Yanga
Gor Mahia FC
Wakati nahodha wa timu ya soka ya taifa ya Rwanda 'Amavubi' na klabu ya APR, Haruna Niyonzima, anatarajiwa kutua nchini leo jioni kwa ajili ya kujiunga na mabingwa wa Ligi Kuu ya Tanzania Bara, Yanga, nyota wa Ghana, Keneth Asamoah, alianza cheche zake jana baada ya kuifungia timu yake hiyo goli katika sare ya 1-1 dhidi ya Gor Mahia ya Kenya.
Katika mechi ya kirafiki iliyochezwa kwenye Uwanja wa Sheikh Amri Abeid mkoani Arusha jana, Asamoah, aliifungia Yanga goli la kuongoza, kabla ya Wakenya hao kusawazisha.
Niyonzima ambaye amesajiliwa na Yanga kwa muda wa miaka miwili, anakuja nchini kuanza kuitumikia timu yake hiyo katika mashindano ya Kombe la Kagame ambayo yanaanza kufanyika nchini kuanzia Jumamosi.
Makamu Mwenyekiti wa Kamati ya Usajili ya Yanga, Seif Ahmed, alisema jana kuwa mchezaji huyo ni mali yao na taratibu zilizobaki za kumnasa ni ndogo ambazo wako katika hatua za mwisho kwa kuzungumza na klabu yake ya APR.
Ahmed alisema kuwa tayari Niyonzima ameshakabidhiwa jezi namba nane na wanawataka mashabiki wa Yanga kujitokeza leo kwenye Uwanja wa ndege wa Julius Nyerere kumpokea nyota wao huyo mpya.
Akizungumza katika mahojiano maalumu na kituo cha Redio One juzi, Niyonzima, alisema kwamba anawaomba Wana-Yanga wampe ushirikiano ili aweze kufanya kazi yake iliyomleta kikamilifu nchini.
Niyonzima ambaye ni maarufu kwa jina la 'Fabregas' alisema sasa anataka atambuliwe kwa jina jingine la 'Iniesta' kwa sababu uwezo wake hivi sasa umeongezeka na ndio maana Yanga wamevutiwa naye.
"Nakuja Tanzania kufanya kazi, ninaomba ushirikiano, kucheza Yanga ni moja ya ndoto ambazo nilikuwa nazo kwa muda mrefu," alisema nyota huyo mwenye umri wa miaka 28.
Hata hivyo, Katibu Mkuu wa APR, Adolphe Kalisa, alisema kwamba Niyonzima bado ni mali yao na mkataba wake unamalizika mwezi Oktoba mwaka huu.
NIPASHE pia ilizungumza na Katibu Mkuu wa Chama cha Soka cha Rwanda (FERWAFA), Jules Kalisa, alisema kuwa hadi jana mchana chama chake hakijapokea maombi yoyote ya uhamisho wa kimataifa wa mchezaji huyo.
Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) imetoa angalizo kwa Yanga na Simba kwamba haitaweza kutumia wachezaji iliyowasajili kama hawatakuwa wamekamilisha taratibu za uhamisho wao kwenye mashindano ya Kombe la Kagame.
Wakati huo huo, Shirikisho la Soka Nchini (TFF) limesema kuwa mechi ya mwisho ya hatua ya makundi katika mashindano ya Kombe la Kagame kati ya Elman ya Somalia na mabingwa wa Bara, Yanga, iliyopangwa kufanyika Julai 2, sasa itachezwa siku inayofuata kwenye uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam kwa kuwa Julai 2 kutakuwa na mchezo mwingine utakaowahusisha wawakilishi wa Bara, Simba, watakaoikaribisha Etincelles ya Rwanda.
Kutokana na mabadiliko hayo, mechi za kuanzia hatua ya robo fainali sasa zitaanza Julai 5 huku fainali ya michuano hiyo pia ikichezwa Jumapili ya Julai 10.
Timu ya Vital'O kutoka Burundi iliwasili nchini jana mchana tayari kwa ajili ya kusubiri michuano hiyo ianze wakati El Mereikh ya Sudan, Elman ya Somali na zinatarajiwa kuwasili leo kwa nyakati tofauti.
Mabingwa watetezi, APR, Etincelle zote kutoka Rwanda, Ports (Djibout) zitawasili kesho wakati Bunamwaya ya Uganda ikitarajiwa kutua keshokutwa na St. George ya Ethiopia yenyewe bado haijaeleza itafika lini nchini.
Aidha, TFF inatarajia kukutana na viongozi wa Simba na Yanga ili kupanga mikakati mbalimbali ambayo lengo lake ni kuhakikisha wawakilishi hao wanafanya vizuri na wanalibakisha kombe la michuano hiyo ya nyumbani.
CHANZO: NIPASHE
No comments:
Post a Comment