SALAM Marafiki! Ni imani yangu kwamba mtakuwa wazima wa afya njema na mnaendelea na majukumu yenu kama kawaida. Nawashukuru sana kwa kuchagua kusoma maana hakuna kitakachopotea, zaidi mtaongeza uzuri juu ya uhusiano na mapenzi.
Mada ya wiki iliyopita ilikuwa na changamoto sana kwa wasomaji, nilipokea simu, waraka pepe na ujumbe mfupi wa maneno (SMS) kwa wingi sana kutoka kwa wasomaji mbalimbali wakichangia mada ambayo kimsingi ilitokana na swali alilouliza msomaji wangu wa Kihesa, Iringa.
Mada ya wiki iliyopita ilikuwa na changamoto sana kwa wasomaji, nilipokea simu, waraka pepe na ujumbe mfupi wa maneno (SMS) kwa wingi sana kutoka kwa wasomaji mbalimbali wakichangia mada ambayo kimsingi ilitokana na swali alilouliza msomaji wangu wa Kihesa, Iringa.
Kwa bahati mbaya kuna baadhi ya akina kaka walielewa vibaya, wakaamini hiyo ilikuwa nafasi yao ya kuanzisha uhusiano na dada huyo. Kwa ujumla nilipata usumbufu mkubwa sana, wakitaka niwatumie namba za simu za dada huyo.
Kuna baadhi niliwajibu kwa SMS, waraka pepe na hata kuzungumza hewani, lakini kwa faida ya wale ambao mliomba kutumia namba za simu za dada huyo, nawajibu moja kwa moja hapa chini.
MAPENZI HAYAPO HIVYO
Rafiki zangu, huwezi kumpenda mtu ghafla ambaye hujamuona. Hizo naziita ni tamaa na kwa hakika ni nadra sana kati ya ninyi mliotuma maombi ya kupewa namba zake kuwa mume sahihi wa dada yule.
Wengi inaonekana walivutiwa zaidi na maelezo yake, wakiamini kwamba kutokana na matatizo aliyokuwa nayo, hasa kwa kuwa alisema wazi kuwa ana pesa, wakaona ‘wangeponea’ hapo.
Lakini inawezekana waliamini kutokana na udhaifu wake wa kuachwa na wanaume wengi, wakaamini ni nafasi yao kupata nafasi ya bwerere, jambo ambalo si sahihi. Hisia za mapenzi hazipo hivyo, hizo ni tamaa tu!
Rafiki zangu, ni aibu sana kama kweli wewe ni mdau wa ukurasa huu, halafu uoneshe udhaifu wa ghafla wa kumtamani mwanamke ambaye hujamuona kwa vile tu ameomba ushauri. Naamini hapa unapata masomo kila wiki ambayo yanakujenga na kukuongezea ufahamu wako zaidi katika mambo ya mapenzi, hivyo unapaswa kuwa mwalimu kwa wengine.
Hata hivyo, isingekuwa rahisi kutoa namba ya simu ya mtu ambaye hajatoa ruhusa yake. Katika mada zilizopita niliwahi kuandika mada yenye kichwa; Usikubali hisia zako zikuongoze!
Katika mada hiyo nilifafanua kwa undani zaidi. Sina shaka nitakuwa nimeeleweka vyema na wasomaji wangu (hasa wale waniomba namba za dada huyo) na sasa watakuwa na kitu kipya vichwani mwao. Sasa twende kwenye mada yetu ya leo.
Leo nazungumzia juu ya ahadi ambazo wenzi hutoleana wanapokutana mara ya kwanza. Kwa bahati mbaya sana, wengi wanapokutana mara ya kwanza, hutoa ahadi yoyote ilimradi iwe ya kumvutia muhusika amkubali kuwa naye.
Rafiki yangu mpenzi, hebu tuzungumze na uwe mkweli katika hili; Siku ya kwanza kukutana na mpenzi wako mlimuahidi nini? Je, ahadi zako zimetekelezeka? Uhusiano wako ukoje sasa hivi?
Ngoja nikuambie kitu ndugu yangu, inawezekana upo katika uhusiano (ndoa) na mwenzi wako, lakini kila siku mnagombana, unajaribu kuweka mambo sawa, lakini baada ya siku mbili, tatu ugomvi unarudi pale pale, umejiuliza tatizo ni nini?
Subiri nikumegee siri, utafiti usio rasmi niliofanya kwa muda wa mwaka mmoja sasa, unaonesha kwamba, ugomvi mwingi unaotokea baina ya wapenzi/wanandoa husababishwa na ahadi! Yaani unakuta mtu alipokutana na mpenzi wake mara ya kwanza alimpa ahadi kedekede, kwamba atamfanyia hili na lile au hatafanya hivi na vile, lakini wanapokuwa kwenye uhusiano anajisahau na kufanya kinyume na makubaliano, hapo unaibuka mtiti!
Hili ni somo ambalo litakuweka sawa wewe ambaye upo kwenye uhusiano kwa muda mrefu na mwenzi wako, kukuweka sawa na kukufanya ukumbuke makosa yako ili upate nafasi ya kutuliza hali ya hewa katika penzi lenu.
Hata hivyo, itawasaidia zaidi wale ambao bado hawajaingia kwenye uhusiano, kujua madhara ya kuahidi ahadi za uongo. Kwanza, hebu tuone mambo ya kuzingatia kabla ya kutoa ahadi kwa mpenzi wako unapokutana naye kwa mara ya kwanza, halafu baadaye tutaona ahadi ambazo ‘feki’ zinazotolewa na wenzi wanapokutana kwa mara ya kwanza, halafu zikaleta matatizo baadaye.
KWANINI UNAAHIDI?
Eti marafiki, kwani lazima unapokutana na mwenzi kwa mara ya kwanza utoe ahadi? Unaahidi nini? Kwani unataka ubunge mpaka uanze kutoa ahadi? Kimsingi kuahidi, ni sawa na kuonesha jinsi ambavyo una mashaka ya kukataliwa, ndiyo maana unakimbilia kutoa ahadi.
“Kwa kweli nitabadilisha maisha yako...kwanza sisi kwetu mambo safi...nafanya kazi kwenye ofisi ya mdingi na mimi ndiye director. Kwanza nadhani itabidi nifanye mchakato uanze kazi pale! Hivi elimu yako kiwango gani vile?”
Rafiki yangu, yote hayo ya nini? Baadhi ya ‘mbumbumbu’ au wapenda ahadi, watakuona wa maana na inawezekana kabisa ukapewa nafasi ya kuwa naye, lakini uliyosema ni ya kweli? Ataingia kwenye uhusiano akiwa na matarajio makubwa sana kichwani mwake, kumbe si kweli umemwingiza mwenzio ‘chaka!’
Mada inaendelea rafiki zangu, lakini kutokana na ufinyu wa nafasi, naomba niweke kituo kikubwa hapa, wiki ijayo tutaendelea. Bila shaka utavuna mambo sana, SI YA KUKOSA!
Joseph Shaluwa ni Mshauri wa Mambo ya Mapenzi ambaye anaandikia magazeti ya Global Publishers, ameandika vitabu vya True Love na Let’s Talk About Love vilivyopo mitaani. Unaweza kumtembelea kwenye mtandao wake;www.shaluwanew.blogspot.com au jiunge naye kwenye facebook.
No comments:
Post a Comment