ANGALIA LIVE NEWS

Friday, June 17, 2011

Uzembe Simba wasotesha wachezaji Congo

Makosa ya timu ya Simba kwenda bila ya kutanguliza watu nchini Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo kwa ajili ya kuandaa mipango ya kuipokea timu, yaliwagharimu wachezaji wa miamba hao soka nchini kusota kwenye uwanja wa ndege wa Kinshasa kwa saa tano kwa kukosa basi la kuwapeleka hotelini.
Simba ilitua jijini Kinshasa jana saa nne asubuhi tayari kuwakabili wenyeji wao DC Motema Pembe katika mchezo wa marudiano wa Kombe la Shirikisho ambayo utafanyika keshokutwa Jumapili na si Juni 26 kama ilivyoripotiwa katika mtandao wa Shirikisho la Soka la Afrika (CAF).

Huku wakijua kwamba wakati mwingine wenyeji hutumia "mbinu chafu" za kuwaondoa wageni mchezoni, Simba waliingia katika "mtego" huo mwepesi na kujikuta wakibaki uwanjani hapo na kuishia kuwalaumu viongozi wa Chama cha Soka cha nchi hiyo.
Akizungumza na gazeti hili, Mwenyekiti wa Simba, Ismail Aden Rage, alisema kuwa kikosi cha timu hiyo kilifika salama mjini humo lakini kilikaa kwenye uwanja wa ndege wa mji huo kikiwasubiri wenyeji wao bila ya kufahamu wapi waende baada ya kutowaona uwanjani hapo kama kanuni zinavyoelekeza.
Rage alisema wachezaji walisota kwa saa zote hizo tano hadi balozi wa Tanzania nchini humo aliyepo Kinshasa alipookoa jahazi kwa kwenda katika Chama cha Soka cha Congo na kuwaleza juu ya ujio wa Simba, ambapo balozi huyo alielezwa kwamba hawakuwa na taarifa yoyote rasmi ya kutua kwa Simba na ndio sababu viongozi wa DC Motema Pembe hawakuwa wamejiandaa kuwapokea wageni wao.
Alisema kwamba hawakutanguliza ujumbe kwa sababu waliamini ofisa wa ubalozi na taarifa za TFF zitawafikia wenyeji wao na kwamba muda baina ya mechi ya awali na marudiano ulikuwa ni mfupi.
"Kwa kweli tumesikitishwa sana na hali hii, tunaishukuru Wizara ya Mambo ya Nje na ofisi ya ubalozi kwa kutusaidia kuhakikisha timu inapokelewa na kwenda hotelini ili kujiandaa na mechi hiyo ya Jumapili, lakini Simba tuliwajulisha TFF tangu Jumatatu kwamba tutaelekea Kinshana leo (jana)," alisema Rage.
Kuhusu mabadiliko ya mchezo huo kama baadhi ya vyombo vya habari vilivyoripoti jana mchana, Rage, alisema kwamba wao wanachofuata ni taarifa waliyopokea kutoka CAF na kupitia mwakilishi wa Tanzania ambaye ni balozi aliyeko Kinshasa.
"Mechi ni Jumapili kama ambavyo tulielezwa, na balozi wetu alikwenda katika shirikisho lao na kuhakikishiwa kwamba siku ya mchezo haijabadilishwa," alisema Rage.
Aliongeza kuwa hata vyombo vya habari vya nchi hiyo vinaeleza kwamba mechi yao iko keshokutwa na waamuzi wake watakaochezesha wanatoka Gabon.
Rage alisema kuwa wachezaji wote wako katika hali nzuri na suala la kuchelewa kuondoka kwenye uwanja wa ndege halijawasumbua kwa sababu walijiandaa kukabiliana na hali zote.
"Ni kawaida ya kila timu kuweka mazingira ya kuwachanganya wageni, lakini sisi (Simba) hilo lilikuwa ni jambo dogo, wanafahamu wamekwenda huko kupambana na mazingira watakayokutana nayo watapambana nayo," Rage aliongeza.
Alisema pia kesho yeye pamoja na wadau wengine wa timu hiyo wanatarajiwa kuondoka kulekea Kinshasa ili kuungana na wachezaji wao na wanaamini watarejea nyumbani wakiwa na furaha.
Makamu Mwenyekiti wa Simba, Geofrey Nyange 'Kaburu' ndiye ameongoza msafara wa wachezaji 17 na wamepanga kurejea nchini Jumatatu.
Mshambuliaji, Mussa Hassan 'Mgosi' aliipatia Simba ushindi wa goli 1-0 katika mchezo wa kwanza uliofanyika kwenye uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam Jumapili iliyopita.

CHANZO: NIPASHE

No comments: