ANGALIA LIVE NEWS

Tuesday, July 12, 2011

Serikali yashindwa kuwadhibiti wauza mafuta

Ramadhan Semtawa
KATIKA kile kinachoonekana kuwa ni kuzidiwa nguvu na wafanyabiashara wakubwa wa mafuta, Serikali imeshindwa kutoa agizo la mara moja la kushusha bei ya bidhaa hiyo na sasa inakuna kichwa kupata suluhu.

Serikali katika bajeti yake ya Sh13.5 trilioni ya mwaka 2011/12 ilitangaza kushusha kodi ya mafuta ya petroli ili kupunguza kasi ya kupanda kwake kama hatua mojawapo ya kupunguza ukali wa maisha.


Hata hivyo kodi ya mafuta ya taa iliongezwa ili kudhibiti uchakachuaji ambao umekuwa ukifanywa na wafanyabiashara wasio waaminifu.

Kwa mujibu wa Serikali, bei ya petroli ilitarajiwa kuanza kushuka Julai 1, 2011 lakini hadi jana hakukuwa na mabadiliko yoyote zaidi ya bei ya mafuta ya taa kupanda kwa kasi.

Bei ya petroli katika vituo vya mafuta ilikuwa kati ya Sh2,090 na Sh2,130 wakati bei ya mafuta ya taa kwenye vituo hivyo ni kati ya Sh2,080 na Sh2,120 kwa lita moja. Kabla ya Julai mosi, petrol ilikuwa ikiuzwa kwa wastani wa Sh2,060 wakati mafuta ya taa yalikuwa yakiuzwa kwa wastani wa Sh1, 550 kwa lita moja.

Juzi alipoulizwa na Mwananchi kuhusu suala hilo, Waziri wa Fedha na Uchumi, Mustafa Mkullo, alihidi kuwa angetoa ufafanuzi jana baada ya kupata maelezo ya kina juu ya utata huo wa bei kutoka Mamlaka ya Mapato nchini (TRA) pamoja na mamlaka nyingine ili kubaini chanzo tatizo hilo.

Mkulo alisema agizo la Serikali lilikuwa la moja kwa moja kwamba, bei za mafuta zilitakiwa kushuka kuanzia Julai 1, ambayo ni siku ya kwanza ya utekelezaji wa bajeti hiyo .

Alifahamisha kuwa mawasiliano anayotaka kufanya yatamwezesha kujua sababu za utekelezaji wa agizo kushindwa kuanza.

“Ninachotaka kufanya ni kupata taarifa za wataalamu, na mamlaka husika ili niweze kuwa na majibu ya msingi juu ya kwa nini bei ya petroli imezidi kupaa,” alisema Mkulo.

Katika bajeti ya mwaka huu, Serikali ilitangaza maeneo manne ya msingi kama kipaumbele katika bajeti ambayo moja, ni kuongeza nguvu za uzalishaji na kupunguza kodi ya mafuta ya petroli.

Kilio cha watanzania walio wengi kwa muda mrefu ni kutaka Serikali ipunguze bei ya mafuta ya petroli kwa vile imekuwa ikiongeza gharama za maisha, kuanzia usafiri na uzalishaji.

Hata hivyo, hadi jana alipoulizwa kuhusu hatua ambayo Serikali imechukua kuhusu ongezeko hilo la bei ya mafuta, Mkulo alisema bado alikuwa akisubiri maelezo muhimu kuona nini kinasababisha bei kutokushuka.

"Hadi sasa naendelea kufanya mawasiliano na mamlaka husika kupata jibu sahihi, subiri nitafute taarifa za kutosha kisha nitazungumzia  kwa kina jambo hilo," alisema Mkulo na kuongeza:

"Ngoja niendelee kutafuta taarifa za kutosha, watu wangu wanalifanyiakazi kwa karibu jambo hilo.”
Wakati akisoma bajeti, Mkulo alitamba na kuahidi bajeti hiyo ya serikali kwa mwaka 2012/2012, akiita imekuja kumboa mtanzania wa kawaida kwa kumpunguzia ughali wa maisha.

Mkanganyiko wa bei
Mara baada ya bajeti ya Serikali kutangazwa, Mkurugenzi wa Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma za Nishati na Maji (Ewura), Haruna Masebu, alisema Watanzania wangeanza kufaidika na mpango huo wa Serikali kuanzia Julai mosi.

Kwa mujibu wa Masebu, wafanyabiashara wa mafuta walipaswa kushusha bei kwa lazima kwa sababu hata kama sehemu ya mafuta waliyonayo walinunua kwa viwango vya zamani va kodi, walipaswa kuwasiliana na TRA ili warejeshewe kiasi kilichozidi.

Masebu alisema katika kikao na wafanyabiashara wakuu wa mafuta nchini walikubaliana kushusha bei katika vituo vyote ingawa viwango vingeweza kutofautiana kidogo kulingana na bei ya kununua.

Hata hivyo, ilipofika siku hiyo uchunguzi wa Mwanachi ulibaini kuwa bei za petroli na dizeli zilikuwa zikiendelea kupaa, lakini kukawa na ongezeko kubwa katika bei ya mafuta ya taa kwa Sh500.

Mwishoni mwa wiki iliyopita Ewura iilitoa ufafanunuzi tofaito ya bei ya mafuta ya taa na dizeli ikisema: “Marekebisho yaliyofanywa na Serikali katika kodi ya mafuta ya taa ni kuongezeka kutoka Sh52 hadi Sh 400.30 huku mafuta ya dizeli yakipunguzwa kodi kutoka Sh 514 hadi 415, hali inayofanya tofauti kati ya kodi kwa mafuta ya taa na dizeli kuwa Sh 14.70. Awali tofauti ya kodi kati ya mafuta ya taa na dizeli ilikuwa ni Sh 462”.


Kulingana na mkakati wa serikali bei ya mafuta ya taa ingeongezeka kwa wastani wa Sh400 kwa lita.

Mwananchi

No comments: