ANGALIA LIVE NEWS

Wednesday, June 15, 2011

JK aenda kuhudhuria mkutano wa ILO Uswisi

Rais wa Jakaya Kikwete ni miongoni mwa viongozi saba duniani ambao watakuwa wageni maalum kwenye Mkutano wa 100 wa Shirika la Kazi Duniani (ILO) ulioanza Juni Mosi mwaka huu Geneva, Uswisi.
Rais Kikwete ambaye aliondoka, jana , kwa ziara ya siku tatu nchini Uswisi, amepangiwa kuhutubia mkutano huo leo, akiwa mgeni maalum wa mwisho kuhutubia mkutano huo unaomalizika keshokutwa.

Viongozi wengine walioalikwa kuhutubia mkutano huo ni pamoja na Rais wa Jamhuri ya Indonesia, Susilo Bambang Yudhoyono na Kansela wa Ujerumani, Angela Merkel ambao walihutubia mkutano huo jana.
Kwa mujibu wa taarifa ya Ikulu, viongozi wengine watakaohutubia mkutano huo unaojumuisha washiriki kutoka nchi zote 183 wanachama wa ILO ni Waziri Mkuu wa Russia, Vladimir Putin; Rais wa Jamhuri ya Uswisi, Micheline Calmy-Rey; Rais wa Finland, Tarja Kaarina Halonen, na Waziri Mkuu wa Mamlaka ya Palestine, Salam Fayyad.
Shughuli za mkutano huo wa 100 tokea kuanzishwa kwa ILO mwaka 1919, unaodhuhuriwa na watu 7,000 unashirikisha viongozi wa nchi na serikali wa zamani, mawaziri wa nchi mbalimbali, taasisi za kimataifa, na taasisi za kiraia.
Mada za jumla zinazozungumzwa katika mkutano huo ni pamoja na kiwango kikubwa cha ukosefu wa ajira duniani, zahama ya kimataifa ya ukosefu wa ajira miongoni mwa vijana, jinsi ya kuongeza kiwango cha kulinda watu zaidi duniani kupitia mifuko ya hifadhi za kijamii, na haki za wafanyakazi na watumishi kazini na hasa zile za watumishi wa ndani.
CHANZO: NIPASHE

No comments: