Waziri wa Fedha, Mustafa Mkulo
Posho za wabunge sasa ni zogo kubwa. Waziri wa Fedha, Spika wa Bunge, wabunge na wanaharakati wanakamatana koo juu ya uhalali wa kuendelea kulipwa huku wananchi wakitaabika kwa umaskini wa kutupwa.
Moto mpya wa kupinga posho wanazolipwa wabunge jana ulizidi kusambaa kwa kasi, baada ya wana harakati kuingilia kati kutaka zifutwe na kutangaza kampeni ya kuzipinga.
Kampeni maalum ni ya kukusanya na kupokea maoni ya watu milioni moja kote nchini, kwa lengo la kushinikiza kufutwa posho zisizo na tija za wabunge na watumishi wa serikali, inaanza rasmi leo.
Kampeni hiyo inaendeshwa na Taasisi ya Muungano wa Maendeleo (ADO) na inataka posho hizo zisaidie katika shughuli za kijamii. Mkurugenzi Mtendaji wa ADO, Ntamilyango Buberwa, aliwaambia waandishi wa habari kuwa ukusanyaji na upokeaji wa maoni utafanyika kabla ya kusomwa bajeti ya Wizara ya Fedha na Uchumi kisha watayawasilisha kwa Rais Jakaya Kikwete wakiamini ni kiongozi makini mwenye kujua umuhimu wa maendeleo nchini.
Alisema wanaamini baadhi ya malipo wanayolipwa wabunge na watumishi wa serikali, ni kinyume cha taratibu kwani zinalenga kulipia kazi ambazo ni sehemu ya majukumu yao ya kila siku ambayo inalipwa kupitia ujira wa mishahara yao ya mwezi.
Alisema vitendo vya wabunge na viongozi wa serikali kutaka kuendelea kupatiwa posho za vikao na misimamo tofauti inayotolewa na viongozi wa Bunge, akiwamo Spika, vinawapa shaka na utayari wa uzalendo wao katika kusimamia maslahi ya umma. Buberwa alisema viongozi hao wanawapa Watanzania wasiwasi wanapotoa misimamo inayosigana na kwamba, dhana ya namna hiyo, ni kukosa dhamira ya kweli katika uwakilishi wao kwa maendeleo ya wananchi.
Alisema katika nchi kama Tanzania, ambako kima chini cha chini cha mshahara wa mfanyakazi hakizidi Sh. 160,000 kwa mwezi, ni aibu ya aina yake kwa mbunge kukubali kulipwa pesa za walipakodi maskini Sh. 150,000 kila siku kwa vikao, ambazo ni sawa na Sh. 1,050,000 kwa wiki, nje ya mishahara yao.
TGNP: NI KOSA KULIPA POSHO HIZO
Mtandao wa Jinsia Tanzania (TGNP) umesema ni kosa kwa serikali kuendelea kutoa posho kwa wabunge na viongozi wengine wa ngazi za juu serikalini huku wafanyakazi wa ngazi ya chini wakipata mshahara usioweza kukidhi mahitaji yao.
Hayo yalisemwa jana jijini Dar es Salaam na Mkurugenzi Mtendaji wa TGNP, Usu Mallya, alipokuwa akitoa tathmini ya bajeti ya mwaka huu.
Mallya alisema sehemu yoyote duniani kipimo cha kupanga kima cha chini cha mshahara kwa wafanyakazi huwa ni gharama ya mahitaji muhimu ya mfanyakazi wa ngazi ya chini kuyapata kwa kutumia mshahara wake.
" Hii ndiyo inayofanyika duniani kote. Sasa sisi kama wanamtandao, tunapinga kwa nguvu zote kutoa posho ya aina yoyote kwa wabunge kama ilivyo kwa maofisa wengine wakubwa wa serikali, kwa kuwa wana hali nzuri kimapato ukilinganisha na wafanyakazi wa ngazi ya chini na hasa walio pembezoni, wanawake wakiwemo,” alisema.
MKULO AWABEZA WANAOZIPINGA
Wakati wanaharakati wakipinga, Waziri wa Fedha, Mustafa Mkulo, amesema hana uwezo wa kuondoa posho za Mbunge wa Kigoma Kaskazini (Chadema), Zitto Kabwe, na wenzake wa NCCR- Mageuzi wanaotaka ziondolewe.
Akizungumza na NIPASHE mjini Dodoma jana, Mkulo alisema Baraza la Mawaziri pekee ndilo lenye uwezo wa kutengua sheria hiyo na si yeye hivyo wanaomtaka azihamishe hawajui wanachosema.
" Mimi Mkulo sina uwezo wa kubadilisha maamuzi ya baraza la mawaziri hata siku moja, suala likishaamriwa kule mtu binafsi huna uwezo wa kulitengua, labda niende kwenye baraza hilo nijenge hoja wakubali,” alisema.
Katika hatua nyingine, Mkulo alishangaa hatua ya wabunge wanaokataa posho hizo zipelekwe kwenye majimbo yao badala ya kuiachia serikali uamuzi.
" Kama wanataka zifutwe waseme, lakini kusema ziende sehemu fulani haina maana, kama kweli wanataka kubana matumizi waseme posho hizi zifutwe na wafuate taratibu maana ziko kwa mujibu wa sheria za nchi,”alisisitiza Mkulo.
" Zitto ni mjumbe wa kamati ya uongozi ya Bunge kama kweli hataki hizi posho angesema kule zikatwe sasa mbona alishiriki kuzipitisha? "alihoji.
Wabunge wa Chadema na wengine wanne wa NCCR-Mageuzi wote kutoka majimbo ya Mkoa wa Kigoma, wanataka posho hizo zifutwe.
Akizungumzia posho hizo za vikao, Mbunge wa Vunjo (TLP), Agustine Mrema, alisema kwa kuwa serikali ilishatangaza katika bajeti yake kuwa itapunguza posho zisizo za lazima, basi itaangalia kama posho za wabunge nazo hazina ulazima.
" Mimi naunga mkono posho zisizo za lazima ziondolewe, kama serikali itaona posho za wabunge si za lazima na ikaziondoa mimi sina neno, wakiona mbunge anaweza kuja hapa Dodoma na akafanya kazi zake bila kuhitaji hiyo posho sawa mimi nasubiri uamuzi wa serikali,” alisema.
Mbunge wa Wawi (CUF), Hamad Rashid, alisema kuwa: " Katiba inatamka wazi kwamba mtu akifanya shughuli hii malipo yake ni haya sasa tatizo ni nini."
Alisema kama wanaopokea posho hizo wanaona hawana haja nazo waandike hundi na kuzirejesha zilikotoka badala ya kupiga kelele kwenye vyombo vya habari.
" Hizo ni cheap politics (siasa uchara) ambazo mimi binafsi sizitaki na kamwe sitazishabikia, mbona wanapokwenda kwenye halmashauri kule wanasaini posho iweje wakija huku ndipo waseme hawazitaki, maoni yangu ni kwamba tukiamua kubadili sheria na kuziondoa sawa sitakuwa na tatizo, lakini kwa kuwa sasa hivi ziko kisheria tatizo linatokea wapi, ” alisema Rashid.
Spika wa Bunge, Anne Makinda, alisema kuna watu wanapotosha kuwa mshahara wa mbunge ni zaidi ya milioni saba wakati mshahara halisi ni Sh. milioni 2.5 na wanakatwa Sh. 900,000 kila mwezi kwa ajili ya mikopo ya magari waliyochukua.
Imeandikwa na Sharon Sauwa na Joseph Mwendapole, Dodoma; Muhibu Said na Raphael Kibiriti, Dar.
CHANZO: NIPASHE
No comments:
Post a Comment