ANGALIA LIVE NEWS

Tuesday, June 21, 2011

Ngassa kuivaa Man U Marekani

Mshambuliaji wa timu ya Azam inayoshiriki Ligi Kuu ya Tanzania Bara, Mrisho Ngassa
Mshambuliaji wa timu ya Azam inayoshiriki Ligi Kuu ya Tanzania Bara, Mrisho Ngassa, anatarajiwa kuwavaa mabingwa mara 19 wa Ligi Kuu ya England, Manchester United, katika mechi ya kirafiki itakayofanyika Marekani Julai 20 akiwa na timu ya Seattle Sounders ya huko.

Akizungumza jana jijini Dar es Salaam, Makamu Mwenyekiti wa Seattle Sounders, Lance Lopes, alisema kuwa Ngassa ataondoka nchini kati ya Julai 6 au 7 kwenda Marekani kwa ajili ya kufanya majaribio na klabu hiyo kwa wiki mbili.
Lopes alisema kuwa lengo la kukubali kumchukua Ngassa kwenda kufanya majaribio Seattle na kumpa nafasi ya kucheza katika mechi hiyo ya kirafiki dhidi ya klabu hiyo iliyocheza fainali za Klabu Bingwa Ulaya hivi karibuni, ni kutangaza soka la Tanzania.
"Lengo letu katika kushirikiana na klabu za Tanzania ni kutaka kuendeleza vipaji vya wachezaji chipukizi na baadaye tutaendelea kwa mfumo wa kupitia vituo vya soka," alisema kiongozi huyo ambaye pia aliishukuru serikali ya Tanzania kwa kuruhusu kuendelea na mchakato huo wa kuitangaza nchi kimataifa.
Alisema kuwa mbali na soka pia klabu hiyo ina mikakati ya kushirikiana na Tanzania katika nyanja mbalimbali za uwekezaji, utalii na masuala ya kijamii.
Mwenyekiti wa Azam, Saidi Mohammed, alisema kuwa klabu yake imefurahishwa na jitihada zilizofanywa na wenzao wa African Lyon kwa kufanikisha Ngassa kupata nafasi hiyo ya kucheza dhidi ya klabu hiyo kubwa duniani.
Mohammed alisema kuwa kutokana na klabu hiyo kuwa na malengo ya kuendeleza vipaji, imeridhia mchezaji wake kwenda kufanya majaribio nchini Marekani na itakuwa ni nafasi muhimu kwake kujifunza mambo mbalimbali katika muda huo yatakayomsaidia kuendeleza kiwango chake.
"Ngassa atakuwa ni mchezaji wa kwanza wa Tanzania kuivaa Manchester United na fursa hiyo ni muhimu sana kwake na ni jambo la kujivunia kwake na kwa klabu yetu, pia inaweza ikawa ndio ufunguo wa kupata klabu ya kuichezea huko Marekani au kwingine duniani," alisema kiongozi huyo wa Azam.
Aliongeza kwamba klabu yake itaendelea kuwaruhusu wachezaji wake pale watakapopata nafasi za kwenda kufanya majaribio nje ya nchi kwa sababu wanaamini kwamba ndipo maendeleo ya soka la Tanzania yatakapoanza.
Ngassa ambaye pia ni tegemeo katika kikosi cha timu ya taifa, Taifa Stars, aliwahi kwenda kufanya majaribio katika klabu ya West Ham United ya England lakini hakufuzu na kurejea nchini kuendelea kucheza soka wakati huo akiwa na Yanga.
Kiongozi wa African Lyon, Rahim Zamunda, alisema kwamba baada ya kupata nafasi hiyo waliamua kumchagua Ngassa kwa sababu ndiye mchezaji mwenye kiwango cha juu nchini.
CHANZO: NIPASHE


No comments: