Rais Jakaya Kikwete (kushoto) akiongoza ujumbe wa Tanzania kwenye mazungumzo ya kiserikali na Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani, Hillary Clinton (kulia) akiwa na ujumbe wake Ikulu jijini Dar es Salaam jana.
Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani, Hilary Clinton, amepongeza juhudi za Tanzania katika kupambana na uharamia na akaahidi kuendelea kuiunga mkono ili kuhakikisha kuna usalama wa uhakika
Akizungumza na waandishi wa habari kwenye mkutano uliofanyika Ikulu, jijini Dar es Salaam jana,Clinton alisema serikali ya Rais Barack Obama inalipa kipaumbele suala hilo.
Alisema serikali ya Marekani itafanya kazi kwa karibu na Tanzania pamoja na nchi nyingine za Kiafrika katika kulitafutia ufumbuzi tatizo la uharamia.
Pia, Clinton alieleza kuridhishwa kwake na uwajibikaji wa serikali kwenye eneo la kuwaletea maendeleo na kuwawezesha wananchi wake.
“Viongozi hapa wana kiwango kikubwa cha uwajibikaji.Tutaendelea kuwaunga mkono na kuongeza mahusiano ya kiuchumi na nchi za kiafrika kupitia kwenye Jumuiya ya Maendeleo ya Kusini mwa Afrika (SADC),” alisema.
Akijibu maswali toka kwa waandishi wa habari, Rais Jakaya Kikwete, aliishukuru Marekani kwa msaada wake wa kupambana na uharamia na hasa katika eneo la kujengea uwezo maofisa nchini wa kupambana na uharamia.
Alisema kumekuwa na ongezeko la tishio la maharamia katika eneo la maji la Bahari ya Hindi ambapo serikali imechukua hatua kadhaa za kukabiliana na uharamia kitu kilichopelekea maharamia 11 kukamatwa na kufikishwa mahakamani katika kipindi cha tokea Machi mwaka jana hadi hivi sasa.
Aidha, alisema katika kipindi hicho majaribio 27 ya uharamia yamefanyika katika eneo la bahari la Tanzania ambapo 13 kati ya majaribio hayo yalikuwa yamelenga kuteka meli kubwa ambapo maharamia walifanikiwa kuteka meli nne.
“Kati ya majaribio hayo,maofisa usalama walifanikiwa kuokoa meli mbili,” alisema.
CHANZO: NIPASHE
No comments:
Post a Comment