Mkuu wa Kitengo cha Mauzo cha Vodacom M-Pesa, Franklin Bagalla (kushoto), akitoa maelezo jinsi ya kutumia M-Pesa kulipia kodi kwa Naibu Kamishna Mkuu wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), Placidus Luoga (katikati) na Mkurugenzi wa Fedha TRA, Salehe Mshoro, kwenye mkutano na waandishi wa habari Dar es Salaam jana. Picha na Salhim Shao
Mosha MAMLAKA ya Mapato Tanzania (TRA), imezindua huduma ya malipo ya kodi kwa kutumia simu za mkononi, kwa kutumia huduma ya M- Pesa.
Akizindua huduma hiyo jana, Mkurugenzi wa Fedha wa TRA, Salehe Mshoro, alisema huduma hiyo itasaidia wateja wao kulipa kodi kwa muda unaotakiwa na kuepuka foleni vituo mbalimbali vya mamlaka hiyo. Mshoro alisema mamlaka kwa kushirikiana na kampuni za simu nchini, zilikaa pamoja na kuamua kuanzisha huduma hiyo, lengo likiwa ni kumsaidia mteja kama ilivyo kwa malipo mengine ya maji na umeme.
“Hii huduma sio ngeni nchini kwa sababu ilishaanza kutumika katika malipo mengine kama maji na umeme, hivyo wateja wetu hawataona tofauti yoyote ile tuna imani wataifurahia,” alisema Mshoro. Alisema wataanza kutumia Kampuni ya Vodacom, ambayo ndiyo iliyomaliza mchakato wa matumizi ya huduma hiyo nchini, lakini baadaye itahusisha kampuni zote za simu.
Mshoro alisema wataanza na malipo ya kodi ya majengo na mapato, mteja akilipa ataweza kuulizia risiti ofisi za TRA, kwa sababu kumbukumbu zinahifadhiwa kwa usalama. Kwa upande wake, Ofisa Mauzo Kampuni ya Vodacom M- Pesa, Franklin Bagalla, alisema wateja watakuwa wanakatwa Sh750 pindi wanapotumia huduma hiyo. Alisema mteja atatakiwa kupiga simu M-Pesa kisha atafuata maelekezo atakayopewa. Mwisho
No comments:
Post a Comment