ANGALIA LIVE NEWS

Thursday, June 16, 2011

Mahakama yakwama kutoa hati kukamatwa Askofu Mokiwa

Jeshi la Polisi Mkoa wa Arusha, limesema limeshindwa kumkamata Askofu Mkuu wa Kanisa la Anglikana, Dk. Valentino Mokiwa, na mwenzake Stanley Konso Hotai, kwa sababu mahakama bado haijatoa hati ya kuwakamata.
Askofu Mkuu Mokiwa anatakiwa kukamatwa kwa amri ya Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Arusha, kwa madai ya kukiuka amri ya kutomsimika Askofu wa Dayosisi ya Mount Kilimanjaro, Hotai, kufuatia pingamizi lililowasilishwa mahakamani hapo na wakili wa wadai, De’suzer Junior.

Haa hivyo, kanisa hilo likiongozwa na Mokiwa lilifanya sherehe za kumfanya Hotai kuwa askofu Jumapili iliyopita, lakini lilisema halikumsimika kuwa Askofu wa Dayosisi ya Mount Meru kama ilivyoamriwa na mahakama.
Kufuatia hali hiyo, Jumatatu iliyopita, Jaji Kakusulo Sambo wa Mahakama hiyo, alitoa amri ya kukamatwa kwa maaskofu hao na kufikishwa mahakamani, lakini hati hiyo ya kukamatwa haikutolewa hadi jana.
Kaimu Kamanda wa Upelelezi Mkoa wa Arusha, Faustine Mafwele, alithibitisha jana kuwa ofisi yake haijachukua hatua yo yote ya kumkamata Mokiwa kwa sababu hawajapata amri ya mahakama inayowaelekeza kufanya hivyo.
Alisema kuna taratibu za kisheria zinazotakiwa kufuatwa kabla ya kutekeleza amri hiyo, kama vile kupewa nakala ya uamuzi uliotolewa na mahakama pamoja na hati ya kukamatwa.
Alisema ofisi yake itakapopokea nakala halisi ya uamuzi na hati ya mahakama, itatekeleza kama ilivyoagizwa.
Hata hivyo, alidai kwa kuwa hiyo ni kesi ya jinai, basi watatakiwa kufanya upelelezi wa kosa na kupeleka jalada kwa
Mwanasheria Mkuu wa Serikali ambaye naye baada ya kusoma na kuridhika atatoa kibali cha kufunguliwa kesi.
Hata hivyo, mwanasheria mmoja alipinga hatua hiyo akisema kosa la kudharau mahakama halihitaji kufunguliwa mashtaka bali husikilizwa na hakimu papo hapo kisha kutoa uamuzi.
Alisema polisi watakuwa wanajitwisha kazi ambayo haiwahusu kwa sababu amri ya Jaji Sambo aliyoitoa Jumatatu ya wiki hii, haikusema kwamba Askofu Mokiwa anatakiwa kukamatwa na kushtakiwa.
" Jaji hakusema Askofu Mokiwa akamatwe na kushtakiwa bali alisema, akamatwe na kufikishwa mahakamani, anatakiwa akasikilizwe ni kwa nini asichukuliwe hatua kwa kudharau amri ya mahakama,” alisema mwanasheria huyo wa taasisi moja ya kimataifa jijini hapa.
Lakini habari za kimahakama zilisema jana kuwa kuna taratibu ambazo zinatakiwa kutekelezwa kwanza kabla ya kutoa hati hiyo.
" Kuna ugumu bado, lakini ninachoweza kuwaelezeni ni kwamba sheria lazima itazingatiwa, hakuna suala la siasa hapa, ni sheria tu,” alisema ofisa mmoja mahakamani hapo.
Askofu Mokiwa alikaririwa na vyombo vya habari jana akisema kuwa yuko tayari kukamatwa kwa sababu anaamini hajatenda kosa lolote.
CHANZO: NIPASHE

No comments: