Vinoth Praveen
Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Dar es Salaam, imemuhukumu Vinoth Praveen (25), mwenye asili ya Kiasia adhabu ya kunyongwa hadi kufa, baada ya kupatikana na hatia ya kumuua mfanyabiashara, Basit Abdallah.
Hukumu hiyo ilitolewa jana na Jaji wa Mahakama hiyo, Dk. Fauz Twaid baada ya ushahidi ulitolewa na upande wa mashtaka kuwa alitenda kosa hilo. .
Jaji Twaid alisema Mahakama hiyo inakubaliana na upande wa mashtaka pasipo shaka kuwa Praveen alihusika na mauji hayo kwa kukusudia.
Ilidaiwa kuwa mtuhumiwa huyo baada ya kumuua Basit, aliyekuwa mkazi wa Dar es Salaam aliuweka mwili wake ndani ya begi la nguo kisha kuufungia kwenye gari na kulitelekeza kwenye maegesho ya magari ya jengo la JM Mall (sasa Harbour View Tower).
Ilidaiwa kuwa alimuua mfanyabiashara huyo kwa kutumia visu na mishale Februari 6, mwaka 2009 baada ya kumuita nyumbani kwake Mtaa wa Kipata uliopo Kariakoo katika Manispaa ya Ilala .
Hata hivyo, Jaji Twaib alipinga utetezi ambao ulitolewa na Praveen kwamba alimuua mfanyabiashara huyo kwa nia ya kujitetea baada ya kuanza kumpiga na fimbo mgongoni na miguuni.
Jaji huyo alisema mahakama ilipima mazingira ya kesi hiyo na kubaini kuwa mtuhumiwa huyo alikuwa amekusudia kufanya kosa hilo kwani katika utetezi alioutoa wakati alipokuwa akihojiwa polisi ulikuwa ni tofauti na ule alioutoa mahakamani.
Katika utetezi wake, mtuhumiwa huyo wakati akichukuliwa maelezo ya onyo na Inspekta Mapunda, alikiri kuua na kusema hakuhitaji shahidi yoyote kuwepo kwani wakati anaua alikuwa peke yake.
Inadaiwa kuwa mtuhumiwa huyo alikuwa anadaiwa na mfanyabiashara huyo Dola za Marekani 20,000
Aidha, Jaji Twaib alitupilia mbali utetezi wa mtuhumiwa huyo ulioungwa mkono na hoja za mwisho za wakili wake, Majura Magafu, aliyekuwa akisaidiana na wakili Irene Maira, kuwa mshtakiwa alitenda kosa hilo wakati akijitetea na badala yake alikukubaliana na hoja za upande wa mashtaka zilizotolewa na Wakili wa Serikali, Shadrack Kimaro, akisaidiana na Cecilia Mkonongo kuwa kulingana na mazingira ya tukio hilo, alitenda kosa hilo kwa kudhamiria.
Jaji huyo alisema mtuhumiwa huyo alikusudia kufanya kosa hilo kutokana na ushahidi kuonyesha kuwa mfanyabiashara huyo alichomwa visu mara nane katika sehemu za mgongoni na shingoni na pia alikutwa na vipande vya mshale mdomoni.
Dk. Twaib alisema hata kama alikuwa akijitetea kama alivyodai kuwa mfabyabiashara huyo ndiye aliyeanza kumpiga, lakini alitumia nguvu kubwa kupita kiasi katika kujitetea.
Alisema mtuhumiwa huyo alipokuwa akihojiwa na Inspekta Mapunda ni kwa nini aliamua kutumia visu viwili wakati alikuwa akijitetea, alisema ni kwa sababu havikuwa imara na kwamba alitumia na mishale kwa sababu alitaka kumuua kwani kama angepona yeye (mtuhumiwa) angekuwa katika wakati mgumu.
Alisemamazingira hayo yanaonyesha dhahiri kuwa alikusudia kufanya kitendo hicho.
Alisema kwa mujibu wa sheria, adhabu ya kosa la mauaji ya kukusudia mtuhumiwa anatakiwa kunyongwa hadi kufa ingawa ana haki ya kukata rufaa.
Baada ya hapo Jaji Twaib alimhukumu mtuhumiwa huyo kunyongwa hadi kufa.
Mapema, mtuhumiwa huyo alikuwa akishtakiwa na mke wake, Komal Bhupende (23), kabla ya Bhupende kufutiwa shtaka lake baada ya kuonekana hana hatia.
Baada ya hukumu hiyo, ndugu na jamaa wa mtuhumiwa huyo walionekana wakiwa katika masikitiko na askari kumfunga pingu kisha kuondoka naye.
CHANZO: NIPASHE
No comments:
Post a Comment