Katibu Mkuu wa TFF, Angetile Osiah
Timu ya soka ya Tanzania, Taifa Stars, itacheza mechi ya kirafiki ya kimataifa dhidi ya Palestina ugenini Agosti 10, Shirikisho la Soka Nchini (TFF) limesema jana.
Nchi nne za Palestina, Qatar, Shelisheli na Umoja wa Nchi za Kiarabu (UAE), zilituma maombi ya kutaka kucheza mechi na Stars katika siku hiyo inayotambuliwa na Shirikisho la Soka Duniani (FIFA), lakini Tanzania imechagua kucheza na Palestina.
Akizungumza jana na gazeti hili, Katibu Mkuu wa TFF, Angetile Osiah, alisema kuwa kocha na uongozi wa shirikisho hilo umeamua kuipeleka Taifa Stars nchini Palestina kutokana na wenyeji wao kuonyesha kuwahitaji zaidi tofauti na nchi nyingine tatu ambazo ziliomba kucheza na Tanzania.
Osiah alisema kuwa wameamua Stars icheze na Palestina ambao nao waliwahi kuja nchini kutokana na kuthibitisha kwamba wako tayari kwa mchezo huo tofauti na nchi hizo nyingine ambazo maandalizi yake yanaandaliwa na mawakala mbalimbali wa mechi za kimataifa.
Alisema kwamba kabla ya kufikia maamuzi ya kucheza na Palestina, TFF iliwaandikia wote walioomba kucheza na Taifa Stars kutaka kufahamu ni jinsi gani timu hiyo itahudumiwa lakini Palestina ndio waliotoa jibu la haraka na kuridhishwa na maelezo yao kwenye barua waliyowaandikia.
Alisema pia licha ya maombi hayo, TFF haikuwa imeomba mechi yoyote kama ambavyo kocha, Jan Poulsen, alivyoelekeza kwamba anahitaji kuvaana na nchi zilizoendelea na zilizoko nje ya ukanda wa Afrika Mashariki na Kati.
Hata hivyo, Osiah alishindwa kuthibitisha kama Shelisheli ambayo yenyewe imeomba mechi yake dhidi ya Stars ichezwe hapa nyumbani mwishoni mwa mwezi Julai kwa sababu shirikisho hilo linakabiliwa na ukata.
"Mechi dhidi ya Shelisheli itaamuliwa na hali ya uwezo tutakaokuwa nao,'' alisema katibu mkuu huyo wa TFF.
Alisema kuwa mchezo huo utakuwa ni sehemu ya maandalizi ya kuivaa Morocco katika mechi za kuwania tiketi ya kucheza fainali za Kombe la Mataifa ya Afrika mwakani nchini Gabon na Equartorial Guinea.
CHANZO: NIPASHE
No comments:
Post a Comment