ANGALIA LIVE NEWS

Tuesday, July 12, 2011

Mr. II `Sugu` afikishwa mahakamani

Mbunge wa Mbeya Mjini (Chadema), Joseph Mbilinyi maarufu kwa jina la Mr. II Sugu, amefikishwa mahakamani na kusomewa shitaka moja la kufanya kusanyiko la umma kinyume cha sheria.
Sugu alifikishwa jana katika Mahakama ya Hakimu Mkazi ya Mkoa wa Mbeya akiwa pamoja na wenzake wawili ambao kwa pamoja walikamatwa Ijumaa iliyopita na Polisi wakituhumiwa kufanya mkutano wa hadhara bila kuwa na kibali cha Jeshi la Polisi.

Watuhumiwa wengine waliopandishwa kizimbani pamoja na mbunge huyo ni Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) Wilaya ya Mbeya Mjini, John Mwambigija na Katibu mwenezi wa chama hicho, Wilaya ya Mbeya Mjini, Job Zebedayo Mwanyerere.
Akiwasomea mashtaka mbele ya Hakimu Mkazi Mfawidhi wa Mahakama ya Mkoa wa Mbeya, Michael Mtaite, Wakili wa Serikali, Apimaki Mabrouk, alidai kuwa Julai 8, mwaka huu watuhumiwa hao wakiwa katika eneo la Nzovwe jijini Mbeya waliitisha na kufanya mkutano wa umma pasipo kutoa taarifa kwa ofisa wa Polisi wa eneo husika.
Mabrouk alidai kuwa kitendo hicho ni kinyume cha kifungu cha 43 (i) na kifungu cha 46(iia) cha sheria ya Jeshi la Polisi kama ilivyorekebishwa mwaka 2002.
Baada ya kuwasomea shitaka hilo, watuhumiwa wote walikana kufanya kosa hilo na ndipo Hakimu Mteite alipouliza upande wa mashtaka kama ulikuwa na pingamizi lolote kuhusiana na dhamana ya watuhumiwa hao.
Wakili Mabrouk aliiambia mahakama kuwa kwa kuwa shauri linalowakabili watuhumiwa linadhaminika kisheria, upande wa mashtaka hauna pingamizi lolote kuhusiana na dhamana ya watuhumiwa hao.
Aliongeza kuwa upande wa mashtaka umekamilisha upelelezi wa shauri hilo na hivyo akamuomba hakimu kutaja tarehe ya kuanza kusikilizwa kwa shauri hilo.
Hakimu Mteite alisema kuwa baada ya kupitia maelezo ya watuhumiwa wote, amebaini kuwa mshitakiwa namba moja ni Mbunge wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na hivyo akatoa muda kwa mbunge huyo kwenda kuendelea na vikao vya Bunge la bajeti vinavyoendelea mjini Dodoma.
Alisema watuhumiwa wote kabla ya kuondoka mahakamani hapo watatakiwa kujidhamini wenyewe kwa Sh. 100,000 kila mmoja.
Watuhumiwa wote walijidhamini na kuachiwa huru hadi Septemba 6, mwaka huu kesi hiyo itakapoanza kusikilizwa mahakamani hapo.
Wakati kesi hiyo ikitajwa mahakamani, chumba cha mahakama kilifurika wananchi waliojitokeza kushuhudia mbunge wao akifikishwa mahakamani.
Wafuasi wa Chadema waliokuwa wamevalia sare za chama hicho, walijitokeza kwa wingi na kumlaki kwa shangwe na vifijo Mr. Sugu wakati alipotoka mahakamani.
Julai 8, mwaka huu Jeshi la Polisi liliwakamata watu sita wanaodhaniwa kuwa ni wanachama wa Chadema akiwemo Mbunge huyo wakati wakiendelea na mkutano wa hadhara uliokuwa ukifanyika katika eneo la Nzovwe jijini Mbeya.
Mbali na wale waliofikishwa mahakamani jana, wanachama wengine waliokamatwa na Polisi ni aliyekuwa Meneja Kampeni wa Sugu wakati wa Uchaguzi wa mwaka jana, Anyandwile Mwalwiba; mwanachama wa Chadema, Peter Leila na dereva wa Mbunge huyo. Hata hivyo, watuhumiwa hao waliachiwa moja kwa moja Jumamosi iliyopita.
Watuhumiwa hao, akiwemo Sugu kwa pamoja walisota rumande kwa zaidi ya saa 18 kabla ya kupewa dhamana Jumamosi na jana kupandishwa kizimbani.
CHANZO: NIPASHE

No comments: