ANGALIA LIVE NEWS

Thursday, June 16, 2011

Nape azidi kumng'ang'ania Dk Slaa

Ally Mkoreha, Dodoma
KATIBU wa Itikadi na Uenezi wa CCM , Nape Nnauye, anazidi kumn'ang'ania Katibu Mkuu wa Chadema, Dk Willibrod Slaa, safari hii akimtuhumu kuwa yeye na chama chake siyo wazalendo wala hawana uchungu na nchi.
Hatua hiyo inatokana na kitendo cha Dk Slaa kudaiwa kutolipa kodi za serikali kupitia mshahara wake wa Sh7.5 milioni.

Nnauye alisema kitendo hicho, kinapingana na kauli ya Waziri Kivuli wa Fedha, Zitto Kabwe, alipowasilisha bungeni bajeti mbadala ya kambi hiyo inayoongozwa na Chadema kwa mwaka wa fedha 2011/12.
Alitoa shutuma hizo Dodoma jana, alipokuwa akizungumzia bajeti iliyowasilishwa na Zitto, ikijibu bajeti ya serikali kwa mwaka ujao wa fedha.
“Chadema wanakiri kupitia bajeti yao mbadala iliyowasilishwa na Waziri Kivuli wa Fedha, Zitto Kabwe kuwa kuna watu wengi wanaopata mapato makubwa, lakini hawalipi kodi. Kauli hii inapingana na matendo yao halisi, kwani itakumbukwa wanamlipa Katibu mkuu wao, Dk Willibrod Slaa, zaidi ya Sh7 milioni fedha ambayo haikatwi kodi yoyote,” alisema Nnauye.
Nnauye alisema hali hiyo inajitokeza wakati Zitto akisisitiza haja ya kila Mtanzania mwenye kipato, alipe kodi na kwamba kulipa kodi ndiyo ishara ya uzalendo na tiketi ya raia kuionyooshea kidole serikali.
“Kwa kauli hii ya Zitto, anauthibitishia umma wa Tanzania kuwa, Dk Slaa siyo mzalendo na wala Chadema pia si wazalendo. Dk Slaa alitakiwa kukataa kuchukua mshahara usiokatwa kodi na chama chake kilipaswa kupeleka kodi za watumishi wake serikalini,” alisema Nnauye.
Kuhusu bajeti mbadala ya Chadema, Nnauye alisema imedhihirisha porojo na hadaa zilizokuwa zikikitolewa na viongozi wa chama hicho wakati wa kampeni za uchaguzi mkuu mwaka jana.
Alisema licha ya mambo mengine, kupitia bajeti hiyo, Chadema imeshindwa kuonyesha kwa vitendo jinsi ambavyo ingetoa bure elimu ngazi zote, hasa ikizingatiwa kuwa hoja ya elimu bure wakati wa kampeni, ilivutia mno watu wengi.
"Waziri Kivuli anasema wataondoa ada kwa wanafunzi wa sekondari za kutwa na kupunguza ada kwa sekondari za bweni kwa kiwango cha asilimia 50 kwa wavulana na bure kwa wasichama kwa maneno mengine, Chadema wamekiri kuwa serikali haiwezi ikatoa elimu bure ndiyo maana katika bajeti yao mbadala wanakiri kuwa watapunguza ada kwa asilimia 50," alisema na Nnauye na kuongeza:
"Hakika huu ni usanii mkubwa, kumbe walikuwa wanatafuta kura za vijana hawa wakati hawana mpango nao." 

CHANZO:MWANANCHI

No comments: