ANGALIA LIVE NEWS

Thursday, June 16, 2011

Pangua kubwa wakuu polisi

  Wamo MaRPC na MaRCO
  Wengine wastaafu utumishi
JESHI la Polisi nchini limefanya mabadiliko kwa mara nyingine kwa kuwahamisha baadhi ya makamanda wake wa mikoa, kuwapandisha vyeo baadhi ya maofisa na wengine kurudishwa katika makao makuu yake.
Vyanzo vya habari vya kuaminika ndani ya jeshi hilo, vimeliambia NIPASHE kuwa makamanda watakaokumbwa na uhamisho huo ni kutoka mikoa ya Pwani, Kilimanjaro, Manyara, Tanga na Kanda Maalum ya Tarime- Rorya iliyopo mkoani Mara.

Vyanzo hivyo vya habari vililiambia gazeti hili kuwa, Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Pwani, Absalom Mwakyoma, amehamishiwa Mkoa wa Kilimanjaro na nafasi yake itachukuliwa na Mkuu wa Huduma za Polisi Jamii Makao Makuu ya jeshi hilo, SACP Isaya Mngulu.
Habari zinaeleza kuwa Mwakyoma anachukua nafasi ya Lucas Ngh’oboko ambaye amestaafu wiki mbili zilizopita.
Kadhalika habari zinasema kuwa Kamanda wa Polisi Mkoa wa Manyara, SACP Parmena Sumary amestaafu na nafasi yake imechukuliwa na Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Tanga, Kamisha Msaidizi wa Polisi (ACP), Liberatus Sabas.
Kwa mujibu wa habari hizo, Kamanda wa Polisi Kanda Maalum ya Tarime/Rorya, Kamishna Msaidizi wa Polisi (ACP), Constantine Massawe, amehamishwa na kupelekwa Mkoa wa Tanga.
Vilevile ACP Deusdit Kato ambaye alikuwa Mkuu wa Upelelezi wa Makosa ya Jinai Mkoa Mara, amepandishwa cheo na kuhamishiwa Tarime/Roya kuwa kamanda wa kanda hiyo wakati Mkuu wa Polisi Wilaya (OCD) ya Musoma , SSP Emmanuel Rukura, amepandishwa cheo kuwa kamanda wa Mkoa wa Mara.
Kadhalika, jeshi hilo limefanya mabadiliko mengine kwa baadhi ya maofisa wake ambapo Afisa Mnadhimu (SO) kutoka Dar es Salaam, ACP Ngonyani amehamishiwa Mkoa wa Dodoma na SO wa Morogoro ACP Kimei atapelekwa Makao Makuu na nafasi yake itachukuliwa na ACP Lugira kutoka Chuo cha Polisi Dar es Salaam.
Wengine waliokumbwa na uhamisho wa kurudishwa Makao Makuu ni pamoja na RCO Dodoma ambaye nafasi yake imechukuliwa na SP Polycapy Urio kutoka ofisi ya RCO Dodoma. Kadhalika, mabadiliko hayo yamemkumba RCO Singida, SSP Wankyo Nyigesa, ambaye amehamishiwa Makao Makuu.
SACP Brown Lekey kutoka Makao Makuu ya Idara ya Upelelezi ya Jeshi la Polisi (CID HQTS) atakuwa Afisa Mnadhimu wa Idara hiyo baada ACP Tarimo kustaafu.
Wengine ni ACP Matei ambaye alikuwa SO Air Port na kuwa CO wa eneo hilo wakati SACP Kiponza amepelekwa Makao Makuu.
Vile vile, Ofisa wa Uparesheni Ilala, SSP Juma Ndaki, amehamishiwa Mkoa wa Tanga kuendelea na nafasi hiyo wakati Afisa Oparesheni Kanda ya Dar es Salaam, SP Sousan Kaganda, amehamishiwa Kituo cha Kati, Dar es Salaam kuwa OCD.
Msemaji wa Jeshi hilo, Advera Senso, alithibitisha kuwepo kwa mabadiliko hayo na kueleza kuwa bado yanaendelea kufanyiwa kazi na jeshi hilo na pindi yatakapokamilika, yatatangazwa.
Mkuu wa jeshi hilo, Inspekta Jenerali Said Mwema, ameshafanya mabadiliko kama hayo mara kadhaa. Februari, mwaka jana, alimteua ACP David Misime kuwa Kamanda wa Mkoa wa Kipolisi wa Temeke baada Sabas kuhamishiwa Mkoa wa Tanga.
Mabadiliko hayo pia yalimhusu aliyekuwa Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Mwanza, Jamal Rwambow kwa kurejeshwa Makao Makuu na nafasi yake kuchukuliwa na Simon Sirro. Mwezi uliofuata, Mwema alifanya mabadiliko mengine kwa kumteua Kamishna Msaidizi Mohammed Mpinga kuwa kamanda mpya wa Kikosi cha Usalama Barabarani, baada ya James Kombe, kustaafu.
Nafasi ya Mpinga ilichukuliwa na mkuu wa usalama barabarani mkoani Pwani, Mrakibu Mwandamizi Johansen Kahatano.
Katika mabadiliko hayo, alimteua ASP Advera kuwa Msemaji msaidizi wa polisi baada ya SSP Suzan Kaganda, kuhamishiwa Kanda Maalum ya Dar es Salaam kuwa msaidizi wa kitengo cha Operesheni.
Naye Ofisa Mnadhimu wa Mkoa wa Tanga, ACP Simon Mgawe, alihamishwa makao makuu ya Polisi wakati mkuu wa kikosi cha usalama barabarani mkoani Kigoma, SP Salehe Mbaga, alihamishiwa Pwani.
Mkuu wa upelelezi wa Kikosi cha Reli, SP Adolphina Kapufi, aliteuliwa kuwa ofisa Mnadhimu wa Mkoa wa Tanga na nafasi yake inachukuliwa na SP Sebastian Mbutta kutoka Idara ya Upelelezi mkoani Singida.
Mwishoni mwa mwaka jana, mabadiliko mengine alifanyika ambapo miongoni mwa waliohamishwa kutoka maeneo yao ni Charles Kenyela ambaye aliteuliwa kuwa Kamanda wa Mkoa wa Kinondoni akitokea makao makuu.
CHANZO: NIPASHE

No comments: