ANGALIA LIVE NEWS

Thursday, June 16, 2011

Katika usaliti; muda, giza si kigezo-2-GPL

TUKUMBUSHANE;
Kama atajifanya ‘msafi’ wakati wewe umetilia shaka akishapanda kitandani dai haki yako ya msingi ya tendo la ndoa, hapo ndipo penye mtihani mkubwa. Kwa sababu umemzoea, utajua tu kama ametoka kukusaliti au sivyo.
SASA ENDELEA…

HABARI za leo mabibi na mabwana, siku nyingine tena ambapo tunaangalia mada yetu ambayo ni kiporo cha wiki iliyopita. Hii si nyingine bali ni; Katika Usaliti, muda giza si kigezo… 


Kumekuwa na ushahidi wa kutosha kwamba, wapenzi wengi, mmoja anapochelewa kurudi nyumbani, ikafika saa sita na kuendelea, imani inayokaa kichwani kwa mwenza wake ni usaliti.

Dhana hii imekuwa ikiwatesa wengi kiasi cha kuvunja ndoa au uhusiano na baadaye majuto na maumivu ya moyo.
Wapenzi wengi wanaumizwa na muda na giza, wakiamini ndiyo mambo ya mapenzi hufanyika kwa sababu gizani kuna mambo mengi ya siri wakati si kweli.

Mwanamke mmoja, mkazi wa Sinza ya Kijiweni, jijini Dar es Salaam, namtaja kwa jina moja la nyumbani, mama Chris, aliwahi kufanya mahojiano na safu hii na kutoa ushuhuda kuwa, usaliti hauna muda.

Anasema: “Mimi niliolewa mwaka 2008, katika Kanisa la Mtakatifu Joseph, Posta, jijini Dar.
“Katika maisha yetu ya mume na mke, haikuwahi kutokea hata siku moja nikahisi mwenzangu anatoka nje ya ndoa kwa sababu asubuhi ya saa mbili alikuwa akienda kazini, saa kumi na moja jioni anarudi,” anasema mama Chris.

Akaendelea kusema kuwa, mumewe huyo alikuwa akisharudi nyumbani muda huo, hatoki tena mpaka kesho yake hali iliyokuwa ikimpa imani kubwa kwamba, hasalitiwi.
“Nilikuwa najiuliza moyoni atanisaliti muda gani wakati muda wa mchana yupo kazini, jioni nyumbani.”

Kipengele hiki kinamaanisha kuwa, mwanamke huyu alijenga imani kubwa kwamba, usaliti katika uhusiano mara zote ni wakati wa giza.
Lakini alisahau kwamba, alikuwa akitumikia dhana iliyopitwa na wakati, hasa kwa kizazi cha siku hizi ambacho kinakwenda na akili.

Mama Chris anaendelea kusema: “Lakini siku moja, nilikutana na shoga yangu mmoja, mama Adam, aliniuliza kama nina kifua aniambie jambo kuhusu mume wangu.
“Nilishtuka sana, nikamwambia ninacho. Akasema mara kwa mara amekuwa akimuona mume wangu saa nne au saa tano asubuhi akiingia gesti moja iliyo jirani na nyumbani kwake.
“Sikuyaamini maneno yake, ikabidi nijipage kwa ajili ya kuligundua jambo hilo kwa vile niliamini muda huo mume wangu yupo kazini.

“Siku moja asubuhi ya saa nne na nusu, mama Adam alinipigia simu kuniambia kuwa, shemeji yake, yaani mume wangu kaingia kwenye gesti hiyo akiwa na mrembo mmoja wa nguvu, mweupe pee.
“Nilichukua Bajaj na kuwahi, nikafikia kukaa nje ya nyumba ya shosti wangu huyo nikisubiri. Saa sita na nusu, mume wangu akiwa hana hili wala lile alitoka akiwa ameshikana mkono na mwanamke huyo ambaye kusema ukweli ni mzuri, ameumbika.”

Unaona mpendwa msomaji wa safu hii? Kumbe baba Chris alikuwa akitumia muda wa kazi kumsaliti mama Chris, lakini kwa sababu alikuwa anapatikana nyumbani saa kumi na moja jioni aliamini hasalitiwi.
Kuna ushahidi mkubwa na wa kutosha kwamba, wapo wanaume, wanawake ambao wapo katika agano la ndoa, wanarudi majumbani saa sita, lakini walikotokea hakukuwa na mwanamke hata mmoja.

Ndoa nyingi zinawaka moto kila kukicha kwa sababu ya muda wa kurudi na si vinginevyo. Kinachowauma wengi, ni mazingira, akiyaingiza kichwani anaamini giza, akijumlisha na tabia, sawasawa usaliti.

TABIA ZA WANAUME
Uchunguzi wa kitaalam umethibitisha kwamba, wanaume wengi wanaosaliti ndoa zao huanza mambo hayo saa kumi jioni mpaka saa  moja, akitoka hapo huenda baa (kama mnywaji) na baadaye nyumbani.

Kwa hiyo wanawake wanapolia na muda wa usiku, wanakuwa wamechelewa kwani usaliti ulishapita muda mrefu.
Utafiti pia unaonesha kuwa, wanaume ambao hawana baa maalum za kunywa, wengi wao ni wasiliti. Utakuta mwanaume leo anakunywa Miller Pub, kesho Rombo Green View, keshokutwa Yenu Bar, mtondogoo Legho Hotel, hapo inakuwaje?
Wanaume wa hivi, wakiulizwa na wake zao walipo, husema baa, wakiulizwa baa gani hujibu ‘lakini karibu tunahama’ wakihofiwa kufuatwa.

Lakini hata hivyo, katika utafiti wa muda wa usaliti, wanawake ndiyo wanaongoza kusaliti mapema zaidi kuliko wanaume.
Wanawake wengi, husaliti nyakati za asubuhi, hata ya saa mbili kabla ya kufika kazini. Jioni hupatikana nyumbani wakionekana kama ‘wasafi’ lakini kumbe hakuna lolote.
Bw. Johannes, mkazi wa Kimara ya Korogwe, jijini Dar alipowahi kuongea na safu hii alisema kuwa, wanawake hatari katika usaliti ni wale wenye tabia ya kubeba dressing table kwenye mikoba yao.

Ana maana gani? Mwenyewe anasema: “Utakuta mwanamke akienda kazini kwenye mkoba wake anaweka kioo, pafyumu, upande wa khanga, kitana kikubwa na kidogo, lips stick, poda, toilet paper  na vikorombwezo vingine kibao.

“Wanawake wa hivi, katika kumi, sita si waaminifu kwani hutumia nafasi hiyo kufanya usaliti na kujiweka sawa, akirudi nyumbani anakuwa ‘safi’. 
Johannes anasema haoni sababu ya wanawake kubeba vitu vyote hivyo kwa kisingizio cha ‘wanawake wana mambo mengi.’
Tukutane wiki ijayo na mada yetu hii.

No comments: