Juma Kaseja Juma.
Wakati kikosi cha Simba kilitarajiwa kuondoka nchini leo alfajiri kuelekea Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo kuivaa Darling Club Motema Pembe ya Kinshasa, uongozi wa Yanga umekiri kwamba ulitaka kumsajili kipa chaguo la kwanza la timu hiyo, Juma Kaseja Juma.
Mwenyekiti wa Kamati ya Usajili ya Yanga, Salim Rupia, aliimbia NIPASHE jana kuwa ni kweli kwamba uongozi huo ulijaribu kumsajili Kaseja, ambaye amesaini mkataba mpya wa miaka miwili wa kubaki Simba.
"Lakini jambo hili lilifanyika baada ya kumalizika kwa ligi kuu ya Tanzania Bara, sio jana wala juzi kama uvumi mpya unavyodai," alisema Rupia.
Uongozi wa Yanga ulidaiwa kumfuata Kaseja juzi kwa nia ya kumsajili baada ya kuona kiasi wanachotakiwa kukitoa kwa kipa, Shabani Kado, wa Mtibwa Sugar kuwa ni kikubwa. Imeripotiwa kwamba Yanga imetakiwa kutoa Sh. milioni 55, ambapo Sh. milioni 35 kwa Mtibwa na Sh. milioni 20 kwa Kado mwenyewe)
Kaseja ambaye anaonekana kwamba kiwango chake kimeshuka katika siku za karibuni, amewataka mashabiki wa timu hiyo kutokuwa na hofu yoyote kuhusu hatma yake kwa sababu ataendelea kuidakia timu hiyo.
"Nipo bado Simba, roho zenu (Wana-Simba) zitulie," alisema kwa kifupi kipa huyo ambaye anatarajia kupata upinzani mwingine wa kipa Wills Ochieng kutoka Kenya ambaye anafanya majaribio ya kutaka kusajiliwa katika klabu hiyo ya Msimbazi.
Kuhusiana na mechi ya Jumapili, Kaseja, alisema kuwa kikosi chao kiko vizuri na wanaenda Kinshasa kupambana ili kupata matokeo mazuri na hatimaye kutinga hatua ya nane bora.
"Mungu ni mkubwa na sisi tunamuomba ili tukafanikiwe, tumejiandaa vizuri na tunaamini kwamba tutapata matokeo mazuri," alisema Kaseja.
Kocha wa Simba, Moses Basena, aliliambia gazeti hili kwamba wanaenda Kinshasa kupambana ili kusonga mbele licha ya mechi hiyo kuwa ngumu.
Basena alisema kwamba watacheza kwa juhudi na anaamini goli 1-0 walilopata hapa nyumbani ni mwanzo mzuri kwao na litawafanya wapinzani wao kucheza kwa hofu.
Alisema kuwa wachezaji wake wako vizuri na kwamba mapengo aliyo nayo ni sehemu ya changamoto kuelekea msimu mpya wa ligi.
Simba imebakiwa na wachezaji 17 tu walio kwenye usajili wa mashindano hayo ya kimataifa kufuatia kuuzwa kwa baadhi ya wachezaji na wengine kuwa wagonjwa.
Basena alisema endapo watafuzu hatua ya nane bora, wataongeza wachezaji wengine katika usajili huo wa kimataifa.
Simba inahitaji sare ya aina yoyote ili kusonga mbele katika mashindano hayo baada ya kuwafunga wapinzani wao goli 1-0 hapa nyumbani.
CHANZO: NIPASHE
No comments:
Post a Comment