ANGALIA LIVE NEWS

Tuesday, July 12, 2011

Dini yaibuka ikizuia kutibiwa hospitalini

Na Masau Bwire, Kibaha 

MADHAHEBU ya dini yanayozuia waumini wake kwenda hospitali wala kutumia dawa ya aina yoyote wanapougua yameibuka Kibaha mkaoni Pwani na tayari watu
wawili wameripotiwa kupoteza maisha kwa kuzingatia masharti.

Mchungaji wa kanisa hilo kwa sasa jina tunalihifadhi kwa sababu hatujampata kuzungumzia madai dhidi yake, anadaiwa kuwazuia waumini wake kwenda hospitali wala kutumia dawa ya aina yoyote kwa madai kuwa kufanya hivyo ni kumkufuru Mungu wao mwenye kutibu kila aina ya ugonjwa.
 

Mchungaji huyo anadaiwa kuwakataza waumini wake kushirikiana na mtu yeyote asiyekubaliana na imani yao, hata kama ni wazazi wao.

Muumini wa kanisa hilo akiugua na ndugu wakaonekana kutaka kumhudumia, mahitaji ya kawaida na tiba, mchungaji huyo anamhamisha nyumbani.

Kutokana na imani hiyo, watu wawili, Bw. Tumainieli Mfinanga aliyefariki Oktoba mwaka jana na mkewe Bi. Jane Mathayo aliyefariki mwishoni mwa wiki iliyopita, Julai 9, 2011 kutokana na kukataa kwenda hospitali kutokana na imani hiyo.

Wakazi wa Kibaha na ndugu wa marehemu hao wameiomba serikali ifunge huduma hiyo na kumchukulia hatua mchungaji husika.

Akizungumza na Majira juzi katika mazishi ya Jane ambaye mara baada ya kujiunga na dini hiyo alibadili jina na kuitwa Sarah, ndugu wa marehemu huyo, Bi. Rebeka Mfinanga aliyetengwa na familia baada ya kukataa imani hiyo, alimfananisha mchungaji huyo na Joseph Kibwetere wa Uganda aliyewafungia kanisani waumini wake ili wasubiri siku mwisho kisha kuwateketeza kwa moto.

Alisema ndugu yake alianza kuugua Machi, 2011 na mchungaji huyo akamhamishia nyumbani kwake kumficha ili ndugu wasije wakampa dawa au kumpeleka hospitali hadi ndugu walipochukuwa hatua za kumshtaki polisi ambapo Julai 9, 2011 alimbeba mgonjwa akiwa ajitambui na kumtelekeza jirani na nyumbani kwa Bw. Bright Mfangavo ambaye ni binamu yake.

Alisema akiwa hajitambui alibebwa na kupelekwa katika hospitali ya Tumbi ambapo daktari aliyewapokea aligomba kumchelewesha mgonjwa kumpeleka hospitalini hadi kuzidiwa kiasi hicho.

Pamoja na mgonjwa huyo kupatiwa tiba hospitalini ya Tumbi, haikufaa kitu kwa kuwa ugonjwa ulikuwa umekwishafikia hatua mbaya na akaaga dunia.

Baada ya kifo hicho mchungaji alijulishwa lakini akadai hayamhusu kwa kuwa imani yake inaagiza kuwaacha wafu wazikane wenyewe na kuwataka ndugu wa marehemu watawanyike kila mmoja arudi katika makazi yake kabla hayajawakuta makubwa.

Bw. Mfangavo alisema, kauli hiyo ya mchungaji iliikera familia na kujiandaa kwa vita dhidi yake lakini wakalazimika kutoa taarifa polisi kuhusu vitisho vya mchungaji huyo na hatua walizokusudia kuzichukua dhidi yake.

Alisema mchungaji huyo aliwazuia baadhi ya ndugu wa marehemu ambao ni waumini wake kushiriki katika msiba, akiwamo mama mkwe wa marehemu, Bi. Christina Eliatosha, wifi yake Bi. Justa Mfinanga na mtoto wa marehemu, hadi juzi familia ilipokwenda kuwachukua kwa nguvu nyumbani kwa mchungaji, pamoja na mali za marehemu zilizokuwa zimebaki kwa mchungaji.

Bw. Mfangavo alisema mchungaji huyo alichoma moto baadhi ya mali za marehemu ikiwemo televisheni kwa madai kwamba ni mali haramu kwa kuwa marehemu alizipata kabla hajamjua Mungu.

Katika hatua nyingine, Bw. Mfangavo alililalamikia jeshi la polisi kwa kushindwa kutoa ushirikiano wa aina yoyote katika tukio hilo linalohusisha uhalibifu wa mali.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Pwani, Bw. Ernest Mangu alisema hajapata taarifa yoyote kuhusu tukio hilo na kuahidi kuchukua hatua pale taarifa zitakapomfikia.

Jitihada za gazeti hili kumpata mchungaji huyo ziligonga mwamba kwani alipofuatwa nyumbani kwake hakupatikana na simu yake ya mkononi ilikuwa haipatikani hewani.


Majira

No comments: