ANGALIA LIVE NEWS

Wednesday, June 15, 2011

Spika Makinda alikoroga

Kauli ya Spika wa Bunge, Anne Makinda, iliyotafisriwa kama ni kuwabeza watu wa Kariakoo, eneo maarufu kwa biashara jijini Dar es Salaam, jana ilimlazimu kiongozi huyo kuomba radhi.
Makinda akitoa matangazo na ufafanuzi wa masuala mbalimbali bungeni jana, kwanza akieleza kusikitishwa kwake na mwenendo wa wabunge ndani ya Bunge kwa kufanya mambo kinyume cha kanuni zinazokubalika, alifananisha hali hiyo na kama watu wako Kariakoo.

Awali Makinda alisema kuwa alichokuwa amefanya Kiongozi wa Kambi ya Upinzani Rasmi Bungeni, Freeman Mbowe, kwa kutaka mwongozo wa Spika baada ya kupata majibu yasiyoridhisha kutoka kwa Waziri wa Uchukuzi, Omari Nundu, alikuwa sahihi na si kama wanavyofanya wabunge wengine wanaopiga tu kelele za kuomba mwongozo wa Spika wakati mzungumzaji akiwa bado anaendelea kuzungumza kama wako Kariakoo.
Makinda alisema kimsingi, mwongozo wa Spika unaombwa mara tu baada ya tukio husika kumalizika ndani ya Bunge, kama ambavyo alikuwa amefanya Mbowe.
Mbowe alisema katika majibu ya waziri juu ya ujenzi wa njia ya kurukia ndege katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa Kilimanjaro (KIA) alikuwa amepotosha kwa kusema kuwa fedha za ujenzi zilikuwa zimetolewa na aliyekuwa mwekezaji wa uwanja huo.

Mbowe alisema ukweli ni kwamba fedha za ujenzi huo Dola za Marekani milioni nne, zilitolewa na Benki ya Dunia na kujengwa na kampuni ya Federitsi, kwa maana hiyo alimuomba Spika amtake Waziri aondoe majibu ya swali hilo katika hansard za Bunge.
Hata hivyo, Makinda alimtaka Mbowe kuwasilisha kwa maandishi hoja yake ili iweze kufanyiwa kazi kwa kuwa hakuwa na majibu ya papo kwa papo kama ni nani alikuwa sahihi kati yake na Waziri.
Ni katika muktadha huo, Spika aliwataka wabunge kuacha mambo ya ovyo wanapokuwa katika vikao vya Bunge kwani wanatia aibu kwa watu wanaowatazama na wameligeuza Bunge kama Kariakoo.
Vile vile, aliwaasa wasome vizuri bajeti ili watakapochangia wachangie vitu vya msingi badala ya kuzungumza mambo yasiyohusu bajeti.
Baada ya malekezo hayo aliyotoa jana baada ya kipindi cha maswali na majibu kabla wabunge hawajaanza kujadili mpango wa miaka mitano, pia alieleza jinsi alivyosikitishwa na kikao cha juzi jioni.
Alisema alisikitishwa na hali iliyotokea juzi katika kikao cha jioni kilichokuwa kikiongozwa na Mwenyekiti wa Bunge, Mbunge wa Kibakwe, George Simbachawene.
Alisema katika kikao hicho wabunge walifanya vituko vya ajabu kiasi cha yeye (Makinda), kushindwa kuendelea kuangalia mwenendo wa kikao hicho.
“Hii ni aibu kubwa na sijui kwa nini mnajidharaulisha kwa wananchi, mnajua watu huko nje wanawaheshimu sana, sasa mkifanya mambo ya ovyo wanawadharau na mjue haya yote yanayofanyika humu yanaonekana, mimi mwenyewe nilikuwa naangalia, lakini nikashindwa kuendelea kwani nilikuwa naona vitu vya ajabu ajabu,” alisema Makinda na kuongeza kuwa:
“Hapa bungeni kuna utaratibu wa kuzungumza, mtu akiwa anazungumza wengine mnapaswa kumsikiliza, lakini jana (Juzi) mtu mmoja anachangia na wengine wanazungumza utadhani mko Kariakoo.”
Katika kikao cha juzi jioni, kilichoongozwa na Simbachawene, wabunge walikuwa wakiwasha vipaza sauti vyao na kutoa maneno ya vijembe kwa wenzao na wengine wakizomea wachangiaji. Hali hiyo ilimpa wakati mgumu Simbachawene, ambaye alikuwa akilazimika kuwakatisha wabunge waliokuwa wakiomba mwongozo ili kuwabana wazungumzaji walioonekana kuwakejeli wengine.
“ Waheshimiwa wabunge tutumie muda wetu kujadili huu mpango ulio mbele yetu, nikiruhusu kila mtu asimame atoe mwongozo muda wote tutakuwa tumeupoteza bure, naomba tuwe makini,” alisema Spika Makinda.
Baada ya kurusha kombora kwa watu wa Kariakoo, mchana Makinda alilazimika kuomba radhi kutokana na tafsiri iliyoonekana kuwakera baadhi yao.
Kauli kwamba wabunge wasizungumze kama wako Kariakoo ilionekana kuwakera baadhi ya watu waliomtumia ujumbe wakimweleza kuwa amewadhalilisha na kwa kuonyesha kuwa eneo hilo halina maana.
“Nawaomba radhi waliokwazika na kauli yangu, lakini sikumaanisha kuwadharau watu wa Kariakoo, nilichokuwa na sema ni kwamba watu watofautishe kati ya kuzungumza bungeni na mitaani, hapa bungeni kuna taratibu zake za kuzungumza, mtu mmoja akizungumza wengine mnapaswa kumsikiliza tofauti na sehemu kama sokoni Kariakoo ambapo mtu mmoja anaweza kuwa anazungumza na wengine wanazungumza wakati huo huo.

AMTIMUA MBUNGE
Katika hatua nyingine, Makinda jana alimtoa nje ya ukumbi wa Bunge Mbunge wa Kasulu Mjini (NCCR-Mageuzi), Moses Machali, kutokana na kuvaa mavazi yasiyoruhusiwa na kanuni za Bunge.
Machali aliingia katika ukumbi wa Bunge katika kikao cha jioni jana, akiwa amevaa kaunda suti ya mikono mifupi ya rangi ya bluu na suruali nyeusi.
Baada ya mjadala kuhusu Mpango wa Maendeleo wa Taifa kuanza, Mbunge wa Karagwe (CCM), Gosbert Blandes, alisimama na kuomba Mwongozo wa Spika kwa kutumia kanuni ya 146 vifungu (1), (2) na (3) sehemu (a) na (b) vinavyoeleza namna mbunge, spika na naibu spika wanavyotakiwa kuvaa wakiwa ndani ya ukumbi wa Bunge.
Vifungu vya kanuni hiyo vinaeleza: “Mbunge anayeingia kwenye ukumbi wa Bunge atawajibika kuvaa mavazi ambayo ni safi na yenye kuhifadhi heshima yake, hadhi ya Bunge na utamaduni wa nchi, kama ilivyoainishwa katika kanuni hii.”
“Vazi Rasmi la Spika na Naibu Spika litakuwa ni joho lenye kuonyesha rangi za Bendera ya Taifa, Nembo ya Taifa na baadhi ya mazao makuu nchini, lililoshonwa maalumu kwa ajili hiyo, ambalo litavaliwa juu ya vazi lolote ambalo ni vazi rasmi kwa wabunge.”
“Vazi rasmi kwa Wabunge litakuwa lolote kati ya yafuatayo:-Kwa Wabunge wanawake:- vazi lolote la heshima yaani ambalo si la kubana mwili, lisiloonyesha maungo ambayo kwa mila na desturi za Kitanzania hayapaswi kuonyeshwa na ni refu kuvuka magotini; gauni la kitenge au blauzi inayovaliwa na kitenge au sketi ya rangi yoyote; kilemba cha kadri au mtandio; vazi linalovaliwa wakati wa eda.”
“Kwa Wabunge wanaume:- suti ya Kiafrika au safari ya mikono mirefu au mifupi yenye ukosi au shingo ya mviringo na yenye fulana au bila fulana ndani ya rangi moja, isiyokuwa na nakshi, pamoja au bila baragashia; vazi la kimwambao yaani kanzu rasmi na nadhifu, koti, baragashia na makubadhi au viatu; suti kamili ya kimagharibi ya rangi ya kadri isiyomeremeta; koti aina ya blazer na tai, pamoja na suruali yoyote ya heshima; au”
“Tarabushi na kilemba cha Singasinga, au kilemba chochote kinachovaliwa kwa mujibu wa masharti ya imani au mila.”
Baada ya kusoma kanuni hiyo, Blandes alimtaja Machali kwamba, amevaa mavazi, ambayo yanakiuka kanuni hiyo.
Baada ya Blandes kumtaja mbunge huyo kwa jina, Spika alimuamuru (Machali) kutoka nje ya ukumbi wa Bunge na kwenda kuvaa mavazi mengine.

MJADALA WA BAJETI LEO
Wakati huo huo, wabunge leo wanaanza mjadala wa siku tatu kujadili Bajeti ya Serikali kwa mwaka ujao wa fedha wa 2011/2012, ambao unaonekana utakuwa na mvutano mkubwa.
Hii inatokana na bajeti iliyowasilishwa na Waziri wa Fedha na Uchumi, Mustafa Mkulo, Juni 8, mwaka huu, kugusa eneo la posho, ambalo limezua mapambano makubwa bungeni.
Mapambano hayo yanahusisha baadhi ya wabunge, yakishikiwa bango zaidi na Mbunge wa Kigoma Kaskazini (Chadema), Zitto Kabwe, wanaharakati, Spika wa Bunge, Anne Makinda na serikali.
Hali hiyo inaonekana kumweka Zitto katika hatari ya kufukuzwa bungeni.
Tishio hilo limekuja baada ya Zitto, kutoa kauli kuwa kuanzia sasa hatasaini daftari la mahudhurio kama njia ya kukwepa kulipwa posho za vikao, ambazo ameshatangaza kwamba, hazitaki.
Bajeti hii ya Waziri Mkulo kama zilivyo nyingine za miaka ya nyuma, itapita, lakini dalili zote zinaonyesha kuwa itakumbana na mikwaruzo.
Hali hiyo ilianza kujitokeza baada ya baadhi ya wabunge na wananchi wa kada mbalimbali, wakiwamo wachumi na wafanyabiashara, hasa wamiliki wa viwanda kupitia shirikisho lao (CTI), waliozungumza baada ya Waziri Mkulo kuwasilisha Bajeti yake bungeni, kuikosoa.
Bajeti hiyo inaonekana serikali kuifilisi kambi ya upinzani kwa hoja ya kupunguza matumizi yake, kufuatia maamuzi magumu yaliyotangazwa na Waziri Mkulo, baada ya kugusa posho, magari, samani na safari za nje za watumishi wa serikali.
Kwani kwa maamuzi hayo, serikali imesitisha ununuzi wa magari mapya aina zote isipokuwa kwa kibali maalum cha Waziri Mkuu; na kufuta posho zote za watumishi wa serikali ambazo hazina tija. Pia kupiga marufuku ununuzi wa samani kutoka nje, kupunguza matumizi ya mafuta kwa magari ya serikali, kuondoa semina na warsha, kupunguza matumizi ya fedha kwenye sherehe na maonyesho.
Mbali na maamuzi hayo, ambayo ni miongoni mwa hoja ambazo zimeshikiliwa bango na kambi ya upinzani, pia Waziri Mkulo akiwasilisha bajeti hiyo alisema serikali inakusudia kufuta mlolongo wa kodi kwenye petroli.
Alisema kiwango cha upunguzwaji kitatolewa Juni 23, mwaka huu wakati wa kuwasilisha muswada wa bajeti.
Katika bajeti hiyo, ambayo serikali inakusudia kutumia Sh. trilioni 13.525,895, kati yake matumizi ya kawaida yakiwa ni Sh. trilioni 8.600,287 na maendeleo Sh. trilioni 4.924,608, pia kodi mbalimbali zimepandishwa kwa kiwango cha asilimia 10.
CHANZO: NIPASHE

No comments: