ANGALIA LIVE NEWS

Friday, June 24, 2011

Zitto aikamata serikali pabaya

Waziri wa Fedha, Mustafa Mkulo (wa pili kushoto) akimsikiliza Mbunge wa Kigoma Kaskazini ambaye pia ni Waziri kivuli wa Wizara hiyo wakati akisisitiza jambo baada ya mabishano makali bungeni jana.
Wabunge wa upinzani, wamezidi kuipa serikali wakati mgumu, kwa mara nyingine tena jana  baada ya mawaziri waandamizi wa serikali kujikuta wakipokezana kusimama kujibu tuhuma dhidi ya Baraza la Mawaziri zilizoibuliwa bungeni na Mbunge wa Kigoma Kaskazini (Chadema), Zitto Kabwe.

 Hali hiyo pia ilimkuta Spika wa Bunge, Anne Makinda, ambaye pia alilazimika kusimama mara kwa mara kutuliza mvutano mkubwa kati ya pande hizo uliozuka bungeni, baada ya Zitto kuibua tuhuma hizo dhidi ya Baraza hilo.
Mawaziri waliosimama kumjibu Zitto ni mawaziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu, George Mkuchika (Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi)) na William Lukuvi (Sera, Uratibu na Bunge).

 Zitto alilituhumu Baraza hilo akisema  uamuzi wake wa kupendekeza Shirika Hodhi la Mali za Mashirika ya Umma (CHC) liongezewe muda wa uhai kwa miaka mitatu  kisha kuhamishia majukumu yake kwenye Ofisi ya Msajili wa Hazina ni matokeo ya ushawishi uliofanywa na wajanja kwa baraza hilo.

 Alitoa tuhuma hizo wakati akichangia mjadala kuhusu maelezo ya Azimio la Bunge la Kuongeza muda wa uhai wa CHC, lililowasilishwa na Waziri wa Fedha na Uchumi, Mustafa Mkulo, bungeni jana.

 Zitto ambaye pia ni Naibu Kiongozi wa Kambi ya Upinzani Bungeni na Mwenyekiti wa Kamati ya Fedha na Uchumi, alisema muda uliopendekezwa na serikali uongezwe kwa CHC, hautoshi kutokana na shirika hilo kutokamilisha majukumu yake makubwa.

 Majukumu hayo ni pamoja na kurekebisha Kampuni ya Reli Tanzania (TRL) baada ya Kampuni ya Rites ya nchini India kuondoka na kurekebisha Kampuni ya Simu Tanzania (TTCL) baada ya hatua ya awali ya ubinafsishaji kushindikana na mwekezaji wa Kampuni ya Airtel kuonyesha nia ya kutaka kutoka katika ubia katika kampuni hiyo.

 Majukumu mengine, ni kushughulikia uuzaji wa hisa za serikali katika Benki ya NBC (T) Limited, uperembaji wa mashirika 34 yaliyobaki na kukamilisha ufilisi wa mashirika ya umma 24 yaliyobaki.

Pia ukusanyaji wa madeni ya iliyokuwa NBC yenye thamani ya Sh. bilioni 64.9 na madai ya ubinafsishaji yenye thamani ya Sh. bilioni 15.8, ambapo mwaka juzi, CHC ilikusanya Sh. bilioni 2.6 ukilinganisha na Sh. bilioni 1.2 mwaka 2008.
 Kutokana na hali hiyo, Zitto alishauri CHC kupewa muda wa kutosha ili iweze kukamilisha majukumu yake.

 Alisema pendekezo la serikali kutaka majukumu ya CHC yahamishiwe kwenye Ofisi ya Msajili wa Hazina, ni kitu kisichowezekana katika mfumo wa uendeshaji wa mashirika ya umma nchini.

 " Hiyo ni sawa na taasisi ya kudhibiti inapewa kazi ya utendaji. Ni sawa na Ewura (Mamlaka ya Udhibiti wa Nishati na Maji), ambayo imepewa jukumu la kusimamia bei ya nishati, vipi ipewe kazi ya utendaji?” alihoji Zitto.

 Alisema pia kuna mashirika 25 ya umma, ambayo Ofisi ya Msajili wa Hazina haijui ziliko hati zake na kuhoji: “Vipi tuipe majukumu makubwa kama hayo?”

 Zitto alisema katika Kamati ya Bunge walimshauri Waziri wa Fedha na Uchumi na kukubaliana, kwamba CHC ipewe ama miaka mitano au hadi kumaliza majukumu yake ya kusimamia mashirika ya serikali yaliyobinafsishwa.

 " Ni matokeo ya ushawishi wa 'Lobbyists' (wajanja washawishi), Baraza la Mawaziri 'was ill advised' (lilishauriwa vibaya),” alisema Zitto.

 Kauli hiyo ya Zitto ilizua mabishano makali, wa kwanza kutaka uthibitisho alikuwa Waziri Mkuchika.
 Zitto alisimama na kusisitiza kuwa alichotamka ana uhakika nacho.

 Baada ya kutamka hivyo, Lukuvi naye alisimama  na kudai uthibitisho kutoka kwa Zitto kwa mujibu wa kanuni za Bunge.
Zitto alisimama na kutamka tena: “Nasema tena ni matokeo ya 'Lobbying' na  tusiruhusu tena Baraza la Mawaziri iendeshwe kwa lobbying.”

Alisema anasimama katika msimamo wake huo, vinginevyo athibitishiwe waraka wa maoni ya vyombo mbalimbali, ikiwemo Kamati ya Makatibu Wakuu wa Wizara kwa mawaziri.

 Lukuvi, alisimama na kumuomba Spika Makinda amuagize Zitto kwa mujibu wa kanuni za Bunge aeleze ni nani aliyefanya ushawishi huo na kwa namna ipi hoja kutaka Baraza la Mawaziri lilivyoshawishiwa.

 Makinda alimuagiza Zitto ifikapo Ijumaa wiki ijayo kupeleka ushahidi wa madai yake.

 Katika majumuisho yake, Waziri Mkulo aliridhia hoja za wabunge wengi waliopinga CHC kupewa kipindi hicho kifupi na majukumu yake kuhamishiwa kwa Msajili wa Hazina wakisema hawezi kumudu majukumu hayo, kwamba CHC itapewa miaka mitatu lakini jukumu lake halitahamishiwa kwa Msajili wa Hazina. Hoja hiyo itarudishwa tena Bungeni.

Wabunge wengine akiwamo Hamad Rashid Mohammed (Wawi-CUF), Alphaxard Lugola (Mwibara-CCM) na Dk. William Mgimwa (Kalenga-CCM), walipinga CHC kukabidhiwa kwa Msajili wa Hazina, wakidai imeonyesha udhaifu mikubwa katika utendaji wake.

Waziri Mkulo pia aliahidi wizara yake kufuatilia kwa karibu mno shughuli za CHC ambayo hadi sasa inafuatilia madeni ya mashirika na madai ya mashirika  ya umma 29 yaliyobinafsishwa na maendeleo yake. 

MBOWE: TAKUKURU INA UWEZO MDOGO
Naye Kiongozi wa Kambi ya Upinzani Bunge, Freeman Mbowe , alisema takwimu zinaonyesha kuwa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru) zinaonyesha kuwa bado ina uwezo mdogo wa kuchunguza na kufungua mashtaka ya rushwa.

Kauli hiyo aliitoa wakati akiwasilisha maoni ya kambi hiyo kuhusu makadirio na matumizi ya Ofisi ya Waziri Mkuu, Sera, Uratibu na Bunge, Uwekezaji na Uwezeshaji, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa kwa mwaka wa fedha za 2011/2012.

Alisema kutokana na dhaifu huo rushwa imezidi kuota mizizi katika taasisi nyeti za utawala wa umma kama ilivyoonyeshwa na matokeo ya utafiti wa ‘East Africa Bribery Index. 

Kwa mujibu wa matokeo ya utafiti huo, alisema Jeshi la Polisi lilishika nafasi ya kwanza nchini na ya tano katika ukanda wa nchi Afrika Mashariki likiwa limepewa asilimia 65.1. 

Alizitaja taasisi nyingine za kiserikali zinazofuatia kwa rushwa kwa mujibu wa utafitihuo ni Mahakama asilimia 56.4, Msajili wa Vizazi na Vifo 46.7, Idara ya Magereza  43.2, Mamlaka ya Bandari   40.8, Mamlaka ya Mapato (TRA) 37.8, Uhamiaji asilimia 37.2 na Wizara ya Ardhi  32.8

Alisema tathmini yao inaonyesha kuwa Takukuru imekuwa ikiacha kazi yake ya msingi ya kuzuia na kupambana na rushwa na kubaki ikifanya zaidi kazi za Idara ya Polisi ya Upelelezi wa Makosa ya Jinai (CID) na kwamba imekuwa ikishughulika zaidi na rushwa ndogo ndogo na kuacha rushwa kubwa. 

“Mfano mzuri ni jinsi taasisi hiyo ilivyojaribu kuwasafisha wahusika wa kashfa ya Richmond na rada," alisema na kusisitiza kuwa: “Rushwa  ni ugonjwa mkubwa ambao unalitafuna taifa na kwa kuwa imekuwa vigumu sana kwa Serikali kukabili tatizo hilo kikamilifu sababu kubwa ikiwa wapokeaji wakubwa wa rushwa wako katika serikali hii hii.”

Ili kukabiliana nayo, alisema  upinzani unaushauri iundwe kamati ya kudumu ya Bunge inayosimamia dhidi ta rushwa.

MBUNGE CCM AMLIPUA DC
Wakati huo huo, Mbunge wa Mvomero (CCM), Amos Makalla, akichangia hotuba ya Waziri Mkuu, alimtuhumu Mkuuwa Wilaya ya Mvomero, mkoani Morogoro, Fatma Mwassa, kuwa alificha chakula cha msaada na kukiuza.
Makalla alisema kuwa serikali ilipeleka tani 80,000 na kwamba kati ya huzi, tani 8,000 zilitakiwa  kugawiwa bure, lakini Mwassa alikificha na kuanza kukiuza.

Mbunge huyo alisema alitumia fedha zake kukinunua na kukigawa kwa wananchi.

Baada ya Makalla kutoa tuhuma hizo, Mbunge wa Kasulu Mjini, Moses Machali (NCCR-Mageuzi), aliombwa mwongozo wa Spika kwa kutumia kanuni namba 64 akisema kuwa kama kauli ya Makalla ni ya kweli, DC huyo anastahili kushitakiwa mahakamani na kuongeza kuwa katika nchi nyingine kosa hilo adhabu yake ni kunyongwa.

Hata hivyo, Mwenyekiti wa Bunge, Jenista Mhagama, alisema kuwa kanuni hiyo haikuwa sahihi bali zilikuwa hisia za Machali. 
CHANZO: NIPASHE

No comments: