika Kusini, Albertina Sisulu.
Rais Kikwete ndiye mkuu wa nchi pekee mbali na mwenyeji Rais Jacob Zuma, aliyekwenda katika maziko hayo na baadhi ya watu niliporudi nyumbani waliniuliza kwa nini Rais Kikwete aende peke yake na wakuu wengine wa nchi wakabaki?
Niliwajibu ni kama ilivyokuwa kwa nini Tanzania iwe SADC wakati katika jiografia haiko kusini mwa Afrika? Swali hilo alipata kulijibu Rais Kikwete akiwa Waziri wa Mambo ya Nje, kuwa mnasahau Watanzania walipigana kufa kupona, wakamwaga damu kukomboa Kusini mwa Afrika?
Likawa jibu la kujitosheleza na likawatosheleza walioniuliza. Tulisafiri kwenda Soweto katika maziko ya Mama Sisulu (92), mke wa mwanamapinduzi Walter Sisulu kiasi kwamba walipofunga ndoa, Mama Sisulu aliitwa mke wa pili kwa kuwa mke wa kwanza wa mzee Sisulu, alikuwa Harakati za Mapinduzi.
Mmoja wa Watanzania niliowakuta uwanjani katika maziko hayo, ni mwanaharakati mashuhuri, Jenerali Ulimwengu. Tulisalimiana na baada ya hapo, nilimuuliza, hivi kule nyumbani, tunaye mtu wa aina ya Mama Sisulu? Tunayeweza kumpa jina la Mama wa Taifa?
Niliuliza swali hilo kwa kuwa najua mpaka leo, hicho cheo hakipo na hatujakitunga kwa ajili ya kumpa mtu. Namfahamu kidogo Jenerali kwa historia yake katika harakati za vijana wakati wa ukombozi wa Afrika na pia harakati zake kwa sasa katika ujenzi wa demokrasia yetu.
Nilitarajia anaweza kunipa jibu la chap chap, lakini haikuwa hivyo, nikagundua wote tunawaza na hatujui nani anafaa kushika cheo hicho. Kuwa mkuu wa nchi za Kiafrika uchaguzi ndio huamua, lakini si Baba wa Taifa au Mama wa Taifa.
Cheo hicho ni heshima ambayo tabia yake ni kukubalika katika taifa na kuwa sura ya matumaini ya kila mmoja. Hakitokani na kuolewa, kuoa wala kugombea, bali utu wa mtu kwa Taifa. Sina hakika kama tunasubiri mwanamama mmoja afariki dunia ili tumpake mafuta kwa mgongo wa chupa, kama ilivyo desturi yetu ya maziko.
Nasema hivyo kwa kuwa waliofariki dunia, mpaka sasa hakuna hata mmoja tuliyempa cheo hicho; na hata walio hai, hakuna aliyepewa. Tabia nyingine ya cheo hicho, lazima ukubalike kwa kila mmoja. Ni kama ilivyo kwa Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere; Watanzania tukipata shida kidogo tunaimba; “Kama sio juhudi zako Nyerere…” Ndivyo ubaba wa taifa na umama wa taifa unavyotakiwa – alama ya umoja, alama ya kumbukumbu.
Swali langu kwa Jenerali, lilijibiwa na Rais Zuma katika hotuba yake katika maziko hayo ya kitaifa katika uwanja wa mpira wa klabu ya Orlando ulioko Soweto, alikokuwa akiishi Mama Sisulu na ndiko alikozikwa, pembeni ya kaburi la mumewe, Walter.
Rais Zuma alisema si kila nchi duniani, iliyojaliwa kuwa na Mama wa Taifa wa aina ya Mama Sisulu, nadhani kwa kuwa mababa wa taifa, wapo karibu katika kila nchi, pengine kwa kuwa wanaume wengi ndio walikuwa marais au wakuu wa nchi wa kwanza wa nchi zilizojikomboa.
Haina maana kuwa wanawake hawakuwa na mchango katika mapambano ya kutafuta uhuru, lakini labda kamzizi ka mfumo dume kalianzia mbali na kakawa na nguvu wakati wa harakati za kugawana vyeo vya baada ya ukombozi na kakazuia wengi kukosa cheo cha Mama wa Taifa.
Hata hivyo, Zuma alisema moja ya sifa ya “Ma Sisulu” kama wanavyomwita, ni kushiriki kwa nguvu zake zote kutafuta haki na kukaa pembeni wakati wa kugawana vyeo. Hakupenda vyeo.
Nikadhani hizo tabia za Ma Sisulu, zinaweza kuwa sababu ya msingi kwa Jenerali kushindwa kunipa jibu moja, la hasa nani anastahili kuwa Mama wa Taifa la Tanzania, hapa msomaji nadhani na wewe unaweza kujikuta ukikosa jibu moja.
Jenerali alisema; "wapo wanawake (anatumia wingi, anakwepa kumtaja mmoja) wa Tanzania waliotoa mchango wao nyumbani, unaweza kumfananisha Mama Sisulu na Mama Maria Nyerere na hata Mama Sophia Kawawa katika historia; yupo pia Mama Fatma Karume, hawa ni akina mama walezi wa Taifa."
Katika jibu la Jenerali, nadhani kama Afrika Kusini wasingekuwa na Mama Sisulu, mwanaharakati wa aina yake angejibu wako akina Mama Winnie Madikizela Mandela na wengineo, ambao wapo na mchango wao upo.
Tena kwa hali ilivyokuwa katika uwanja huo, Mama Winnie anayo nguvu kisiasa na sina wa kumfananisha naye hapa nyumbani. Lakini wote hao, wake wa mababa wa Taifa, wanaharakati wa kisiasa hakuna hata mmoja wao aliyepewa jina la Mama wa Taifa, isipokuwa Mama Sisulu na mumewe hakuwa Baba wa Taifa.
Yupo pia mwanamuziki Miriam Makeba (1932 –2008), aliitwa Mama Afrika, sijajua Yvonne Chaka Chaka atapewa jina gani, lakini angeweza kupewa jina hilo la Mama wa Taifa kwa mchango wao katika ukombozi wa Afrika Kusini na Afrika kwa ujumla kupitia nyimbo zao, lakini amepewa Mama Sisulu na sijui kama atapewa mwingine kwa Afrika Kusini.
Labda tuangalie nini hasa kilisababisha aitwe Mama wa Taifa wakati mke wa Baba wa Taifa yupo, lakini kaachwa, sasa katafutwa mke wa mmoja tu wa wapigania uhuru, mwanamapinduzi Walter. Na katika hilo, tujiulize yupo Mama wa Taifa Tanzania?
Albertina alianza kujifunza ujasiri akiwa mtoto, alipolazimika kuanza kulea wadogo zake akiwa na umri wa miaka 15 tu baada ya mama yake kuwa mgonjwa. Shuleni alikuwa na maendeleo mazuri na alifanikiwa zaidi katika michezo na mambo ya utamaduni ambako alionesha uwezo mkubwa wa uongozi kiasi cha kuchaguliwa Dada Mkuu akiwa darasa la tano tu.
Hata hivyo alilazimisha kuacha shule mara kwa mara kwenda kutunza wadogo zake na akalazimika kurudia shule mara kwa mara na kuwa msichana mkubwa kwa zaidi ya miaka miwili katika darasa lake.
Hakuona tabu kuwa mkubwa peke yake darasani, wala haikuwa tatizo kwa walimu wake, isipokuwa alipofanya mtihani wa kushindania kujiunga na elimu ya juu kwa miaka minne. Pamoja na kuongoza katika matokeo ya mtihani huo, hakuchaguliwa kwa madai kuwa alikuwa na umri mkubwa na nafasi yake akapewa mtu mwingine.
Walimu wa Albertina hawakuridhika, wakaandika barua kwenda katika gazeti moja la lugha ya ki-Xhosa, wakilalamikia Albertina kunyimwa haki yake. Kwa bahati nzuri mmoja wa mapadre wa Kanisa Katoliki, alisoma na kuwasiliana na uongozi wa kanisa hilo ukampatia nafasi Albertina katika chuo cha Mariazell College.
Baada ya kumaliza, alijiunga na chuo cha uuguzi katika Hospitali ya Watu weusi Johannesburg na baada ya kuanza kazi ya uuguzi, ndipo alipoona athari za ubaguzi akiwa na wauguzi wenzake kabla ya mwaka 1941, alipokutana na Walter, aliyekuwa mmoja wa vijana 'makamanda' na kuanza harakati za kumkomboa mtu mweusi.
Itaendelea wiki ijayo, kuonesha namna gani, alilea watoto wa wafungwa wa kisiasa na kuwabadilisha vijana kuwa makamanda wa kugombea uhuru wa nchi yao, mpaka akawashawishi wanawake wazungu, kuacha kuangalia Taifa likigeuka bucha, wakati wao pia wanajua uchungu wa kuzaa.
Akasema 'ukimgusa mwanamke, umegusa mwamba na si kama mwanamume, anayeweza kuchezewa.'
ITAENDELEA WIKI IJAYO.
No comments:
Post a Comment