Fumbo la mauaji ya kinyama kabisa kuwahi kukumbwa wanafunzi, bado halijapata kufuatia kuuawa kwa mwanafunzi wa darasa la tano katika Shule ya msingi ya bweni ya Living stone English Medium iliyopo Wilaya ya Njombe mkoani Iringa.
Wakati Polisi, mkuu wa wilaya na mkuu wa shule wakiwaomba wananchi wawe watulivu, hofu na simanzi bado vimetanda kwa wazazi wenye watoto wanaosoma katika shule hiyo.
Kifo cha mwanafunzi huyo, Doris Lutego (12), kimepokelewa kwa hisia tofauti na wakazi wa mji huo baadhi wakihisi ni tukio lililopangwa muda mrefu na wauaji huku wengine wakidhani ni chuki.
Doris aliuawa kwa kuchinjwa huku kichwa chake kikitenganishwa na kiwiliwili, baada ya kutekwa na kundi la watu wasiojulikana waliongia katika eneo la shule hiyo Jumapili iliyopita majira ya saa 9:00 alfajiri kwa njia ya kificho na kuvamia bweni la wasichana linaloitwa Star.
Baada ya kuvamia bweni hilo lililopo pembezoni kidogo na majengo ya utawala, wavamizi na wauaji hao walifungua dirisha dogo la kioo, lililopo upande wa kulia, karibu na mlango wa kuingilia bweni hilo na wakafanikiwa kulifungua bila ya kulivunja.
Hata hivyo, dirisha hilo halikuwa na nondo zilizojengewa katikati yake kama vizuizi, hivyo ilikuwa rahisi kwao kumvuta na kisha kumchomoa Doris kupitia dirishani.
Mwandishi wa NIPASHE alipotembelea shule hiyo, alibaini kuwa madirisha ya mabweni yote hayana nondo kutokana na maelekezo ya serikali kwamba madirisha yasiwekwe nondo kwa sababu ya kuwasaidia wanafunzi kujiokoa wakati wa majanga ya moto yanapotokea. Hata hivyo, wakati tukio hilo linafanyika inaelezwa kuwa Doris na wanafunzi wenzake walikuwa wamelala huku yeye (marehemu) akikuwa amelala katika deka la juu (kitanda) na alikuwa pembezoni mwa dirisha hilo. Inaelezwa kuwa baada ya kutoroshwa, ilikutwa damu na jino katika eneo hilo na michirizi ya damu katika dirisha lililotumika kumpitishia.
UCHUNGUZI WA JESHI LA POLISI
Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Iringa, Evarist Mangalla, anasema kuwa kesho yake (Jumatatu) kati ya saa 3:00 na saa 4:00 asubuhi, mwili wa mwanafunzi huyo ulipatikana kilomita 10 kutoka shuleni hapo, ukiwa umetelekezwa baada ya kuuawa.
"Kichwa cha mwanafunzi huyo baada ya kuchinjwa kilikutwa karibu na makazi ya Romanus Menas Mdugo (36), dereva teksi, kikiwa kimehifadhiwa ndani ya begi na kuzungushiwa mawe katika mtaa wa Zengerendete bila kiwiliwili," alisema na kuongeza: "Kiwiliwili cha mwili wake kilikutwa nje ya banda la biashara la Mke wa Mwenyekiti wa Kitongoji cha Kambarage, Pancras Stephano Matinya (51), kikiwa kimehifadhiwa kwenye mfuko wa sandarusi na kuzungushiwa nyasi."
OPERESHENI YA KUSAKA WAUAJI
Baada ya tukio hilo, Mkuu wa Wilaya ya Njombe, Sarah Dumba, aliitisha kikao cha kamati ya ulinzi na usalama na kufikia maamuzi ya kuomba nguvu zaidi ya askari kutoka kwa Kamanda Mangalla kwa ajili ya kuendesha msako. Juni 14, mwaka huu, Kamanda Mangalla alitangaza jeshi la Polisi linawashikilia watu watatu wakituhumiwa kuhusishwa na tukio hilo.
Aliwataja walituhumiwa waliokamatwa kuwa ni fundi wa magari, Christopher Msigwa (25), mkazi wa Kambarage; wakulima wawili Michael Msemwa (32) na James Mtulo (20), wote wakazi wa mtaa wa Zengerendete wilaya ya Njombe.
WALEZI, WALINZI WAHOJIWA
Hata hivyo, hadi juzi jioni walezi wote wa wanafunzi (matrons) pamoja na walinzi wa watatu wa shule hiyo walikuwa wakihojiwa na Polisi kuhusiana na tukio hilo.
BABA WA DORIS: SIAMINI, NAIACHIA DOLA
Baba mzazi wa marehemu Doris, Edson Lutego (51), mkazi wa mtaa wa Mwembetogwa katika Halmashauri ya mji mdogo wa Makambako ni kama haamini kilichotokea. "Sina ninachoweza kukueleza ila tu nilionyeshwa sehemu ambapo mwanangu alipotolewa kwa kupitishiwa dirishani, karibu na alikokuwa amelala…yaani mimi kiujumla bado akili yangu haijakaa vizuri, sijui hata nikwambie nini ndugu mwandishi maana mimi nilipigiwa simu alfajiri ya Juni 12 kwamba kuna tukio limetokea shuleni na mwanangu hayupo,” alisema Lutego ambaye ni mfanyabiashara wa duka la jumla la soda na vinjwaji baridi alipozungumza na NIPASHE nyumbani kwake juzi Mwembetogwa, Makambako.
Alisema alifunga safari akiwa peke yake na baada ya kufika na kuliona dirisha lililotumika kumtoa mtoto wake bwenini, walifuatilia kwa umakini michirizi ya damu na baadaye ikawa haionekani tena, lakini hawakuwa na uhakika kama Doris alikuwa ameuawa. Alisema baadaye alitaarifiwa kwamba mtoto wake alipatikana akiwa amekufa kwa kuuawa kikatili na kichwa chake kutenganishwa na kiwiliwili.
"Sikuwa na jinsi baada ya kuuona mwili wake ila nilikubali kilichotokea na nimemzika Doris jana (Jumanne) kijijini kwetu Ikingula kwenye makaburi ya familia; ni umbali wa kama kilomita 12 hivi kutoka hapa Makambako," alisema Lutego.
Akisimulia maisha ya familia yake, alisema Doris ni mtoto wake wa nne kuzaliwa, akitanguliwa na dada zake wawili, Devota na Diana pamoja na kaka yake, Lwimiko ambao wote waliachwa na mama yao, marehemu Jermana Mgata, ambaye alifariki dunia mwaka 2006. "Mimi naamini kwamba mkono wa dola ni mrefu, sina shaka na hilo maana najua iko siku moja ukweli utapatikana na mbaya wangu atajulikana; kwa maana Mungu ni mwema na anaweza,” alisema na kuongeza: "Ila naiomba tu serikali ifanye kila liwezekanalo hao wauaji wapatikane na wachukuliwe hatua kali za kisheria."
MAZINGIRA YA SHULE YAKO SALAMA KIASI GANI?
Shule ya Living Stone imejengwa kwa kufuata kanuni na taratibu za serikali zinavyotaka shule za bweni ziwe.
Imejengwa mbali na mji, lakini mazingira yake ni rafiki kwa wanafunzi na imejengewa uzio wa mimea na mbao.
Uzio huo ambao unakadiriwa kuwa na urefu wa futi nne, kuna sehemu ambayo umeachia na ndiko kunasadikiwa wauaji hao walipitia. Kuna lango kuu la kuingia shuleni hapo, ambalo limetengenezwa kwa vyuma na ni kawaida kuwa na mlinzi wakati wote. Kila mlinzi wa shule hiyo anatumia rungu wakati wakiwa kwenye lindo lao.
Milango na madirisha ya mejengo ya shule ni makubwa kiasi cha kutosha, na ni rahisi kupitisha wanafunzi wengi kwa mkumpuo kama likitokea janga lolote kama la moto. Siku ya tukio inadaiwa kulikuwa na walinzi watatu, lakini baada ya tukio hilo inadaiwa alionekana mlinzi mmoja tu, huku wengine wakiwa hawapo.
Walinzi wote wanaisaidia polisi kwa sasa. NIPASHE haikufanikiwa kumpata mwalimu mkuu baada ya kuelezwa alikuwa amekwenda mjini Iringa ambako alifuatana na wakaguzi wa elimu kanda waliokuwa wamefika shuleni hapo kukagua shule hiyo kufuatia tukio la juzi.
Kuna kitendawili kigumu ambacho hakijatenguliwa kama wauaji hao walikuwa wanamlenga Doris pekee au ni mwanafunzi yeyote tu, kwani walimpata kirahisi kwa sababu kitanda chake kiko dirishani.
Hata hivyo, kwa jinsi mauaji yalivyofanyika imekuwa ni vigumu kujua kama wanafunzi wengine walikuwa wamelala usingizi wa namna gani kiasi cha kushindwa kusikia aina yoyote ya kelele au kishindo wakati mwenzao akichukuliwa kinyama.
Shule hii kwa miaka mitatu mfululizo imekuwa na mafanikio makubwa kitaaluma, mwaka jana iliongoza katika wilaya ya Njombe kwa kushika nafasi ya kwanza ikifaulisha wanafunzi wote 26; huku ikiwa ya tatu kwa mkoa wa Iringa. Imekuwa katika mafanikio hayo kwa miaka mitatu sasa.
SALAAM ZA DC NJOMBE
Mkuu wa Wilaya ya Njombe, Sarah Dumba, akizungumza wakati akiwa ameungana na wakazi wa mji wa Makambako katika mazishi ya mwanafunzi huyo alisema kuwa:"Serikali imesikitishwa sana na mauaji hayo ya kikatili, iko pamoja na wananchi wote katika maombolezo kuhusiana na tukio hili…ila ninawaombeni muwe watulivu kwa wakati huu ambao Jeshi la Polisi likiwa linaendelea kufanya uchunguzi wa tukio hili kwa vile ukweli wake utapatikana.”
MMILIKI WA SHULE ASIMULIA MKASA
Living Stone English Medium, inamilikiwa na Mkazi wa Kata ya Ramadhani katika Halmashauri ya mji wa Njombe, Alfred Luanda. Katika mahojiano yake na NIPASHE, Luanda alisema kuna mengi yamejificha katika sura ya kawaida ya tukio zima, tangu kutekwa hadi kuuawa kwa Doris.
"Kwa kweli naheshimu sana dhamana ya wazazi waliowaleta watoto wao hapa shuleni na kuendelea kuwaacha licha ya mkasa huu kutokea kwa sababu naamini haipo sababu kwa mtu mzima kufanya tukio kama hilo kwa mtoto mdogo kama Doris," alisema Luanda. Alisema alipigiwa simu na matroni (mlezi wa wanafunzi) majira ya saa 10 alfajiri ya Juni 12, mwaka huu akiambiwa kuna tukio limetokea bwenini.
Alisema alikwenda haraka shuleni ili akajionee kilichotokea katika bweni hilo.
Baada ya kufika shuleni alisimuliwa mkasa huo na matroni naye akawasiliana na mwenyekiti wa bodi ya shule hiyo, ambaye alitoa msaada mkubwa katika zoezi la kumtafuta marehemu Doris pamoja na kuwajulisha Polisi.
WAZAZI WATOLEWA HOFU
Kwanza, naungana na familia ya Mzee Lutego na Watanzania wote kufuatia msiba mzito wa mwanafunzi wetu, Doris aliyeuawa baada ya watu wasiojulikana kuvamia bweni la wasichana na kuondoka na marehemu na kisha kwenda kumuua kikatili.
"Kwa sasa, ulinzi upo na umeimarishwa,wako walinzi saba wenye silaha za moto na katika suala zima la ulinzi tumepanga kuongeza pia ukuta mrefu utakaojengwa kwa matofali ya saruji ili kutoruhusu mtu yeyote kupita kwa urahisi, " alisema Luanda.
Kwa mujibu wa Luanda, shule hiyo ina wasichana 123 na wavulana 114 wa bweni.
Shule hiyo ina mabweni mawili ya wasichana na mabweni mawili ya wavulana. Pia, ina walezi wa wanafunzi sita.
CHANZO: NIPASHE
No comments:
Post a Comment