Furaha Maugo
WAZIRI Mkuu, Mizengo Pinda amesema robo tatu ya watumishi wa umma hawatendi kazi zao kulinganana na matakwa ya taaluma zao na badala yake miongoni mwao wanaegemea zaidi katika vitendo vya rushwa.
Tanzania inakadiriwa kuwa na watumishi wa umma 400,000 na kwa mujibu wa Pinda, 300,000 hawatendi kazi kulingana na taaluma zao hivyo kurejesha nyuma maendeleo ya nchi.Pinda alisema hayo wakati wa akifungua mkutano juu ya maadhimisho ya Siku ya Utumishi wa Umma duniani.
Pinda alisema kuwa suala la mabadiliko na ubunifu wa uongozi katika utumishi wa umma hauwezi kuleta mabadiliko nchini iwapo watumishi wenyewe kuanzia ngazi za juu hadi chini serikalini hawatawajibika na kuepuka vitendo vya rushwa.
Pinda ambaye alitoa maelezo hayo huku akithibitisha kwa kutumia takwimu za tafiti mbalimbali duniani, alisema umefika wakati ambapo watumishi wote wa Serikali wanatakiwa kujituma katika kujua wajibu wao ili kuleta tija sehemu za kazi.
Lakini akawaasa viongozi na watendaji wa ngazi mbalimbali wasijione wao ndio wao bali pia wakubali kukosolewa wakati wowote.“Ili dhana ya mabadiliko na ubunifu wa uongozi katika utumishi wa umma ili ulete mabadiliko ni lazima viongozi wenyewe wakubali kujikosoa na kukosolewa," alisema Pinda ambaye alionekana kutofurahishwa na vitendo hivyo.
Hisia hizo za Pinda alizionyesha kwenye maadhimisho hayo yaliyoandaliwa na Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma.
Kaulimbiu ya maadhimisho hayo ni "Mabadiliko na Ubunifu katika Uongozi wa Utumishi wa Umma yataleta Maisha Bora kwa wote."
Pinda alisema suala la kuheshimu maadili linapaswa kuzingatiwa na watumishi wote wa umma ili waweze kuwa waadilifu na kuleta mabadiliko ya kiuchumi katika nchi zao na sio kuongea tu pasipo kufanya vitendo.
Alisema kuwa dhana ya uwajibikaji kwa watumishi wa umma inatakiwa ieleweke kwa watumishio wote wa Serikali ikiwa ni pamoja na kujua wajibu wao.Alisema kuwa suala la uwajibika ni la kila Mtanzania katika kutekeleza mipango mbalimbali ya maendeleo inayowekwa na Serikali.
Lakini akahimiza kuwa ili mipango hiyo iwe na mafanikio suala la rushwa halina budi kupigwa vita.
Alisema kuwa ikiwa uongozi utakuwa mzuri basi hata utoaji huduma kwa wananchi utakuwa bora na iwapo rushwa itapigwa vita, haki nayo itakuwepo.
Alifafanua kuwa kutokana na ripoti ya tafiti iliyofanywa na taasisi ya kimataifa ya Maendeleo ya Binadamu mwaka 2010 inaonyesha kuwa tatizo la rushwa limekithiri katika taasisi za umma.
Pinda alisema kuwa matokeo ya utafiti huo na utendaji mbovu wa watumishi wa umma ni sababu mojawapo inayosababisha kuathiri ukuaji wa uchumi wa nchi nyingi zinazoendelea, Tanzania ikiwa miongoni.
Alisema kuwa sababu nyingine inayorudisha nyuma maendeleo ni suala la uongozi mbovu au matumizi mabaya ya uongozi.Alisema kwamba ripoti hizo za kimataifa zinaonyesha kwamba Afrika ndiyo yenye watu wengi wenye umasikini zaidi ulimwenguni, hivyo akasema watumishi wa umma wanapaswa kuwajibika ili kuondoakana na hali hiyo.
CHANZO:MWANANCHI
No comments:
Post a Comment