ANGALIA LIVE NEWS

Tuesday, June 21, 2011

RC ajitosa mgogoro wa nyumba ya Kawawa

Mkuu wa Mkoa wa Dodoma, Dk. James Msekela, ameahidi kukutana na familia ya Waziri Mkuu Mstaafu, Hayati Rashid Kawawa, ili kuangalia uwezekano wa kutatua mzozo wa nyumba iliyopo eneo la Uzunguni, Kilimani mjini hapa.
Akizungumza na gazeti hili ofisini kwake jana, Dk. Msekela alisema wao kama serikali hawapendi kuiona familia hiyo ikiishi katika mzozo.

“Sisi kama serikali tutakaa na pande mbili za familia hiyo kuona jinsi ya kuutatua mzozo huo kwasababu tunapenda kuiona familia hiyo ikiishi katika amani.
Alisema jana alitaka kukutana na familia hiyo, lakini kutokana na mtoto mkubwa wa familia hiyo, Mbunge wa Namtumbo, Vita Kawawa, kuwa safarini nchini Ufaransa ameona si vema kuzungumza na familia hiyo bila yeye kuwepo.
Alisema anaamini kuwa matatizo hayo ni ya kifamilia, lakini ameamua kufanya hivyo kwa sababu serikali inapenda kuona familia hiyo ikiishi kwa amani.
Alisema Jumamosi alimuagiza Mkuu wa Wilaya ya Dodoma, John Tupa, kwenda katika familia hiyo kwa sababu alikuwa na majukumu mengine ya kikazi.
Juzi, Tupa alisema  aligundua kuwa mambo hayo ni ya kifamilia na yanahitaji kutatuliwa ndani ya familia.
Jumappili vyombo vya habari viliripoti kuhusiana na mzozo huo ambapo vilisema familia hiyo imeapa kuwa itapigania kulinda heshima ya mwanasiasa huyo baada ya kuwapo tishio la nyumba hiyo kuuzwa na kupangishwa na mama yao wa kambo, Asina Kawawa, ambaye anadai kuwa nyumba hiyo ni mali yake na kwamba anataka kupangisha kwa amadai alirithishwa na Mzee Kawawa.
CHANZO: NIPASHE

No comments: