Katibu Mkuu wa Chama cha Tanzania Labour (TLP), Meja Jesse Makundi, amejiuzulu wadhifa huo katika kile kilichoelezwa na Mwenyekiti wake Taifa, Augustine Mrema, kwamba ni hatua ya kujivua gamba kwa lengo la kukisafisha chama hicho.
Mrema aliwaambia waandishi wa habari mjini hapa jana kuwa Meja Makundi alifikia uamuzi huo baada ya kutajwa na ripoti ya tume iliyoundwa kwa ajili ya kuchunguza sababu za TLP kupata matokeo mabaya katika Uchaguzi Mkuu wa mwaka jana, kwamba, ni miongoni mwa viongozi wakuu wa chama hicho waliohusika katika suala hilo.
Alisema kiongozi mwingine wa kitaifa, aliyetajwa na ripoti hiyo kuhusika na suala hilo, ni Naibu Katibu Mkuu wa chama hicho, Hamad Tao, ambaye amemtaka pia kufuata nyayo za Makundi kujiengua katika nafasi hiyo.
Mrema alisema tume hiyo iliongozwa na Makamu Mwenyekiti wa TLP Zanzibar, Alhaji Hamad Mkadam, ambayo ilifanya kazi kwa muda wa miezi mitatu.
Mrema alisema baada ya kukamilika kwa uchunguzi huo, tume iliwasilisha ripoti kwenye kikao cha kwanza cha Sekretarieti ya Kamati Kuu, ambapo viongozi wote wa juu wa chama hicho walihudhuria.
Alisema katika mkutano huo, waliazimia chama hicho kutofanya kazi yoyote, mpaka watu waliotajwa na tume kwamba, wamehusika kukihujumu chama watakapojivua gamba.
Hata hivyo, alisema baada ya kutajwa kwenye taarifa hiyo, Meja Makundi, alikiri kufanya makosa na Mei 24, mwaka huu aliandika barua ya kujiondoa madarakani na kufanya nafasi hiyo kubaki wazi.
Mrema amemtaka Tao naye kuachia ngazi kwani na yeye ni miongoni mwa watu waliotuhumiwa kwenye taarifa ya uchunguzi ya Tume hiyo.
Hata hivyo Mrema alisema yeye hawezi kujiuzulu kwenye nafasi yake ya uenyekiti kwani hana makosa yoyote TLP na wala taarifa ya tume haijamtaja mahali popote.
“Kuna watu wanatangaza na kunitaka eti nijiuzulu, mimi nawaambia sijiuzulu, nijiuzulu kwa lipi? Kati watu wote waliogombea, mimi ndiye mbunge pekee niliyefanya vizuri,” alisema Mrema.
Aliongeza: “Baada ya Makundi kujiondoa, wapo waliobaki wanafanya fujo na sasa wanadai Mrema ajiuzulu, nijiuzulu kwa sababu zipi?”
Alisema yeye hawezi kujiuzulu hadi hapo uchaguzi mkuu wa TLP utakapofanyika mwaka 2014.
Kwa mujibu wa Mrema hakuna mgogoro wowote wala mpasuko ndani ya TLP isipokuwa matatizo yanaibuka kutokana na watu kueleza mambo ya chama kiholela bila kutumia vikao vya chama.
CHANZO: NIPASHE
No comments:
Post a Comment