ANGALIA LIVE NEWS

Monday, June 13, 2011

Marekani yajitosa umeme Tanzania

Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani, Hilary Clinton akipanda mche wa mboga katika shamba la wanakikundi cha ushirika wa kilimo cha Mlandizi mkoani Pwani, wakati alipokitembelea kujionea mradi 
Serikali ya Marekani imesema itahakikisha Tanzania inapiga hatua katika uchumi kwa kutimiza malengo ikiwemo ya kuwa na umeme wa uhakika ili kuboresha uzalishaji wa kiuchumi.
Ahadi hiyo ilitolewa jana jijini Dar es Salaam na Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani, Hillary Clinton, akisema ili Tanzania ifikie malengo ya kiuchumi iliyojipangia, ni vyema kukawa na umeme wa uhakika jambo ambalo Marekani ipo tayari kushirikiana nayo kwa kuelekeza nguvu zake kwa karibu kuhakikisha linatimia.

Waziri huyo alisema kuwa nchi yake itaisaidia Tanzania kuhakikisha inatimiza lengo lake la kuzalisha na kuingiza umeme wa megawati 300 katika Gridi ya Taifa ikikapo kabla ya mwaka 2015.
Alisema uwepo wa amani ambao ni msingi wa maendeleo na aliahidi kuifanya kazi kwa karibu ili kuwa sehemu ya mafanikio.
Waziri Hillary ambaye yupo nchini kwa ziara ya siku tatu, aliyasema hayo jana alipotembelea kituo cha kufua umeme cha Kampini ya kufua umeme ya Symbion Ubungo Dar es Salaam.
Kampuni hiyo ndiyo iliyoinunua mitambo ya kufua umeme ya Kampuni ya DowansTanzania Limited.
" Nchi yangu inatambua jitihada zinazochukuliwa na Tanzania kuhakikisha inafikia malengo ya Milenia hasa katika sekta ya umeme … hivyo itashirikiana nayo kwa karibu katika eneo hilo ili kuhakikisha mnafikia malengo hayo,” alisema Clinton ambaye yuko katika ziara ya kuzitembelea nchi tatu za Afrika za Ethiopia, Zambia na Tanzania.
Aidha, alisema kwamba ili Tanzania ifikie malengo ya kiuchumi iliyojipangia, ni vyema ikawa na umeme wa uhakika ambao utawezesha uchumi wake kukua na kutimiza malengo.
" Baada ya kutafakari na kuona jitihada za kweli zinazochukuliwa na Tanzania, serikali yetu ilikubali kuiteua kuwa miongoni mwa nchi nne duniani itakayofanya nayo kazi hasa kibiashara kwa karibu … nchi yangu itahakikisha umeme wa uhakika unapatikana hapa nchini kwenu ili kutimiza malengo,” alisema Hillary.
Waziri huyo alisema Tanzania imebarikiwa kuwa na maliasili za kutosha ikiwemo gesi asilia ambayo inaweza kutumika kufanikisha upatikanaji umeme wa uhakika.
Kwa mujibu wa Waziri Clinton, Marekani itaisaidia Tanzania katika miradi ya umeme na kuwashawishi wawekezaji wa nchi hiyo kuwekeza nchini katika miradi ya umeme.
Naye Ofisa Mtendaji Mkuu wa Symbion, Paul Hinks, alisema kampuni hiyo ina uzoefu na uwezo wa kutekeleza miradi ya umeme iliyoichukuwa kwa wakati.
Hinks alisema amefurahishwa kwa makaribisho na kupata baraka zote kutoka kwa serikali hivyo ana uhakika wa kutimiza malengo na kufanikisha adhima ya kuzalisha umeme kwa kadri mikataba inavyoelekeza.
Kwa upande wake, Waziri wa Nishati na Madini, William Ngeleja, alisema ujio wa waziri huyo nchini ni jambo muhimu na linaloleta matumaini hasa kutokana na ahadi ya kusaidia kutatua kero ya umeme nchini.
Akizungumzia mgawo wa umeme, Waziri Ngeleja alisema utaisha kabisa mara pale taifa litakapofikia malengo ya kuingiza megawati zinazohitajika katika Gridi ya Taifa.
Hata hivyo, alisema Shirika la Umeme Tanzania (Tanesco) imekuwa ikichukua jitihada mbalimbali ikiwemo kununua umeme kutoka kwa kampuni ya Symbion ili kukabiliana na kupunguza nakisi ya umeme ya megawati 260 na kwamba wiki ijayo litatangaza utekelezaji wa hatua zilizofanyika.
Waziri huyo leo anatarajia kukutana na Rais Jakaya Kikwete Ikulu jijini Dar es Salaam, kisha kuzungumza na waandishi wa habari kabla ya kumaliza ziara yake na kuondoka nchini.
CHANZO: NIPASHE

No comments: