Baraza la Maadili ya Viongozi wa Umma limezidi kuwa mwiba mkali kwa baadhi ya viongozi wa umma ambao walichelewesha kuwasilisha matamko ya mali zao kama sheria inavyotaka.
Jana Baraza hilo lilimhoji Jaji wa Mahakama Kuu ya Tanzania Kitengo cha Ardhi, Atuganile Ngwala, ambaye alishindwa kujibu maswali aliyoulizwa kuhusiana na sababu zilizomzuia kuwasilisha fomu ya tamko lake kwa wakati.
Badala ya kujibu maswali hayo, Jaji Ngwala alijikuta akimwaga chozi mbele ya Baraza hilo chini ya uenyekiti wa jaji Mstaafu, Damian Lubuva.
Jaji Ngwala aliwasili mbele ya Baraza hilo jana asubuhi katika ukumbi wa Karimjee, jijini Dar es Salaam na muda mfupi baada ya kuanza kuulizwa maswali kwa nini hajajaza fomu za maadili ya viongozi wa umma na kuziwasilisha, alianza kumwaga chozi.
Kutokana na hali hiyo, Baraza hilo lilishindwa kuendelea kumhoji na kumtaka aondoke ili kulipa jopo nafasi ya kujadili hatua za kuchukua dhidi yake.
Jaji huyo baada ya kushindwa kuzungumza na kubaki amesimama kizimbani, aliliommba Baraza hilo limruhusu awasilishe utetezi wake kwa njia ya maandishi.
Mawakili wa Baraza hilo wakizungumza na NIPASHE muda mfupi baada ya kuahirishwa kwa kikao chao, walisema Jaji huyo atawasilisha utetezi wake kwa maandishi.
Baraza hilo mwaka huu limekuwa likiwahoji viongozi wa umma ambao walishindwa kujaza fomu za kuonyesha mali wanazomiliki kama sheria ya mwaka 1995 inavyotaka na kuziwasilisha katika Sekretarieti ya Maadili ya Viongozi wa Umma.
Baadhi ya viongozi wanaokwenda kuhojiwa katika Baraza hilo wamekuwa wakilalamikia utaratibu wa kuwasilisha fomu hizo baada ya kuzijaza.
CHANZO: NIPASHE
No comments:
Post a Comment