ANGALIA LIVE NEWS

Thursday, June 23, 2011

Simba yatema nyota 10

Mchezaji wa Simba, Joseph Owino
Uongozi wa klabu ya Simba umetangaza kuwaacha wachezaji watatu, Hillary Echessa, Rashid Gumbo na Joseph Owino, huku wengine saba ikisema kuwa inawatafutia timu nyingine za kuchezea kwa mkopo katika msimu ujao wa Ligi Kuu ya Tanzania Bara itakayoanza Agosti 20.

Akizungumza jana, Katibu Mkuu wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), Angetile Osiah, alisema kuwa wamepokea taarifa hiyo kutoka Simba ikiwataja wachezaji ambao wanatafutiwa timu nyingine zinazoshiriki katika ligi kuu kuwa ni Juma Jabu, Haruna Shamte, Ali Ahmed Shiboli, Meshack Abel, Mohammed Kijuso, David Naftali na Salim Gilla.
Katibu huyo alisema kuwa endapo Simba itashindwa kuwapatia timu mpya wachezaji hao saba, watatakiwa wawalipe fidia ndipo nafasi zao zitaweza kujazwa na nyota wengine wapya watakaokuwa wamewasajili kwa ajili ya kuichezea timu hiyo katika msimu mpya, la sivyo kanuni zinasema kwamba itabidi iendelee kuwatumia.
Alisema pia Simba imewaarifu kwamba imewauza wachezaji wake wawili, Patrick Ochan na Mbwana Samatta, katika klabu ya TP Mazembe ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo wakati Abdulhalim Humoud ikimpeleka kwa mkopo wa Azam FC ya jijini.
Pia taarifa hiyo ya usajili iliyotolewa na kusainiwa na Katibu Mkuu wa Wekundu hao wa Msimbazi, Evodius Mtawala, inamaanisha kwamba wachezaji wengine waliobaki akiwemo Mussa Hassan 'Mgosi' na Kelvin Yondan ambao hatma yao baada ya kumalizika kwa msimu ilionekana kuwa shakani, wataendelea kuichezea Simba katika msimu huo mpya.
Nyota wengine ambao wataendelea kuvaa jezi za Simba ni pamoja na Juma Kaseja, Ally Mustapha 'Barthez', Nico Nyagawa, Amir Maftah, Juma Nyosso, Shija Mkina, Jerry Santo na Emmanuel Okwi ambaye yuko mbioni kujiunga na Kaizer Chiefs ya Afrika Kusini.
Klabu hiyo ambayo Jumapili iliyopita ilitolewa kwenye mashindano ya Kombe la Shirikisho la DC Motemba Pembe ya Kongo iko katika hatua za mwisho za kusajili nyota wapya kwa ajili ya msimu huo mpya na endapo ikikamilisha taratibu za kuwasajili itaanza kuwatumia katika mashindano ya Kombe la Kagame Jumamosi ambapo wanafungua na Vital'O ya Burundi.
Baadhi ya nyota ambao wanatarajiwa kuibeba Simba ni pamoja na kiungo wake wa zamani, Haruna Moshi 'Boban' na kipa Wills Ochieng, kutoka Kenya ambaye huenda akawa kipa namba moja endapo atamvutia kocha, Moses Basena.
CHANZO: NIPASHE

No comments: