ANGALIA LIVE NEWS

Wednesday, June 15, 2011

Julio awaacha Ngassa, Kado U-23

Kipa aliye katika kiwango cha juu nchini hivi sasa, Shabani Kado
Kipa aliye katika kiwango cha juu nchini hivi sasa, Shabani Kado na winga, Mrisho Ngassa, hawatakuwepo katika kikosi cha wachezaji wa timu ya taifa ya vijana wa umri chini ya miaka 23 watakaoondoka nchini kesho kuelekea Nigeria kwa ajili ya mechi ya marudiano na yosso wenzao wa nchi hiyo itakayofanyika Jumamosi katika mji wa Benin.

Akizungumza jana na gazeti hili baada ya mazoezi ya asubuhi, kocha wa timu hiyo, Jamhuri Kihwelu 'Julio' alisema kuwa Kado ni majeruhi wa kidole alichoumia akiwa na timu ya wakubwa, Taifa Stars, huko Jamhuri ya Afrika ya Kati hivi karibuni wakati Ngassa ameamua kumuacha ili kutoa nafasi kwa nyota wengine kuonyesha vipaji vyao.
Julio alisema kuwa katika kikosi kilichoivaa Nigeria hapa nyumbani, ameongeza wachezaji wawili tu kutoka Taifa Stars, ambao ni Mbwana Samatta na Jabir Aziz.
Alisema anaamini kwamba kikosi hicho kitapata ushindi kwenye mchezo huo wa marudiano ambao unasubiriwa kwa hamu na mashabiki wa soka nchini kwa sababu wachezaji wake wote wanaelewana na wanafahamu kwamba taifa linawategemea kuwapa furaha.
"Nimeshatengeneza vijana wapya ambao wanaweza, huu ni wakati wao na hivyo wanapaswa kuaminiwa, nitaondoka na kikosi kile kile cha ushindi mlichokiona," Julio aliongeza.
Alisema kwamba kipa wake, Juma Seif, ambaye alionekana nyota wa mchezo wakati walipoifunga Nigeria goli 1-0 kwenye uwanja wa Taifa, ndiye anayemtegemea awe mlangoni siku hiyo.
Alisema kwamba timu yao sasa itaondoka nchini kesho saa saba mchana na tayari wameshakamilisha mipango ya kuitoa Nigeria na kuweka rekodi ya kuziondoa kwenye mashindano hayo timu za Afrika Magharibi.
Kocha huyo amewataka mashabiki wa soka nchini kutowahofia wapinzani wao na wanachotakiwa ni kuwaamini vijana wao ili wakapeperushe vyema bendera ya nchi.
Tangu Jumatatu timu hiyo ya vijana imekuwa ikifanya mazoezi kwenye jua ili kujiandaa na hali ya hewa ya joto wanayotarajia kukumbana nayo waendako.
Mshindi kati ya yosso hao wa Tanzania na Nigeria atakuwa amefuzu kutinga hatua ya makundi ambayo itashirikisha nchi nane na tano zitakazofanya vizuri ndizo zitaiwakilisha Afrika kwenye mashindano ya Olimpiki London, Uingereza mwakani.
CHANZO: NIPASHE

No comments: