ANGALIA LIVE NEWS

Monday, June 13, 2011

Posho za wabunge za moto

Upinzani dhidi ya posho kwa wabunge umezidi kupamba moto, baada ya wabunge wanne wa NCCR- Mageuzi, kuunga mkono uamuzi wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) wa kuiomba serikali iwafutie wabunge posho za vikao, wakisema kuwa hazina sababu kwani hiyo ni sehemu yao ya kazi.

Vile vile, wabunge hao leo wanatarajia kuwasilisha barua kwa Waziri wa Fedha, Mustafa Mkulo, ili akate posho zao na kuzihamishia kwenye fungu la maendeleo la Mkoa wa Kigoma, wakisema posho hizo hazina uhalali.
Wabunge hao David Kafulila (Kigoma Kusini), Felix Mkosamali (Muhambwe), Agripina Buyogera (Kasulu Vijijini) na Moses Machali wa (Kasulu Mjini), walitoa msimamo wao jana mjini hapa wakati wakizungumza na waandishi wa habari kwenye ofisi za Bunge.
Akizungumza kwa niaba ya wenzake, Kafulila alisema watapeleka hoja binafsi bungeni ili kuliomba litengue sheria inayoruhusu wabunge kulipwa posho hiyo.
Alisema wanataka pia posho nyingine wanazopata wabunge zikatwe kodi ili kuongeza makusanyo ya fedha za ndani.
Kafulila alisema kwa kuwa wabunge wanalipwa mishahara na fedha za kujikimu wanapotekeleza majukumu ya kibunge nje ya Bunge, hakuna sababu tena ya kulipwa posho za vikao.
“Hii hoja si ya kishabiki, ni hoja ya uhalali wa malipo yenyewe, mbunge analipwa mshahara na fedha za kujikimu anapotekeleza kazi za kibunge nje ya Bunge, hii posho ya vikao inakosa uhalali kwa sababu vikao ni sehemu ya kazi ya mbunge,” alisema.
Wabunge hulipwa posho ya Sh. 80,000 kwa kila kikao. Alisema wabunge wote wanapaswa kuunga mkono hoja hiyo kwani fedha wanazolipwa kwa vikao ni haramu na badala yake zielekezwe kwenye bajeti za maendeleo kwa mikoa wanayotoka. “Tutawashangaa wabunge wasiounga mkono hoja hii maana watakuwa wanakubali kulipwa malipo haramu, kesho (leo) tunampa barua Mkulo akate malipo haya, hatuyataki maana hayana sababu na ni ufisadi tu wa fedha za walipa kodi,” alisema Mbunge wa Muhambwe Felix Mkosamali.
Mkosamali alisema watawasilisha pia hoja ya kutaka vyeo vya wakuu wa wilaya na makatibu tarafa vifutwe kwani navyo vimekuwa mzigo mkubwa kwa uendeshaji wa serikali bila sababu.
Alisema mkurugenzi wa halmashauri peke yake anaweza kusimamia maendeleo na mambo yakaenda, hivyo kuwepo kwa wakuu wa wilaya ni kupoteza fedha.
Alisema iwapo vyeo hivyo vitafutwa, serikali itaokoa Sh. bilioni 200 ndani ya miaka mitano ambazo zinatosha kununua mitambo ya kuzalisha megawati 200 za umeme.
Kuhusu kauli ya Mkulo kuwa serikali imepanga kupunguza matumizi yasiyo ya lazima, Kafulila alisema kauli hiyo ni danganya toto kwani haijasema itaokoa kiasi gani kwa kupunguza matumizi yasiyo ya lazima.
Kafulila alisema fungu lenye matumizi hayo limeongezewa fedha kutoka Sh. trilioni 2.8 mwaka 2010/2011 hadi Sh. trilioni tatu katika bajeti ya mwaka wa fedha 2011/12.
Alisema ni aibu kubwa Waziri wa Fedha kuendelea kulilia misaada kwa wahisani na kulalamika wanaposhindwa kutekeleza miradi.
Kafulila alisema ni aibu pia Tanzania kuwa miongoni mwa nchi saba zinazopata misaada mikubwa kutoka mashirika ya kimataifa na wahisani.
Alisema nchi zilizopo kundi moja na Tanzania kwa kupata misaada mingi, nyingi ziko katika vita na hali mbaya ya kiusalama. “Nasema hii ni aibu kubwa kwa Tanzania yenye amani kusaidiwa sawa na mataifa yenye hali tete ya kiusalama, hii ni aibu lazima tujenge uwezo wa kujitegemea, wakati bajeti ya maendeleo ni asilimia 35 ya bajeti yote, pesa za ndani zilizotengwa kwa maendeleo ni trilioni 1.8 tu hii si sifa kabisa lazima tufanye jitihada tutoke hapa,” alisisitiza.
Alisema tatizo la Tanzania sio ukuaji wa uchumi bali ni maendeleo ya uchumi kwakuwa ukuaji wa uchumi unapimwa kwa kiwango cha uzalishaji ndani ya nchi na namna mapato ya ndani yanavyotumika kuboresha maisha ya watu.
Alisema ukuaji wa uchumi wa Tanzania ambao ni asilimia saba mpaka sasa ni ukuaji wa juu sana na Tanzania ni miongoni mwa nchi 20 zenye kasi kubwa ya ukuaji wa uchumi, lakini vile vile ni miongoni mwa nchi 20 maskini zaidi duniani. “Nidhamu ya ukuaji wa uchumi wetu bado ina walakini kutokana na serikali kushindwa kuhakikisha uimara wa sarafu yetu na kupanda kwa gharama za maisha kusikoendana na pato la Mtanzania,” alisema. Alisema ndio maana wakati serikali ya awamu ya nne ikiweka rekodi ya kupandisha mapato kutoka Sh. bilioni 260 mwaka 2005 hadi Sh. bilioni 470 mwaka 2011 ambalo ni ongezeko la asilimia 80, huo sio ukuaji halisi wa makusanyo kwa mwezi bali ni matokeo ya udhaifu wa sarafu kiushindani.
“Hii ni kwa sababu mwaka 2005 wakati mapato ya ndani yakiwa Sh. bilioni 260 thamani ya sarafu imara kama Dola ilikuwa Sh. 1,000 kwa Dola moja, na leo wakati mapato ni Sh. bilioni 470, Dola moja ni sawa na Sh 1,600 hivyo basi kwa tafsiri ya Dola, mapato yetu ya mwezi yamepanda kutoka Dola milioni 260 mwaka 2005 hadi Dola milioni 269 mwaka huu sawa na ongezeko la asilimia 13 na sio asilimia 80 kama tunavyoambiwa,” alisema.
Ijumaa iliyopita, Chadema kilisema hoja ya kufuta posho za vikao kwa wabunge na watumishi wengine wa serikali ni hoja ya chama hicho na kwamba kwa kufanya hivyo fedha za walipakodi zaidi ya Sh. bilioni 900 zitaokolewa kwa mwaka.
Mwenyekiti wa chama hicho, Freeman Mbowe, aliwaambia waandishi wa habari mjini Dodoma kuwa mapendekezo hayo yatatolewa kama sehemu ya bajeti ya kambi ya Upinzani watakayoiwasilisha bungeni keshokutwa.
“Hoja hii ichukuliwe kama hoja sensitive (muhimu) na isichukuliwe kama hoja ya kuleta migogoro miongoni mwa Zitto (Kabwe) na wabunge ama wabunge wa Chadema na wabunge wengine,” alisema Mbowe.
Alisema wabunge na watumishi wengine wa serikali wamekuwa wakipata posho wakati wa vikao licha ya kwamba wamekuwa wakipata mshahara kila mwezi. Alitoa mfano wa mbunge ambaye amekuwa akipata posho ya kujikimu na vile vile akihudhuria bungeni anapewa posho wakati hiyo ni kazi ya mbunge.
Wakati wabunge wa Chadema na NCCR-Mageuzi wakitoa msimamo wa kuzikataa posho, wabunge wa upinzani, Augustine Mrema (TLP) na John Cheyo (UDP) hawajalitolea uamuzi suala hilo.
CHANZO: NIPASHE

No comments: