ANGALIA LIVE NEWS

Tuesday, June 14, 2011

Polisi yapiga wanafunzi mabomu

Askari wa Kikosi cha Kutuliza Ghasia (FFU) wakiwadhibiti Wanafunzi wa Kitivo cha Sanaa na Lugha cha Chuo Kikuu Dodoma (Udom), baada ya kufanya maandamano ya kwa lengo la kudai posho 
Jeshi la Polisi limetumia mabomu kuwatawanya wanafunzi wa Chuo Kikuu cha Dodoma (Udom) na wa Shule ya Sekondari Mbezi, jijini Dar es Salaam.

Katika tukio la kwanza, jana milio ya mabomu ilisikika katika eneo la Bunge mjini Dodoma, baada ya polisi kuwatawanya wanafunzi wa Chuo cha Sayansi ya Jamii cha Udom, kuandamana hadi bungeni wakitaka kumuona Waziri Mkuu, Mizengo Pinda na Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Ufundi, Dk. Shukuru Kawambwa, kushinikiza kulipwa posho za mafunzo kwa vitendo.
Mapema asubuhi, wanafunzi hao walikusanyika katika viwanja vya Nyerere Square mjini hapa na ilipofika saa 4.00 asubuhi walianza kuandamana hadi bungeni wakishinikiza kumuona Pinda na Kawambwa.
Hata hivyo, jitihada zao zilishindikana baada ya polisi kuwaamuru kuondoka katika eneo hilo na walipokaidi amri hiyo ndipo walipopigwa kwa mabomu ya machozi yaliyofanya wanafunzi hao kukimbia ovyo.
Katika maeneo mbalimbali ya mji wa Dodoma hususan bungeni kulikuwa na ulinzi mkali wa askari wa Kikosi cha Kuzuia Fujo (FFU), waliokuwa wamebeba bunduki na mabomu ya kurusha kwa mkono.
Pia asubuhi daladala zilitakiwa kutopita katika barabara ya Dar es Salaam ambayo ndiyo inayotumiwa na magari hayo siku zote na badala yake walielekezwa kutumia barabara mbadala.
NIPASHE ilishuhudia askari wa kikosi cha usalama barabarani akiwataka madereva wa daladala kutopita barabara hiyo na badala yake kuzunguka eneo la Bunge.
Aidha, baadhi ya wenye maduka katikati ya mji waliamua kuyafunga kwa kuhofia kuwa vurugu hizo zingewaathiri.
Akizungumza na NIPASHE, Rais wa Serikali ya Wanafunzi Kitivo cha Sanaa ya Lugha na Sayansi za Jamii, Mwakabinga Philipo, alisema wameamua kuandamana kutokana na kutotekelezewa madai yao ambayo ni kupatiwa fedha za mafunzo kwa vitendo ambazo wamekuwa wakiahidiwa, lakini hawapatiwi.
Alisema Seneti ya Udom Juni 8, mwaka huu ilitoa taarifa kuwa tatizo la madai ya fedha za mafunzo kwa vitendo halitatokea tena. Alifafanua kuwa licha ya ahadi hiyo, wanashangazwa kuona mpaka sasa haitekelezeki ndio maana waliamua kwenda bungeni kuonana na viongozi hao.
Mwakabinga alisema kutokana na ahadi zilizotolewa na viongozi hao ndio maana waliamua kwenda kuonana na Pinda na Kawambwa ili kupata ufumbuzi wa fedha hizo. Baada ya kutawanywa na polisi, ilipofika majira ya saa 6:00 mchana, wanafunzi hao walikusanyika tena katika viwanja vya Nyerere wakidai kuwa Waziri Kawambwa angekwenda kuzungumza nao.
Baada ya wanafunzi hao kukusanyika, Mkuu wa Mkoa wa Dodoma, James Msekela, alifika katika eneo hilo kwa lengo la kuwatuliza, lakini jitihada zake ziligonga mwamba baada ya kumzomea na kumwambia “hatukutaki wewe, tunamtaka Waziri.” Baada ya Dk. Msekela kuzomewa, askari wa FFU walianza kuwatawanya wanafunzi hao na kukimbizana nao katika mitaa mbalimbali na kufanikiwa kuwakamata baadhi yao.

20 WATIWA NGUVUNI
Zaidi ya wanafunzi 20 wa Udoma inasemekana walikamatwa na Polisi.
Kaimu Kamanda wa Polisi Mkoa wa Dodoma, Safiel Mkonyi, alithibitisha kutokea kwa vurugu hizo na baadhi ya wanafunzi kukamatwa, lakini aliahidi kuwa atatoa taarifa kamili kuhusiana na tukio hilo baadaye.
Mkonyo alisema asingeweza kutoa taarifa ya kuhusu idadi ya wanafunzi waliokamatwa kwa vile polisi walikuwa wanaendelea kuwakamata wengine na kwamba vurugu hizo zilikuwa zinaendelea.

NAIBU WAZIRI: FEDHA ZAO ZIMETENGWA
Wakati huo huo, Naibu Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Ufundi, Philipo Mulugo, alisema bungeni jana kuwa serikali imetenga Sh. milioni 389 kwa ajili ya kuwalipa posho za mafunzo kwa vitendo wanafunzi wa Chuo cha Udom. Bila kutaja watalipwa lini, Mulugo alisema serikali imeshughulikia programu 13 za wanafunzi wa chuo hicho na kwamba kiasi hicho cha fedha kitatumika kuwalipa wanafunzi 1,062.
Mulugo alikuwa akijibu swali la nyongeza la Mbunge wa Muhambwe, Felix Mkosamali (NCCR-Mageuzi), aliyetaka kufahamu serikali itawalipa lini posho za mafunzo kwa vitendo kwa wanafunzi wa vyuo vya SAUT, Udom ambao wengine hadi wamemaliza chuo, lakini bado hawajalipwa.
Mkosamali ambaye ni mwanafunzi wa SAUT, alisema serikali imekuwa ikisababisha wanafunzi kufanya vurugu kwa wanafunzi kuingia mtaani na kuandamana kudai posho hiyo.
Aliwataka wanafunzi waliomaliza vyuo lakini hawajalipwa fedha zao na wamehakikiwa na Bodi ya Mikopo ya Elimu ya Juu kupeleka majina yao serikalini ili kupata stahiki zao. Katika swali lake la msingi, Mkosamali alisema mara kadhaa wamekuwa wakishuhudia migomo na maandamano ya wanafunzi katika vyuo vikuu nchini na malalamiko yakiwa ni Bodi ya Mikopo.

MBEZI SEKONDARI WAFANYA VURUGU
Katika tukio la pili, wanafunzi 27 wa Shule ya Sekondari ya Mbezi, jijini Dar es Salaam wanashikiliwa na polisi kwa tuhuma za kufanya fujo kwa kufunga Barabara ya Morogoro na kukipiga mawe Kituo cha Polisi Kimara. Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Kinondoni, Charles Kenyela, alisema jana kuwa kundi la wanafunzi wa shule hiyo lilifunga barabara hiyo pamoja na iendayo Mpiji Magoe kwa lengo la kuishinikiza serikali iweke matuta eneo hilo.
Kenyela alisema tukio hilo la kufungwa kwa barabara na wanafunzi hao lilitokana na mwenzao mmoja kufa baada ya kugongwa na gari wiki iliyopita katika eneo hilo.
Alisema wanafunzi hao walifanya fujo hizo majira ya saa 5:45 asubuhi na walikuwa na mawe, fimbo, matofali na vitu vingine.
Alisema askari polisi walilazimika kutumia mabomu ya machozi na kupiga risasi hewani kwa lengo la kuutawanya umati wa wanafunzi ha na raia waliokusanyika eneo hilo huku wakiwa wamebeba aina tofauti ya silaha. Alisema wanafunzi hao pamoja na baadhi ya raia waliungana kwa pamoja na kufanya fujo hizo eneo hilo.
" Sipendi kulihusisha tukio hili na kifo cha mwenzao aliyekufa baada ya kugonjwa na gari, lakini kilichotokea ni kwamba wanafunzi hawa walitoka kwenye shule yao na kuamua kufunga barabara ya Morogoro na ile iendayo Mpiji Majoe kwa lengo la kushinikiza uwekaji wa matuta eneo hilo," alisema. Alisema baada ya wanafunzi hao kufunga barabara hizo, walivamia Kituo cha Polisi cha Kimara kilichopo umbali wa mita 100 kutoka eneo walikofunga barabara na kuanza kurusha mawe.
Alisema juhudi za polisi za kuwatuliza wanafunzi hao wasifanye vitendo hivyo zilishindikana ndipo walipolazimika kutumia mabomu ya machozi na kupiga risasi hewani.
" Wakati askari wakipiga risasi hewani, kuna mwanafunzi mmoja aliripotiwa kujeruhiwa, amekimbizwa Hospitali ya Taifa ya Muhimbili bado hatujafahamu kama amejeruhiwa na risasi au la,” alisema.
Keenja alisema jeshi lake limeimarisha ulinzi eneo hilo na tayari wamewakamatwa wanafunzi 27 ambapo kati yao 12 wamewekwa rumande na waliobaki kukimbizwa Muhimbili kutokana na kupata hofu.
Aidha alisema watu wengine waliojeruhiwa kwa mawe ni Inspekta wa Polisi na Mkuu wa Kituo cha Mbezi na gari moja la mtu binafsi liliharibika kwa kupigwa mawe.
Imeandikwa na Sharon Sauwa, Joseph Mwendapole, Augusta Njoji na Peter Mkwavila, Dodoma; Romana Mallya na Sabato Kasika, Dar.
CHANZO: NIPASHE

No comments: