Jeshi la Polisi Zanzibar limegundua mbinu mpya zinazotumiwa na wafanyabiashara wa mihadarati kuingizaZanzibar.
Ofisa Uhusiano wa Jeshi la Polisi Zanzibar, Mohammed Mhina, alisema kugundulika kwa mbinu hiyo kunatokana na kukamatwa kwa mkazi mmoja wa Kilindoni Mafya mkoani Pwani Athumani Issa Mdaba (25) aliyekuwa na mito ya kulalia iliyojazwa mafurushi ya mihadarati ndani badala ya sufi ama sponchi.
Kamanda wa Polisi mkoa wa Mjini Magharibi, Aziz Juma Mohammed, alisema hadi sasa watu watano wamekamatwa kwa tuhuma za kupatikana na kiasi kikubwa cha mihadarati na mmoja kati ya hao amekamatwa bandarini akiingiza mihadarati hiyo kwa kutumia mito ya kulalia.
Aliwataja wengine waliokamatwa kuwa ni Hamadi Saidi Omari( 38) mkoani Lindi, Mahenga Ishaka Jalumeti (39) mkazi wa Saateni mjini Zanzibar, Surea Ali Masudi (35) mkazi wa Magogoni Zanzibar na Nyange Makame Ali (61) mkazi wa Shaurimoyo mjini Zanzibar ambao walipatikana wakiwa na vifurushi 150 vya mihadarati hiyo na viroba viwili.
Alisema kuwa kukamatwa kwa watuhumiwa hao kunatokana na kupatikana kwa taarifa za siri kutoka kwa wananchi za watuhumiwa hao kujihusisha na biashara haramu ya mihadarati.
Alisema kuwa baadhi ya watuhumiwa hao ni mawakala wanaopokea mihadarati hiyo kutoka mikoa mingine ya Tanzania bara na wengine ni wasambazaji na wauzaji wa rejareja na jumla.
Naye, Kamanda wa Polisi Kikosi cha Wanamaji na Bandari Zanzibar SP Martin Lisu, alisema kuwa hivi sasa Jeshi la Polisi kwa kushirikiana na vyombo vingine vya ulinzi na usalama kama vile Maafisa wa Mamlaka ya Mapato nchini (TRA), Maafisa wa Mamlaka ya bandari nchini (THA) Usalama wa Taifa na Askari wa Vikosi vya serikali ya Mapinduzi Zanzibar, wamejenga ushirikiano mkubwa na kufanya kazi kwa pamoja.
Alisema kuwa ni kwa njia hiyo imefanikisha kumnasa mtuhumiwa huyo wa mihadarati akitokea Mafia ambaye alikamatwa bandarini hapo akiwa na mito 11 iliyokuwa na mabunda 277 ya mihadarati hiyo.
Alisema kuwa hiyo ni mara ya pili katika kipindi kisichaozidi mwezi mmoja kukamatwa kwa kiasi kikubwa cha mihadarati ikiingizwa Zanzibar kupitia bandarini ambapo mihadarati mingine ilikamatwa mwanzoni mwa mwezi huu ikiwa imefungwa kama mahindi ya kuchoma.
CHANZO: NIPASHE
No comments:
Post a Comment