ANGALIA LIVE NEWS

Wednesday, June 22, 2011

Jaji Bomani aeleza njia za kupata Katiba mpya

Mwenyekiti wa Kamati ya Maadili ya Baraza la Habari Tanzania (MCT), Jaji Mark Boman
Mwenyekiti wa Kamati ya Maadili ya Baraza la Habari Tanzania (MCT), Jaji Mark Bomani, amependekeza kwa Rais Jakaya Kikwete kuteua jopo au kamati ya wataalamu itakaoyokuwa na wawakilishi wa fikra mbalimbali kama njia ya kuanzia kwenye mjadala wa kupata katiba mpya nchini.
Jaji Bomani alitoa pendekezo hilo jana jijini Dar es Salaam alipokuwa akizindua kongamano la vyombo vya habari kujadili mchakato wa mabadiliko ya katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Alisema kwamba alitoa pendekezo hilo ili kuufanya mchakato huo wa kupata katiba mpya unaoendelea nchini uaminike kwa wananchi wote na kuondoa fikra kwamba serikali ina nia ya kuuteka mchakato huo.
“Kamati au jopo litakaloteuliwa na Rais ndilo litakalopendekeza hadidu za rejea, yaani mambo gani yajadiliwe na kwa utaratibu gani.Ni muhimu hadidu hizi zikawa za wazi na zikajulikana ili mjadala uwe na tija. Hata hivyo kamati au jopo hili liwe na watu wa kutosha, tuseme kati ya watu 25-4,” alisema.
Jaji Bomani alisema kwamba baada ya kuweka hadidu za rejea, pia jopo au kamati hiyo ndiyo ifanye kazi ya kupendekeza mchakato wote utakaofuatwa na ambao utashirikisha wananchi na kupendekeza vilevile aina ya tume ambayo ndiyo itakayofanya kazi ya kukusanya na kuratibu maoni ya wananchi na kutoa mapendekezo.

Alisema timu hiyo nayo inafaa iwe na wajumbe wa kutosha watakaokuwa wametokana na vyombo na makundi mbalimbali.Vile vile alisema kwamba tume hiyo ipewe nyenzo na muda wa kutosha, mwaka mmoja au zaidi wa kukusanya mawazo na kutoa mapendekezo ambayo yatawasilishwa kwa chombo maalumu (Constituent Assembly).
“Chombo hiki kitajumlisha wawakilishi wa bunge lililopo, wawakilishi wa baraza la wawakilishi la Zanzibar lililopo, wawakilishi wa serikali za mitaa,wawakilishi wa makundi mbalimbali kama vile vijana, wanawake, madhehebu ya dini, wasomi na mengine,” alisema.
Katika Kongamano hilo Jaji Bomani alitoa wito pia kwa vyombo vya habari kuielewa vyema katiba iliyopo ili viweze kuwaelimisha ipasavyo wananchi ili hatimaye waweze kutoa mchango wao kwa ufanisi katika zoezi lote la mjadala wa katiba mpya.
Mbali na kuielewa katiba iliyopo, alivitaka pia viwataarifu wananchi juu ya maoni yanayotolewa na watu mbalimbali kwenye mjadala wa katiba kwa kutoa taarifa kamili, isiyo ya upendeleo wowote kama wa kupuuza maoni ya watu fulani na kupendelea wengine.
Aidha alisema sambamba na kutoa taarifa hizo pia vichukuwe jukumu la kupima uzito wa hayo yanayosemwa na pale vinapoona kuna upotoshaji viseme hivyo na vitoe mwongozo ulio wa busara na haki.
CHANZO: NIPASHE

No comments: