Waziri Mkuu aliyejiuzulu kutokana na kashfa ya Richmond, Edward Lowassa
Mnyukano ndani ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) unaendelea kama kawaida safari hii ambaye ameingia kikaangoni ni kada chipukizi na Mwenyekiti wa Umoja wa Vijana wa chama hicho (UVCCM), James Ole Millya baada ya kupewa onyo kali na kuwa chini ya uangalizi kwa mwaka mmoja.
Millya ambaye katika siku za hivi karibuni amekuwa katika malumbano makali na Katibu wa CCM Mkoa wa Arusha, Mary Chatanda, amepewa adhabu hiyo kufuatia kikao cha Kamati cha Halmashauri Kuu ya Mkoa ya Chama hicho kilichokaa mjini hapa juzi.
Katika maamuzi hayo ambayo taarifa yake ilitolewa kwa vyombo vya habari jana, kikao hicho cha dharura kimebatilisha adhabu iliyopendekezwa na Kamati ya Siasa ya Mkoa ya kumvua uanachama Millya na wenzake, badala yake sasa watatumikia adhabu ya onyo kali.
Taarifa ya kikao hicho kilichokaa juzi ilifafanua kwamba badala ya kuwavua uanachama, iliridhia uamuzi wa Kamati ya Siasa ya Mkoa kwa kuwapa adhabu ambapo Millya, Mjumbe wa Baraza Kuu Mrisho Gambo, John Nyiti, Ally Bananga na Ally Majeshi wapewe onyo kali.
Millya amekuwa akitajwa kama mtetezi muhimu wa Mbunge wa Monduli (CCM), Edward Lowassa, na kuna wakati aklidaiwa kuishi katika nyumba moja ya mbunge huyo.
Ingawa mvutano wa Millya na Chatanda unaonekena katika sura ya makada wadogo, Millya akimtuhumu Chatanda kuwa amekipotezea chama nguvu mkoani Arusha kwa sababu ya kuwa na majukumu ya ubunge, picha ya ndani ni harakati ya makundi ya wawania urais wa mwaka 2015. Chatanda ni Mbunge wa Viti Maalum wa Chama hicho.
Mbali na Millya kufungwa ‘kidhibiti mwendo’ cha harakati za kisiasa, wengine waliopewa adhabu ya onyo ni kamati ya utekelezaji ya mkoa, makatibu wa vijana wilaya ambao ni Ezekiel Mollel na Ally Rajabu, na wanachama Fatuma Ngairo, Filomen Ammo na Preygod Kivuyo.
Taarifa hiyo iliyosainiwa na Chatanda ilisema kuwa waliopewa adhabu ya onyo kali watakuwa katika hali ya kuchunguzwa kwa muda usiopungua miezi 12 ili kuwasaidia katika jitihada za kujirekebisha.
Kwa upande waliopewa onyo watakuwa katika hali ya kuchaunguzwa kwa muda usiopungua miezi sita ili kuwasaidia katika jitihada zao za kujirekebisha.
Uamuzi mwingine unamtaka Millya kumuomba radhi Chatanda kwa kauli zake za matusi, kashfa na lugha za udhalilishaji alizozitoa dhidi yake. Kwa upande wake, Mjumbe wa Baraza Kuu la UVCCM Taifa, Mrisho Gambo, ametakiwa kumuomba radhi aliyekuwa mgombea ubunge kwa tiketi ya CCM katika jimbo la Arusha Mjini, Dk. Batilda Buriani, kwa kauli zake za matusi, kashfa na udhalilishaji wa kijinsia.
" Halmashauri Kuu ya Mkoa imelaani vitendo vya vijana kufanya maandamano Mei 19, mwaka huu, na kuagiza mtindo huo ukome usirudiwe tena. Hoja na malalamiko yote yafuate taratibu za vikao ndani ya chama," ilisema sehemu ya taarifa hiyo.
Maandamano hayo yanadaiwa kufanywa na kundi la wafuasi wa Millya ambao walikuwa wakishinikiza kuondolewa kwa Chatanda.
Aidha, kikao hicho kimefuta hoja ya vijana iliyotaka Chatanda aondoke kwa msingi kwamba hakuna tuhuma yoyote iliyotolewa dhidi yake.
Kikao hicho kiliitishwa juzi kuweka sawa hali ya mambo, baada ya kuzuka mpasuko mkubwa wa kisiasa ndani ya CCM Mkoa wa Arusha ukiyahusisha makundi hasimu ndani ya UVCCM kwa upande mmoja na moja ya makundi hayo dhidi ya Chatanda kwa upande mwingine.
Millya na kundi lake wanatuhumiwa kuwatetea vigogo waliotakiwa na Halmashauri Kuu ya Taifa (NEC) ya CCM Aprili mwaka huu kuwajibika kwa kuachia nyadhifa zao wenyewe kabla ya kuwajibishwa na chama kutokana na tuhuma za ufisadi.
Waliotakiwa kujivua nyadhifa zao za ujumbe wa NEC ni Waziri Mkuu aliyejiuzulu kutokana na kashfa ya Richmond, Edward Lowassa; Mbunge wa Igunga, Rostam Aziz na Mbunge wa Bariadi Magharibi, Andrew Chenge.
Rostam amekuwa akituhumiwa ama kuhusika au kuifahamu Kampuni ya Kagoda Agriculture Limited ambayo ilikwapua Sh. bilioni 40 za Malipo ya Madeni ya Nje (EPA) katika Benki Kuu ya Tanzania (BoT) kupitia kampuni hewa ya Kagoda. Jumla ya fedha iliyokwapiliwa ni Sh. bilioni 133.
Aidha, Rostam ambaye ni mfanyabiashara, anahusishwa na Kampuni ya Dowans iliyorithi mkataba tata wa Richmond kimyemela. Hata hivyo, amekanusha kuhusika na kashfa hizo. Chenge anahusishwa na kashfa ya ununuzi wa rada ya kijeshi wakati huo akiwa Mwanasheria Mkuu wa Serikali. Rada hiyo iliigharimu Tanzania zaidi ya Sh. bilioni 40, huku theluthi moja ikitolewa kama kamisheni kwa waliofanikisha ununuzi huo.
Bei hiyo ilizua taharuki kubwa nchini Uingereza ambako Kampuni ya BAE ya kuuza vifaa vya kijeshi baada ya kuwa kwenye uchunguzi mzito wa makachero wa makosa makubwa ya jinai wa Uingereza (SFO), walikubali yaishe kwa kukiri kosa la kuwa wazembe kwa kutokuweka rekodi za kiuhasibu sawa. BAE wamekubali kulipa Sh. bilioni 30 kwa Tanzania kama fidia.
Sakata la Arusha limejifunua katika sura ya kuhasimiana kisiasa, huku kundi la Millya limekuwa likidai kuwa kundi la Gambo kwa kushirikiana na Chatanda walihusika kumhujumu Dk. Burian na kushindwa katika uchaguzi wa mwaka jana na Jimbo la Arusha Mjini kuchukuliwa na Godbless Lema (Chadema).
Adhabu ya onyo kali kwa Millya linaweza kumuathiri Lowassa kisiasa kutokana na kutajwa kuwa ameshaanza maandalizi ya kugombea urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania mwaka 2015, baada ya Rais Jakaya Kikwete kumaliza muda wake.
CHANZO: NIPASHE
No comments:
Post a Comment